Tuesday, August 14, 2012

Dk. Ulimboka Awekwa Mafichoni

YABAINIKA HAYUPO NYUMBANI, TAARIFA ZAKE ZAFANYWA SIRI, BABA, NDUGU, MARAFIKI WAGOMA KUZUNGUMZA
WINGU limegubika sakata la kiongozi wa Jumuiya ya Madaktari Nchini, Dk Steven Ulimboka siku moja baada ya kurejea nchini, huku watu wake wa karibu akiwamo baba mzazi, wakigoma kusema chochote kumhusu.

Dk Ulimboka alirejea nchini juzi akitokea Afrika Kusini alikokuwa amelazwa kwa ajili ya matibabu kwa takriban mwezi mmoja na nusu, baada ya kutekwa, kuteswa na kutupwa kwenye Msitu wa Pande nje kidogo na Jiji la Dar es Salaam usiku wa kuamkia Juni 26 mwaka huu.

Ingawa wakati wa ugonjwa wake baadhi ya watu wake wa karibu walikuwa wakitoa maelezo mbalimbali, jana wote waligoma kusema chochote, huku jitihada za gazeti hili kumpata nyumbani kwake zikigonga mwamba.

Baba mzazi wa Dk Ulimboka, Stephen Mwaitenda aliweka wazi kuwa ni vigumu kumwona daktari huyo jana.
Takriban watu wote waliofika nyumbani kwa Mzee Mwaitenda jana kumjulia hali Dk Ulimboka waliambiwa kuwa hayupo nyumbani.

Mwaitenda alilieleza gazeti hili kuwa ana furaha kuwa mtoto wake alirejea nchini salama licha ya kupelekwa Afrika Kusini akiwa taabani kutokana na kipigo.
Alipotakiwa kueleza juu ya kile kilichompata, mtoto wake huyo alisema: "Mungu na Steven mwenyewe (Dk Ulimboka) ndio wanaojua kilichotokea."
Aliongeza: “Kweli nimefurahi kwamba mwanangu amerudi, lakini siwezi kuelezea nini kilimtokea alipotekwa," alisema Mwaitenda.
Alisema Dk Ulimboka hayupo nyumbani na hajui kwamba angerudi wakati gani. "Hata kama angekuwapo, ni vigumu kumwona," alisema.

Kauli ya Katibu wa Madaktari
Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Edwin Chitage alisema madaktari walikuwa hawajaamua nini kingefuata baada ya Dk Ulimboka kurejea nchini.

Alisema hata hivyo, daktari huyo anahitaji muda wa kupumzika kwanza na familia yake.
“Aliporudi jana (juzi) alitumia muda wake kukaa na familia yake, mpaka sasa hatujajua hatua inayofuata. Dk Ulimboka atazungumza wakati mwafaka ukifika,” alisema Dk Chitage.
Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk Namala Mkopi hakutaka kuzungumzia suala hilo akieleza kuwa alikuwa mkutanoni.

Dk Mkopi alitoa kauli hiyo baada ya daktari aliyemtibu Dk Ulimboka wakati wa tukio la kutekwa, Profesa Joseph Kahamba akiwa amesema yeye (Mkopi) ndiye angesaidia kupatikana kwa Dk Ulimboka ili azungumze na waandishi wa habari.

Dk Chitage alipoulizwa nini kinaendelea baada ya Dk Ulimboka kurejea nchini alijibu, "Hakuna kinachoendelea."

Aliendelea, "Leo hakuna kitu, tumepumzika na hata yeye tumemwacha apumzike na familia yake," alisema Dk Chitage.

Alisema Jumuiya hiyo na familia yake wanaandaa mazingira yatakayowezesha Dk Ulimboka kuzungumza na umma kupitia vyombo vya habari.

"Kuhusu hatua zitakazofuata tutaandaa utaratibu na tutawaarifu, juu ya hatua zipi tutachukua ikiwamo hili linaloumiza vichwa vya wengi la mazingira ya kutekwa kwake," alisema Dk Chitage.

Katibu wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Rodrick Kabangila alipoulizwa kuhusu suala hilo alisema yuko safarini na hajui kinachoendelea.

"Nipo Mwanza, nimesafiri na sijui kinachoendelea," alisema.

Alisema MAT itakutana kujadili suala hilo wakati wowote na kwamba utaratibu utaandaliwa kwa Dk Ulimboka kuzungumza na vyombo vya habari.

"Unajua sisi tuliomba kibali cha kuandamana kushinikiza Serikali kuunda tume huru kuchunguza tukio hilo na kuwabaini waliohusika tukakataliwa. Lakini sasa yeye amerudi na anawajua waliomdhuru. Tutaandaa utaratibu, atazungumza nanyi ili watu wote wajue," alisema Dk Kabangila.

Mkurugenzi wa Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), Ananilea Nkya, alisema hakuwa na mawasiliano yoyote na Dk Ulimboka wala hajui kinachoendelea baada ya kuachana naye juzi Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Nyerere.

Polisi wazungumza

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akizungumza kupitia msaidizi wake, alisema kuwa suala la Dk Ulimboka limefungwa na hawezi kulizungumzia tena kwa kuwa lipo mahakamani.

"Kamanda alikwishasema kuwa suala hilo lipo mahakamani hivyo hawezi kulizungumzia," alisema msaidizi huyo.

Alipoulizwa iwapo polisi ilikubali maombi ya madaktari kutaka tume hiyo ivunjwe na iundwe nyingine huru alijibu, "Tume inaendelea na kazi."

"Tume inafanya kazi yake na polisi pia wapo katika kazi zao," alisema na kukata simu.

Wanasiasa
watoa wito

NCCR-Mageuzi, CUF na Democratic (DP) vimemtaka Dk Ulimboka kuwataja watu waliomteka na kumpiga.

Wito huo ulitolewa jana kwa nyakati tofauti na Katibu Mkuu wa NCCR-, Samwel Ruhuza, Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro na Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila.

“Atumie roho yake na dhamira yake kuwataja watu waliomfanyia unyama ule ili jamii ijue na pengine ndio utakuwa mwisho wa watu kufanyiwa vitu vya aina hii,” alisema Ruhuza.

Ruhuza alisema kuwa kiongozi huyo wa madaktari amerejea huku akiwa na afya njema, lakini bado ana deni kwa watu wasiopenda vitendo vya unyanyasaji.

“Ndiyo maana nikasema azungumze jambo hili kutoka ndani ya moyo wake,” alisema Ruhuza.

Mtikila alisema licha ya kwamba Dk Ulimboka anatakiwa kuwataja waliomfanyia vitendo hivyo, yaliyomkuta yanatakiwa kupelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki za Binadamu.

“Nimeshazungumza na mtu mmoja kutoka mjini London, Uingereza amesema kuwa jambo hilo linawezekana,” alisema Mtikila.

Alifafanua kwamba, atafanya kila njia ili akutane na Dk Ulimboka na kumshawishi akafungue kesi katika mahakama hiyo ili liwe fundisho kwa wanaopenda kuwanyanyasa Watanzania wanaodai haki zao.

“Nitafanya kila njia ili nionane na Ulimboka, hili jambo ni lazima lifike katika mahakama ya kimataifa ya haki za binadamu…, pia anatakiwa kuwataja waliomfanyia unyama huu,” alisema Mtikila.

Kwa upande wake, Mtatiro alisema kuwa Ulimboka anatakiwa kukutana na vyombo vya habari na kueleza mambo yote ili kufichua yaliyokuwa yakifichwa na vyombo vya usalama.

“Ukweli utamweka huru na utawaweka huru watu wengi ambao wanaweza kufanyiwa unyama siku zijazo. Ikiwezekana afungue kesi ili haki itendeke,” alisema Mtatiro na kuongeza:

“Ulimboka anatakiwa kufahamu kwamba Watanzania hawakukubaliana na mateso aliyopewa, unyama aliofanyiwa unalaaniwa na kila mtu,” alisema Mtatiro.

Habari hii imeandikwa na Fidelis Butahe, Aidan Mhando, Joseph Zablon, Geofrey Nyang’oro, Boniface Meena na Leon Bahati.

No comments: