Wednesday, August 22, 2012

Makarani 800 Wagoma Kula Kiapo Cha Sensa


MAANDALIZI ya Sensa ya Watu na Makazi inayotarajiwa kufanyika Agosti 26, mwaka huu yameingia dosari baada ya matukio kadhaa ya kukwamisha kazi hiyo kujitokeza katika mikoa mbalimbali, ukiwamo Dar es Salaam ambako zaidi ya makarani 800 wamegoma kula kiapo cha utii na kutunza siri.

Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa mbali na makarani hao, vipeperushi vyenye ujumbe wa kutaka watu wagomee Sensa vimesambazwa mkoani Arusha, huku mkoani Tanga kukiwa na tukio la Sheikh mmoja kutiwa mbaroni kwa kusambaza vipeperushi vya aina hiyo.

Mgomo wa makarani
Makarani hao waligoma jana ikiwa ni siku yao ya mwisho ya mafunzo ya kazi ya kuhesabu watu na makazi. Makarani hao kutoka vituo mbalimbali kulikotolewa mafunzo hayo, walisema wameamua kugomea kiapo hicho kutokana na fedha zilizotengwa kwa ajili ya malipo ya kazi hiyo kuchakachuliwa kinyume na makubaliano.

Baadhi ya vituo ambavyo makarani wake wamegoma ni Shule ya Sekondari Makumbusho, Kambangwa, Shule ya Msingi Zawadi na vituo kadhaa vilivyopo maeneo ya Buguruni na Kawe.Baadhi ya makarani hao walionekana wakiwa katika makundi, muda ambao walipaswa kuendelea na mafunzo yao kabla ya kula kiapo cha kushiriki Sensa kwa uaminifu na ukamilifu.Baadhi ya makarani ambao waliomba majina yao yasitajwe gazetini, walisema imekiuka makubaliano ya awali.

“Serikali imesema imetenga Sh141 bilioni kwa ajili ya Sensa. Sisi tayari tuliingia makubaliano nayo kwamba tunatakiwa kulipwa Sh35,000 kwa siku, kwa muda wa siku saba jambo ambalo limegeuka na kuwa kinyume.”

“Ukipiga mahesabu fedha ambazo tungetakiwa kulipwa kwa siku hizo saba ni Sh245,000 lakini wao wamekuja hapa na kutupa Sh140, 000 tu. Hatuwezi kuendelea na kazi mpaka tulipwe fedha zetu.”
Karani mmoja katika Kituo cha Sekondari ya Kambangwa, alisema wameamua kugomea kiapo baada ya kuona kuwa mpaka mafunzo yanahitimishwa jana, baadhi yao hawajalipwa chochote.

RC Dar:Watalipwa
Akizungumzia madai ya makarani hao, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki alisema mpaka jana mchana makarani wote walipaswa kulipwa awamu ya pili ya fedha zao. Alisema awamu ya kwanza ya malipo hayo ilifanywa katika siku tano za mwanzo.“Kuna watu wamejichomeka katika zoezi hili, lakini kama kweli karani ameteuliwa lazima atalipwa pesa zake na kama imetokea amesahaulika basi afanye mawasiliano na mratibu wa Sensa wilaya anayotoka ili alipwe,” alisema.

Sheikh mbaroni
Katika hatua nyingine Sheikh Juma Koosa (52) anashikiliwa na polisi wilayani Morogoro akituhumiwa kutumia kipaza sauti kuwatangazia wananchi wasishiriki Sensa.

Sheikh huyo ambaye pia ni mwanafunzi wa mwaka wa pili wa Chuo Kikuu cha Kiislamu Morogoro, alikamatwa Agosti 19 mwaka huu alipokuwa kwenye Msikiti wa Miembeni, Mazinde mara baada ya kukaribishwa na wenyeji wake kuzungumza.Imedaiwa kuwa Koosa alitoa kitabu chenye kueleza sababu za kuwakataza Waislamu kutokushiriki Sensa mwaka huu.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe alisema Sheikh huyo pia alikutwa na nakala 15 za kitabu hicho.Alisema alikamatwa kutokana na taarifa za baadhi ya waumini ambao walichanganywa na taarifa za mgeni huyo... “Baadhi ya waumini walikubaliana naye huku wengine wakimpinga. Hivyo mtafaruku ukajitokeza na ndipo wale waliopinga wakawasiliana na polisi ambao walifika na kumkamata.”

Baada ya kukamatwa alipelekwa Kituo cha Polisi Mombo kwa mahojiano zaidi na kuhamishiwa Makao Makuu ya Polisi Wilaya ya Korogwe, baada ya kuwapo kwa dalili za baadhi ya waumini kuandamana kupinga hatua hiyo.Alisema, mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote.

CWT
Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Ezekiah Oluoch amewataka walimu kutosita kudai masilahi yao kwa kuhofia Serikali kuwaondoa katika shughuli mbalimbali za kitaifa.
Oluoch alisema jana kwamba wanao ushahidi wa maandishi kuwa kuondolewa kwa baadhi ya walimu katika Sensa kumetokana na kushiriki kwao katika mgomo ulioandaliwa na CWT kwa lengo la kudai masilahi yao sekta nzima ya elimu nchini.

Alisema CWT bado ipo katika mchakato wa kukusanya takwimu kwa wanachama wake waliotolewa katika Sensa nchi nzima na imebaini kuwa Serikali imefanya hivyo kama njia ya kuwakomoa.
“Tumepata ushahidi unaoonyesha kuwa walimu wamekatwa kwenye zoezi la Sensa kutokana na kushiriki mgomo” alisema na kuongeza kuwa hatua hiyo haitarudisha juhudi za walimu za kudai masilahi yao kwani madai yao ni muhimu.

Habari hii imeandikwa na Mashaka Kibaya, Korogwe, Aidan Mhando, Fidelis Butahe na Elizabeth Edward

             CHANZO:http://www.mwananchi.co.tz

No comments: