Waumini wa Madhehebu la Shia wakiwasili na kukusanyika katika eneo la makaburi ya Washia Kisutu jijini Dar es Salaam wakijiandaa kuanza maandamano ya kuadhimisha siku ya Ashura kukumbuka kifo cha Mjukuu wa Mtume Muhammad (S.A.W) Imam Hussein yaliyofanyika jana
Mwenyekiti wa Msikiti wa Jamaat Shia Ithna Asheri Bw. Azim Dewji akifafanua kwa waandishi wa habari amesema katika kuadhimisha siku hii Waislam wa dhehebu la Shia watafanya matembezi kutoka makaburi ya Shia Kisutu hadi katika msikiti mkuu wa Shia Ithna Asheri na wakati wa matembezi hayo ndani yake kutakuwa kunafanyika kumbukumbu kwa njia ya kuimba nyimbo za maombolezo tukikumbuka shujaa wetu namna alivyouawa na vile vile sisi kujipa uhai kiroho katika kuonyesha namna kiongozi anaweza kujitolea kwa watu wake na kwamba ni funzo kwa kila mwanadamu ajitolee kwa ajili ya wenzake
Kwa Upande wake Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Alhad Mussa Salum amesema siku hii ni muhimu sana kwa Waislam kote duniani kwa sababu tunamkumbuka Imam Hussein ambaye kifo chake kilikuwa ni kifo cha kinyama, kifo cha wapenda dhulma katika uso wa ardhi. Amesema kifo cha Imam Hussein kinamgusa kila Muislam kwa sababu ilikuwa ni siku ambayo haki ilizimwa na dhuluma, maadui wa haki walijaribu kuitaka batil isimame , kwa hiyo siku ya leo ni sku ya kutetea haki na uadilifu. Aidha Sheikh Salum amesema kwa Waislam wote Tanzania na hata wasio Waislam wanatakiwa wajifunze kutoka kwa Imam Hussein kwamba yeye alikuwa ni mtetezi wa haki, alikuwa anatetea Uadilifu kwa hiyo tujifunze kwamba kutetea haki na kutetea uadilifu ndio jambo linalotakiwa katika maisha ya leo, kutetea wanyonge, kupiga vita Dhuluma na ukandamizaji wa namna yoyote ile ndio lililokuwa jambo alilolipenda Imam Hussein.
No comments:
Post a Comment