Sunday, November 11, 2012

Upinzani Syria wakubaliana kuungana

Makundi ya upinzani nchini Syria yanayokutana mjini Doha,yamekubaliana kimsingi kuhusu mpango wa umoja dhidi ya rais Bashar al-Assad.Washiriki wa mkutano huo wamesema Jumapili(11.11.2012).

"Tumekubaliana kuhusu vipengee viwili juu ya kuundwa kwa muungano wa kitaifa nchini Syria kwa ajili ya majeshi ya upinzani na mapinduzi. tutaendelea na majadiliano yetu kuhusu mambo yanayohusika katika muungano huo leo Jumapili," mmoja wa viongozi wa muungano huo wa upinzani Suhair Atassi ameliambia shirika la habari la AFP baada ya saa 12 za mazungumzo.

"Tulikuwa katika hatua ya kutia saini makubaliano lakini tumeonelea kutoa muda zaidi ili kutathmini sheria za ndani kwa ombi la baadhi ya makundi," amesema mjumbe mwingine Riad Seif, ambaye anaripotiwa kuwa anaonekana na serikali ya Marekani kuwa ana uwezekano wa kuwa mkuu mpya wa upinzani.

NSC lakabiliwa na mbinyo 
Washiriki walitarajiwa kurejea katika mazungumzo leo asubuhi. Mkutano huu unakuja baada ya baraza la taifa la Syria SNC kukabiliwa na mbinyo kutoka kwa mataifa ya Kiarabu na mataifa ya magharibi kukubali mpango wa umoja wa upinzani, huku kukiwa na hali ya kukata tamaa miongoni mwa makundi ya wapiganaji.

Hapo nyuma likiwa linatambulika kama wawakilishi wakuu wa upinzani lakini kadiri ya muda ulivyokwenda lilipoteza hadhi hiyo katika serikali ya Marekani , kutokana na kudhibitiwa na watu ambao wanaishi uhamishoni na hawana uhusiano wa karibu na hali halisi ndani ya nchi, baraza hilo la SNC , lilitakiwa mara mbili kuahirisha mazungumzo juu ya mpango wa kuunda serikali itakayojumuisha makundi mengi ambayo itakuwa inasubiri kuchukua madaraka ndani ya Syria.

Makubaliano hayo yako katika msingi wa harakati zinazochukuliwa na Seif ambazo zina lenga kuundwa kwa serikali ya mpito , ambalo ni baraza la kijeshi litakaloshughulikia makundi ya waasi ndani ya Syria na mahakama ambayo itafanyakazi katika maeneo yanayoshikiliwa na waasi. 
  
Serikali ya mpito
Serikali ya mpito ambayo itakuwa na wajumbe kumi itachaguliwa na kundi jipya lenye wajumbe 60 ambalo litatokana na wanaharakati wa kiraia na wapiganaji waasi ndani ya Syria, pamoja na wale wanaoishi uhamishoni ambao wamedhibiti baraza la SNC.

Jana Jumamosi (10.11.2012) baraza la NSC limewasilisha pendekezo lake na kiongozi wake mpya George Sabra amewaambia waandishi habari mjini Doha kuwa baraza hilo la NSC ni la muda mrefu zaidi kuliko harakati nyingine zozote, akiongeza kuwa makundi ya upinzani hayapaswi kulazimishwa kuwa chini ya chombo chochote kingine.

Kwa mujibu wa shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria , zaidi ya watu 37,000 wameuwawa tangu vuguvugu la harakati za kuuondoa utawala wa rais Bashar al-Assad kuzuka Machi 2011, harakati hizo zilipoanza kwanza kama vuguvugu la amaandamano na kisha kugeuka uasi wa mapambano ya silaha.
Dw

No comments: