Na: Rodrick Maro
Ndugu zangu;
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kinasikitishwa sana na mauaji yanayoendelea kufanywa na vyombo vya dola hususan vyombo vya ulinzi na usalama bila hatua za kisheria kuchukuliwa kwa watuhumiwa wa ukiukwaji huo wa haki ya kuishi.
Tangu mwaka 2001 hadi sasa, LHRC tumekuwa tukifuatilia matukio mbalimbali ya kuuawa kwa raia yanayofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama.
Hivi karibuni, mnamo tarehe 2 Septemba, 2012 tulishuhudia mauaji ya kinyama kule Iringa yaliyofanywa na polisi kwa kutumia kile tunachosadiki kuwa ni ‘bomu la machozi’ kwa kumuua mwandishi wa habari ndugu Daudi Mwangosi.
Leo hii, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimetoa taarifa baada ya uchunguzi na kufuatilia mwenendo wa matukio mbalimbali ya ukiukwaji wa haki za binadamu, hususan ukiukwaji wa haki ya kuishi (waathirika wakiwa mikononi mwa vyombo vya dola).
Taarifa rasmi imeambatanishwa. Kwa mfano kwa mwaka huu tu hadi mwishoni mwa mwezi wa tisa takwimu za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu zinaonyesha kuwa tayari watu 24 walikwisha uawa na watendaji wa vyombo vya ulinzi na usalama. Baadhi ya sababu ni kushindwa kuhimili siasa za vyama vingi na ukosekanaji wa uvumilivu wa kisiasa.
Pia, kushindwa kuwa na mipango shirikishi ya kiusalama katika maeneo ya uwekezaji hususan kwenye migodi na kwenye hifadhi za taifa. Baada ya kutafakari na kuangalia uwajibikaji wa viongozi wa nchi hii, Kituo kimechukua hatua zifuatazo, baina ya nyingine: ·
Kupeleka malalamiko kwa Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kwenye masuala ya mauaji ya raia yanayofanywa na vyombo vya dola (UN-Special Rapporteur on etra-judicial killings). Kumtaka mjumbe huyu kufanya uchunguzi na kuchukua hatua stahiki kwa serikali ya Tanzania. Taarifa ilipelekwa tarehe 28 Septemba 2012.
Na tayari ameshaanza kupitia malalamiko ya Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu; ·
Kupeleka malalamiko kwa Mwendesha Mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa (ICC Prosecutor) na kumtaka kufanya uchunguzi na kuona hatua anazoweza kuchukua, Tarehe 28 September 2012; · Kupeleka suala hili kwenye Tume ya Afrika ya Haki za Binadamu na Haki za Watu katika kikao chake cha mwezi wa Oktoba 2012, kule Ivory Coast na kuitaka Tume kuchunguza na kuchukua hatua ikiwemo kulipeleka suala hili Mahakama ya Afrika; ·
Taarifa hii pia imepelekwa kwa wadau wengine mbalimbali wa haki za binadamu kama Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu (FIDH) na Ofisi za umoja wa mataifa Tanzania kwa hatua mbalimbali.
Nchi hii inaheshimu utawala wa sheria na katiba. Katika haki zilizoainishwa kwenye katiba ibara ya 18 ni haki ya kutoa maoni na uhuru wa mtu kushirikiana na wengine ibara ya 20. Matumizi ya mikutano ya hadhara na maandamano yenye kufuata taratibu za kisheria ni njia mojawapo ya demokrasia.
Hivyo ipo haja kwa serikali kutoa taarifa na habari kwa umma kuhusu juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuwalinda wao na mali zao, kuwaletea maendeleo na kupunguza ugumu wa maisha.
No comments:
Post a Comment