Na: MESHACK MAGANGA- IRINGA
Kila mmoja wetu anajua kwamba Kazi ni kipimo cha utu wake, dini zote zinasisitiza, serikali inasisitiza, watalaamu wa elimu ya mafanikio (Self Help) wanasisitiza hivyo na hata mila na desturi pia zinasisitiza, imelezwa na kufafanuliwa wazi kwenye dini zetu kwamba, “mtu asiyefanya kazi na asile” inatamkwa pia kwamba, mchana umewekwa ili watu watafute riziki, Mungu mwenyewe alifanya kazi kwa siku sita na kupumzika siku ya saba.
Mambo mengi huwa yanapingwa kwa njia mbalimbali, lakini suala la mtu kufanya kazi halijawahi kupata upinzani wa aina yoyote, haliwezi kupata upinzani kwa sababu kazi ndiyo maisha, bila kazi hakuna maisha, maendeleo na ustaarabu ambao binadamu anaweza kujivunia leo hii ni matokeo ya kazi.
Kama kazi ndiyo uhai, kazi ndiyo ustaarabu na maendeleo ya binadamu, mtu asiyefanya kazi anajiweka kundi gani kimaisha? Rais wa kwanza wa Kenya hayati Mzee Jomo Kenyatta aliwahi kusema kwamba, “mtu asiyesoma ni sawa na maiti” lakini bila shaka mtu asiyefanya kazi ni zaidi ya maiti.
Kwa mkabala huo tuna zaidi ya maiti wangapi hapa ndani ya nchi yetu hadi hivi sasa? Majibu ya swali hili ni aibu tupu, kwani idadi ya watu wasiotaka kufanya kazi ni kubwa karibu kama ile ya wanaofanya kazi, siyo kufanya kazi tu kwa maana ya matumizi ya nguvu za mwili na akili katika uzalishaji halali, lakini hata kufikiri ni jambo adimu sana kwetu hivi sasa.
Ni jambo la wazi kwamba baadhi ya wana-Iringa wana sifa moja kubwa sana kwa wageni wote ambao wamewahi kuishi hapa mkoani, wana sifa ya uvivu na maneno mengi ukiwemo ubishi hasa wa kisiasa na mchezo wa mpira wa miguu wa timu za nje ya nchi ya Tanzania, Aidha, wageni wote ambao wamewahi kuishi mkoa huu na hasa manispaa ya Iringa wanapoulizwa juu ya wana-Iringa na hasa kuhusu mitazamo yao katika maisha, watakwambia kuwa ni watu walioridhika na wanaopenda ubishi usio na maana na kushinda kwenye vilabu vya pombe.
Kuna sababu ni kwanini Watanzania wamekuwa hivyo, lakini sababu hizo haziwezi kufanya udhaifu huu kupigiwa upatu kama jambo la maana, jambo la maana ni Wana-Iringa kuanza kutambua kwamba, duniani kote ambako kuna maendeleo, hakukufanyika miujiza, bali kazi, tena kazi ngumu sana, hakuna hata mtu mmoja katika yale maeneo ya dunia ambayo yameinuka kiuchumi juzijuzi ambaye alikaa chini na kusema “saidia”, bali kila mmoja aliamua kufanya kazi. Mtaalamu wa Elimu ya Mafanikio Vincent Norman Peal katika kitabu chake kiitwacho The power of Positive Thinking anasema “Kama unafikiri vibaya,utapata matokeo mabaya.
Kama unafikiri vizuri utapata matokeo mazuri.Hii ni kwa sababu,binadamu hutenda na kuhisi kile anachokifikiri, kwani kisicho mawazoni mwake hakiwezi kumgusa kamwe”.
Nilipata kusoma makala Fulani iliyosema - Wananchi wa Singapore ambao miaka 30 tu iliyopita walikuwa watu wa kubezwa kutokana na umaskini, wamefikia mahali ambapo sasa kuwaita watu wa dunia inayodaiwa ni ya kwanza ni halali, lakini hayo hayakutokea kimiujiza, bali watu wote, raia na viongozi walifanya kazi, kila mmoja alijiuliza kila ilipofika jioni amefanya kitu gani kutwa nzima.
Hata kama mtu siyo mtaalam wa hesabu, akili ya kawaida inaweza kumwambia kwamba hawezi kamwe kubadilika na kufikia maendeleo bila kufanya kazi, ni kujidanganya na ni ujinga kwa mtu kukaa na kusema anasubiri serikali imsaidie au impe mtaji, ni ujinga zaidi mtu kuilaumu serikali kwamba imeshindwa, kabla hajajitazama mwenyewe na kujiuliza kile ambacho amejifanyia. Mjasiriamali maarufu duniani na Mwandishi wa kitabu kinachotamba Duniani kwa sasa cha ‘Rich Dad Poor dad’ Robert Kiyosaki, aliwahi kusema “Ukitegemea serikali ikutatulie matatizo yako basi unatatizo na ukifikiri uchaguzi utatatua tatizo lako basi una matatizo makubwa”.
Hakuna mtu mwingine,chama au kiongozi wa dini anayepaswa au anayeweza kutatua matatizo yetu wana Iringa iwapo tutaendelea kuishi maisha ya vijiweni bali ni sisi wenyewe.Kwa hiyo,jambo la awali tunalotakiwa kulifanya ni kukataa kuishi kimazowea .
Tubaini malengo yetu maishani,tuwe na mitazamo sahihi maishani na iliyothabiti pia, kwani mafanikio yanaweza kwenda kwa mtu yeyote,ili mradi tu uamini kwamba utafanikiwa.
Inashangaza kuona kwamba, mtu na hasa vijana tangu asubuhi amekaa kijiweni akicheza bao au karata, akipiga soga au kunywa pombe, halafu anailaumu serikali kwa kushindwa kumjali, inaingia akilini kweli mtu ashindwe kujijali mwenyewe lakini bado ategemee serikali imjali?.Haiwezekani hapa,iwe ni serikali ya CCM au ya CHADEMA utakuwa unapoteza muda kufikiri hivyo.siyo nia yangu kuisemea au kuitetea serikali kwamba haina udhaifu na mapungufu yake, la hasha, lakini je!
kabla hatujayatazama mapungufu hayo, wenyewe tumetazama mapungufu yetu?.
Kila mmoja wetu akiwa mkweli kwa nafsi yake na kujiuliza kila ikifika jioni amefanya kitu gani cha maana kwa kutwa nzima, ni lazima tutaanza kubadilika na kutambua kwamba sisi wenyewe ndiyo injini ya maendeleo yetu kama tutaamua kufanya kazi, inasemwa mara nyingi kwamba, kabla hatujauliza nani au kipi kimetufanyia kitu gani, tujiulize wenyewe tumejifanyia nini.Tukitaka kufanikiwa au kuanguka kwenye maisha yetu ni uamuzi wetu wenyewe.
Tukijaza fikra zetu imani kwamba tutafanikiwa,nilazima tutafanikiwa,kwasababu mafanikio hayachaguwi mtu kwa rangi au sura,umri wala jinsji,bali namna mtu anavyoamini katika mafanikio na kutumia muda wake vizuri huku akijia kwamba muda ndio Tunu pekee ambayo Mungu amemjalia mwanadamu aitumie kwa akili kubwa.
Kutafuta njia ya mkato ya maisha hakuwezi kutusaidia, kulalamika kutwa kucha bila kufanya kazi ni kujiumiza bure, umefikia wakati ambapo kila mmoja wetu anatakiwa kuanza kujitazama kama yeye kwanza na kuiambia nafsi yake kwamba hana haja ya kujidanganya, kutokufanya kazi ni kupingana na maisha, kama mtu anaamini kwamba anahitaji kula, kuvaa na kulala bila kuingia matatizoni, hana sababu ni kwanini asifanye kazi. Tukutane wiki ijayo…!
SISI WOTE NI WASHINDI, NA USHINDI UNATOKANA NA MATUMIZI SAHIHI YA MUDA
meshackmaganga@mail.com 0713 48 66 36.
No comments:
Post a Comment