Sunday, November 4, 2012

Waasi wa Mali tayari kujitenga na al-Qaida

Wapatanishi wakuu katika mgogoro wa Mali wanajaribu kukishawishi kikundi kimoja cha kiislamu kaskazini mwa nchi hiyo kujitenga na tawi la al-Qaida. Kuna taarifa kwamba kikundi hicho kiko tayari kuitikia wito huo. 

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Burkina Faso, Djibrill Bassole ambaye anasaidia juhudi za usuluhishi zinazofanywa na nchi yake kujaribu kuumaliza mgogoro wa Mali uliodumu kwa miezi saba, amesema atakutana kwa mazungumzo na viongozi wa kikundi hicho, Ansar Dine mwishoni mwa juma hili.

Ansar Dine imetuma ujumbe nchini Burkina Faso na Algeria kuzungumzia kupatikana kwa amani. Rais wa Burkina Faso Blaise Compaore ambaye ni mpatanishi mkuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, katika mgogoro wa Mali, atakutana pia na ujumbe wa Ansar Dine, hii ikiwa ni kwa mujibu wa waziri wake wa mambo ya nchi za nje, Djibrill Bassole.

Compaore anatarajiwa kuwaeleza kinaganaga wajumbe wa Ansar Dine matakwa ya ECOWAS, ambayo ni kulitaka kundi hilo lijitenge na mienendo ya kigaidi na kihalifu, na kurejea kwenye mchakato wa kisiasa.

Ansar Dine tayari kuitupa mkono al-Qaida 

Kiongozi wa Ansar Dine Algabass Ag Intalla ameliambia shirika la habari la AFP kwamba kikundi chake kinajitegemea na kiko tayari kufanya mazungumzo ya amani. Vile vile ameelezea utayari wake wa kukutana ana kwa ana na waziri wa serikali ya mpito ya Mali ambaye kwa sasa yuko mjini Ouagadougou, ikiwa mpatanishi atataka iwe hivyo. Afisa wa serikali ya Mali amesema mkutano baina yao na kiongozi huyo wa Ansar Dine unawezekana.

Blaise Compaore anashinikiza kupatikana kwa suluhisho la amani katika mgogoro wa Mali, ingawa maandalizi ya hatua za kijeshi pia yako mbioni. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwezi uliopita lilipitisha azimio linaloutaka Umoja wa Afrika kufanya matayarisho ya uingiliaji kati kijeshi, ambao utashirikisha wanajeshi zaidi ya 3,000 kulikomboa eneo la kaskazini mwa Mali. 

Ansar Dine ni mojawapo ya makundi yanayoishikilia sehemu kubwa ya kaskazini mwa Mali, baada ya kuupiku uasi wa kundi la wapiganaji wa kituareg, kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyoiangusha serikali ya Mali mapema mwanzoni mwa mwaka huu. Kundi hilo linaloongozwa na Iyad Ag Ghaly, limetuma ujumbe mwingine nchini Algeria, ambayo pia inapakana na Mali. 

Umuhimu wa Algeria 

Kiongozi huyo amekaririwa na gazeti la Algeria, El-Watan, akisema yuko tayari kuvunja uhusiano wake na tawi la Al-Qaida kaskazini mwa Afrika, AQIM, na kujiunga na juhudi za kimataifa kutafuta amani nchini Mali. Algeria inachukuliwa kama mshirika muhimu katika mapambano dhidi ya makundi yenye misimamo mikali ya kiislamu na mwanzoni mwa Juma hili nchi hiyo ilitembelewa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton, ambaye alikuja kuunga mkono mchakato wa kutafuta suluhu kwa mgogoro wa Mali. Vyanzo vingine vya habari ndani ya kikundi cha Ansar Dine kimeelezea uwezekano wa ujumbe mwingine wa kikundi hicho kuizuru Nigeria.

No comments: