KITUO cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimeipeleka Serikali ya Tanzania katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), kutokana na matukio 24 ya mauaji yanayokiuka haki za binadamu yaliyotokea nchini kati ya Januari na Septemba mwaka huu.
Mbali na hilo, LHRC kimepeleka taarifa hizo kwa Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Kimataifa, anayeshughulika na masuala ya mauaji ya raia yanayofanywa na vyombo vya dola.
Hatua hiyo ya LHRC inatokana na ripoti tatu zilizotolewa hivi karibuni kuchunguza kifo cha aliyekuwa Mwandishi wa Habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi kilichotokea katika Kijiji cha Nyololo, Mkoa wa Iringa, Septemba 2 mwaka huu.
Ripoti hizo ni ile ya Kamati ya Kuchunguza Mauaji hayo iliyoundwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi iliyokuwa chini ya Jaji Steven Ihema; Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora iliyokuwa chini ya Jaji Kiongozi Mstaafu, Amir Manento na ile ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) na Jukwaa la Wahariri Tanzania (Tef), iliyoongozwa na John Mirenyi.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Dk Helen Kijo-Bisimba alisema kuanzia Januari hadi Septemba mwaka huu, jumla ya watu 24 wameuawa na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama.
“Tumepeleka mashtaka 24 ICC tangu Septemba 28 mwaka huu, ambayo yanahitajika kufanyiwa uchunguzi na kuchukua hatua kali dhidi ya Serikali ya Tanzania ambayo imekuwa ikiwalinda viongozi wake wanaokiuka haki za binadamu,” alisema Dk Bisimba.
Alisema taarifa hizo pia wamezipeleka kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu katika kikao kinachoendelea huko Ivory Coast, lengo likiwa ni kuchunguza na kuchukua hatua katika Mahakama ya Afrika.
“Tunatarajia kuona uwajibikaji wa viongozi wote wa Serikali na vyombo vya dola waliohusika kwa njia yoyote ile. Hatua hizo au uwajibikaji huo ni pamoja na kujiuzulu, kuachishwa kazi na kufikishwa Mahakamani, ” alisema.
Aliitaka Serikali kuacha propaganda zinazotaka kuchochea vurugu katika taifa huku akisema inapaswa itambue kuwa hivi sasa nchi iko katika zama za vyama vingi vya siasa na kuacha kutumia vyombo vya dola kuleta chuki na mafarakano.
Dk Bisimba alisema baada ya kupitia taarifa zote tatu, LHRC kimesikitishwa na taarifa ya Kamati ya Dk Nchimbi...
“LHRC hakijashangazwa sana pale taarifa hiyo ilipoonyesha wazi nia ya kuwalinda watuhumiwa kwa kuwa Serikali yetu bado haijajenga mfumo wa kujichunguza na kujiwajibisha yenyewe.”
“Serikali imeudhihirishia umma kuwa haikuwa na nia ya dhati ya kuchunguza suala la mauaji yaliyofanywa na Jeshi la Polisi, bali ilikuwa na lengo la kulisafisha Jeshi la Polisi na kuwalinda maofisa wake.”
Dk Bisimba alisema tangu mwaka 2001 hadi sasa, kituo hicho kimekuwa kikifuatilia kwa karibu matukio mbalimbali ya mauaji yanayoendelea kufanywa na vyombo vya dola na hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi ya wahusika. Werema ashangaa, mawakili watofautiana Akizungumzia suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema alisema hana taarifa za Serikali kushtakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya The Hague.
“Kwa nini wameamua kutushtaki katika Mahakama ya The Hague? Kwani hapa nchini hakuna mahakama au wameona ni bora wavuke mipaka... Kwa sasa siwezi kulizungumzia zaidi suala hilo.”
Wakili wa Kujitegemea, Gaudioz Ishengoma alipotakiwa kuzungumzia hilo alisema anaunga mkono uamuzi wa kituo hicho kuipeleka Serikali kwenye Mahakama ya Kimataifa.
Alisema hilo ndilo eneo sahihi ambalo Serikali inatakiwa kupelekwa kwa sababu ya ukiukaji wa haki za binadamu na kwamba huko ndiko ambako haki inaweza kupatikana.
Hata hivyo, Wakili mwingine wa Kujitegemea, Majura Magafu alipinga hatua hiyo akisema kituo hicho kimekosea kuipeleka Serikali The Hague kwa kuwa imekuwa ikichukua hatua za kisheria dhidi ya makosa mbalimbali ya mauaji ambayo yamekuwa yakitokea.
“Kwa mawazo yangu, hawa LHRC wamekosea nadhani wamefanya hivyo kwa masilahi yao binafsi hasa ili kuonyesha kwamba wanafanya kazi,” alisema. Alisema hata kama Serikali itakuwa imeshindwa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wauaji, kituo hicho kilitakiwa kuishtaki Serikali katika mahakama za hapa nchini.
“Hawa sijui wanataka kutupeleka wapi kwa sababu wananchi wengi wa Afrika wakiwemo wa Kenya wamekuwa wakitaka mashtaka yasipelekwe nje ya nchi, hivi kila kitu tunawategemea Wazungu kwa sababu gani hasa?”
Utaratibu wa mashtaka Kwa mujibu wa Mahakama hiyo, nchi mwanachama au Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ndiyo wanaoweza kuelezea hali ya uhalifu ndani ya mipaka ya Mahakama hiyo na maelezo hayo hupelekwa kwa Mwendesha Mashtaka Mkuu wa ICC.
Mwendesha mashtaka mkuu atayapitia na kuanza uchunguzi isipokuwa pale tu atakapoona kuwa hakuna haja ya uchunguzi kwa maana ya kuwa kuna ushahidi wa kutosha juu ya uhalifu husika.
Uchunguzi wa mwendesha mashtaka utahusisha taarifa zote na ushahidi unaotakiwa kutathmini uhalifu unaotajwa huku ukizingatia haki zote za anayetuhumiwa. Katika kipindi chote cha uchunguzi, mwendesha mashtaka atakuwa akitoa taarifa anazopata kwa Baraza la Awali la Mahakama (Pre-Trial Chamber) ambalo litakuwa na wajibu kwa maelekezo ya mwendesha mashtaka mkuu kutoa hati ya kukamatwa kwa wahusika au hati ya kuitwa mahakamani hapo.
Mtuhumiwa anapofika mahakamani hapo, husomewa mashtaka yake ambayo yatakuwa msingi wa kesi nzima. Baada ya kuthibitishwa kwa mashtaka, kesi hiyo itasikilizwa na Baraza la Awali la Mahakama chini ya majaji watatu na kutoa uamuzi wake wa ama kuwaachia au kuwatia hatiani watuhumiwa.
Tayari ICC imeshawapandisha kizimbani wanasiasa maarufu wa Kenya kutokana na kutuhumiwa kuhusika kuchochea vurugu za uchaguzi nchini Kenya mwaka 2008 ambazo zilisababisha vifo vya watu 1,133.
Wanasiasa hao ni Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta, Mbunge wa Eldoret Kaskazini, William Ruto, aliyekuwa Mkuu wa utumishi, Francis Muthaura na Mtangazaji wa Redio ya Kass FM, Joshua Sang.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment