Friday, November 16, 2012

Waziri Mkuu wa Misri aitembelea Gaza


Waziri Mkuu wa Misri Hisham Kandil leo ameutembelea Ukanda wa Gaza na kuahidi kuwasaidia Wapalestina kurejesha utulivu kwa kusitisha mashambulizi ya Israel ambayo yameendelea licha ya ziara hiyo. Waziri Mkuu wa Misri Hisham Kandil leo ameutembelea Ukanda wa Gaza na kuahidi kuwasaidia Wapalestina kurejesha utulivu kwa kusitisha mashambulizi ya Israel ambayo yameendelea licha ya ziara hiyo.

Wakati huo huo Wapalestina nao wamerudia wito wao kwa Umoja wa Mataifa wakiutaka kuingilia kati mashambulizi yanayofanywa na Israel katika ukanda wa huo. aWaziri Mkuu huyo wa Misri amewaahidi Wapalestina kuwa nchi yake itafanya juhudi kuhakikisha inawarejeshea utulivu kwa kukomesha mashambulizi ya Israel ambayo ameyaita kuwa ni ya kikatili. 

Kandil amesema kuwa Misri haitasita kuongeza juhudi zake na kujitolea ili kusitisha ukatili huo. Kiongozi huyo ameyasema wakati akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuitembelea hospitali ya Shifa iliyoko Gaza City na kuwaona baadhi ya majeruhi wa mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na Israel. 

Israel yakiuka ahadi ya kusitisha mashambulizi 
Hapo kabla Israel ilitoa taarifa kuwa itasitisha mashambulizi wakati wa ziara ya kiongozi huyo kama nchi yake ilivyoomba lakini hilo halikuwezekana kwa mashambulizi yameendelea kufanyika. Ndege za kivita za Israel zimelishambulia eneo la kaskazini mwa Gaza asubuhi ya leo na kuwauwa watu wawili. Shirika la habari la AFP linaarifu kuwa ndege hizo zilipiga mabomu kwenye kundi la raia katika eneo la Nazila kaskazini mwa Gaza City.

Tukio hilo limefanyika muda mfupi baada ya Israel kulituhumu kundi la Hamas kuwa limekiuka makubaliano ya kutofanya mashambulizi wakati wa ziara ya Kandil. Ziara hiyo ilielezwa kuwa itachukua muda wa masaa matatu na inatazamwa kama hatua ya Misri kuonyesha mshikamano na kuliunga mkono kundi la Hamas katika kipindi hiki kigumu. Misri iliiomba Israel kusitisha mashambulizi wakati wa ziara hiyo na Israel imekubali. Afisa katika serikali ya Israel anasema kuwa Netanyahu amekubali kusitisha harakati zote za kijeshi kwenye ukanda wa Gaza kama Misri ilivyoomba.

Hata hivyo majibu hayo pia yanasema kusitishwa huko kwa mashambulizi kutafanya kazi tu endapo Hamas nao watafanya hivyo hivyo. Misri inapinga mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza ikisema hayakubaliki, wakati Marekani ikisema kuwa inatambua haki ya Israel ya kujilinda na mashambulizi ya Hamas. Hapo kabla Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alizungumzia mashambulizi ya nchi yake dhidi ya Gaza na kusema Taarifa zilizotolewa hivi karibuni na jeshi la nchi hiyo zinasema kuwa tayari limeanza kuandikisha vikosi vya askari 16,000 kati ya 30,000 vilivyoamriwa kuwa tayari. 

Nayo Mamlaka ya utawala Wapalestina imepeleka kilio kuhusu mashambulizi hayo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likilitaka kuingilia kati na kusitisha mashambulizi ya kijeshi ya Israel katika ukanda wa Gaza ikiwa ni siku moja baada ya Baraza hilo kushindwa kuchukua hatua hapo jana. 

Mwangalizi wa Palestina katika Umoja wa Mataifa Riyad Mansour ameliandikia barua baraza la usalama akisema kuwa kitendo cha Israel kupeleka vikosi vya kijeshi vya ardhini ikiwemo vifaru magari ya silaha karibu na mpaka wa Gaza kinasababisha wasiwasi wa hali ya juu na hivyo wanahitaji zingatio la jumuiya ya kimataifa. Jana Wapalestina 19 kati yao wakiwemo raia 12 na Waisrael 3 wameuawa jana kutokana na majibizano ya mizinga ya angani. Kati ya raia 12 waliouawa huko Gaza sita ni watoto. 

dw

No comments: