Na. Zawadi
Msalla- MAELEZO 20/11/2012,
Arusha.
Rais Jakaya Kikwete
ameiasa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi Kusini mwa Afrika (SADC) kuimarisha
ushirikiano kati yake na nchi wanachama wa Jumuiya hiyo ili kufanikisha
utekelezaji wa Mkakati wa pili wa kushughulikia masuala ya Siasa, Ulinzi na
Usalama wa Jumuiya hiyo.
Rais Kikwete
ameeleza hayo wakati akizindua Mkakati wa kushughulikia masuala ya
Siasa, Ulinzi na Usalama wa Jumuiya hiyo (SIPO II) jijini Arusha wakati wa
mkutano uliowahusisha wawakilishi mbalimbali kutoka katika Jumuiya wanachama wa
SADC.
Amesema
ili malengo ya Mkakati huo yaweze kufanikiwa ni lazima ushirikiano
wa ndani na nje wa nchi hizo wanachama uimarishwe na kuongeza kuwa
SADC haiwezi Kutegemea mikakati ya ndani ya ulinzi na Usalama ya nchi fulani
kutaka kutekeleza mkakati wake.
"SADC haitakiwi
kuiingilia kwa kutaka kuibadili mikakati ya ndani ya Nchi wanachama ya ulinzi
na usalama badala yake washirikiane kwa karibu kuangalia nini cha kufanya"
Amesema Rais.
Kuhusu umuhimu wa
mkakati huo Rais Kikwete amesema utakuwa muongozo wa
SADC katika masuala yote ya ulinzi, usalama na siasa, na umejikita katika
kutatua vikwazo mbalimbali vya kiulinzi vilivyopo.
Amefafanua kuwa
Utekelezaji wa SIPO na maazimio yake utapelekea hali ya amani na utawala bora
kwa Nchi nyingi za Afrika na kuongeza kuwa katika awamu ya pili ya SIPO
mabadiliko mengi yamefanyika yakiwemo uongezaji wa vipaumbele katika mfumo wa
utekelezaji na ufuatiliaji wa masuala ya ulinzi na usalama.
Uzinduzi wa SIPO II
utaangalia ushirikiano kati ya Nchi wanachama, ushirikiano katika masuala ya
kibiashara, uhakika wa kushughulikia masuala ya upatikanaji wa Amani na
ushirikiano katika nyanja ya habari.
Akieleza historia ya
chombo cha Usalama cha SADC alisema kabla ya kuanzishwa kwa chombo hicho
kulikuwa na ushirikiano wa nchi katika masuala ya ulinzi na usalama na
kubainisha kuwa kuanzishwa kwa SIPO kunatokana na nchi wanachama
kuona umuhimu wa kuwa na chombo kinacho waongoza katika masuala hayo
yote.
Awali akizungumza na
wajumbe wa mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Benard
Membe amesema kuwa SIPO imekuwa ni nyenzo muhimu nay a kutegemewa na nchi za
SADC katika masuala yote ya usalama.
Amesema SIPO
ilizinduliwa rasmi mwaka 2004 na baadae kufanyiwa marekebisho ya kimsingi mwaka
2007 na kueleza kuwa kutokana na marekebisho hayo ya Mwaka 2007 ilikubaliwa kuwa
mikakati na vapaumbele vya SIPO iwe inapitiwa kila baada ya miaka
mitano.
Aidha uzinduzi huo
utafuatiwa na mafunzo mbalimbali yatakayoendeshwa na wataalamu kwa muda wa siku
nne.
No comments:
Post a Comment