Saturday, November 24, 2012

Madaktari Zanzibar Wakutana Kujadili Katiba yao

 Dk. Juma Salum Mambi ambae ni Katibu wa Jumuiya ya Madaktari, akifafanua jambo kwa wajumbe kuhusu katiba yao
 Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari Zanzíbar Dk. Said Mohammed Abdallah akisikiliza kwa makini hoja zilizotolewa na wajumbe wakati wa mkutano wao uliofanyika leo katika ukumbi wa Wizara ya Afya
  Madaktari mbalimbali wakimsikiliza kwa makini Dk. Juma Salum Mambi (hayupo pichani) wakati alipokuwa akijibu maswali yaliyo ulizwa na wajumbe hao.
 Marijani Msafiri akiuliza suali kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Mdaktari Zanzibar Dk. Said Mohammed Abdallah juu ya suala la kuwa na Mwanasheria wa jumuiya yao katika mkutano wa wanachama uliofanyika Wizara ya Afya leo.
                PICHA NA MAKAME MSHENGA

Na:  Fatma Mzee, Maelezo

JUMUIYA ya Madaktari Zanzibar, imefanya mkutano wa kujadili katiba yake kwa lengo la kuifanyia marekebisho ili iende na wakati wa sasa. 

Miongoni mwa marekebisho hayo, ni pamoja na kuongeza kipengele cha jumuiya hiyo kuwa na mwanasheria wake.
Mwenyekiti wa jumuiya hiyo ambaye ndiye aliyeongoza mkutano huo Dk. Said Mohamed Abdullah, aliwashauri wanachama kuisoma vyema katiba hiyo na kuainisha maeneo wanayohisi yanahitaji kurekebishwa ili kuiimarisha zaidi .

Alisisitiza umuhimu kwa wanachama kutopuuza kuhudhuria na kufuatilia vikao kwa lengo la kuwa na jumuiya iliyo imara na inaweza kusimamia vizuri matarajio yao.
Hata hivyo, wajumbe wote wa jumuiya hiyo walikubaliana na katiba hiyo, ingawa baadhi yao waliomba wapatiwe muda zaidi wa kuipitia kwa kina kabla kutoa mapendekezo yao.

Mjumbe mmoja Yussuf Haji, aliwaomba wanachama wenzake kuiheshimu katiba hiyo, kwani ndio muongozo utakaowezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. 

Kwa upande wake, Katibu wa jumuiya hiyo Dk. Juma Salum Mambi alisema, ili jumuiya hiyo ifanikiwe na na kufanana na jumuiya nyengine zilizopiga hatua kubwa, ni vyema madaktari wazingatie haja ya kuzidi kuonesha umoja na mshikamano utakaosaidia kuiimarisha jumuiya yao.

Mkutano huo umeakhirishwa hadi Disemba 8, mwaka huu ili kutoa fursa kwa wanachama kuipitia kikamilifu katiba hiyo.

No comments: