MGOGORO wa makada wawili wa CCM; Benard Membe na Hussein Bashe umechukua
sura mpya, baada ya mbunge huyo wa Mtama, kukiomba chama hicho tawala
kuingilia kati ili kuupatia suluhu.
Mvutano wa Bashe na Membe ulianza wakati wa kampeni za uchaguzi wa ndani
wa CCM hasa uchaguzi wa NEC baada ya Bashe kumtuhumu Membe kwa mambo
mbalimbali ikiwamo kukigawa chama.
Kauli hiyo ya Bashe ilimkera Membe ambaye kwa nyakati tofauti amekuwa
akisisitiza kuwa atamshughulikia mwanasiasa huyo chipukizi wa CCM ili
amtambue.
“Nitashughulika na Bashe ndani ya chama kwa maana ya kumfikisha kwenye
kamati zetu, ili ayaeleze vizuri ambayo amenipakazia na kunichafua sana…
Lakini mambo mengine ambayo yamekaa kijinai sasa hayo ndiyo
nitakayoyapeleka mahakamani,” alisema Membe baada ya taarifa hizo.
Habari zilizopatikana jana zimeeleza kuwa Membe amemwandikia barua
Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Phillip Mangula kumwomba amtake Bashe
athibitishe kauli zake mbalimbali dhidi yake.
Moja ya mambo Membe anamtaka Bashe ayathibitishe ni kwamba waziri huyo
wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, kuwahi kusema kuwa akiwa
Rais, atawafukuza watu kumi na moja nchini ambao anaamini kuwa siyo
Watanzania.
“Barua hii ina tuhuma nyingi, lakini kikubwa mheshimiwa huyo (Membe)
amekiomba chama kimtake Bashe athibitishe tuhuma zake dhidi yake,
ikiwamo hili la kuwafukuza Watanzania 11,” kilidokeza chanzo chetu cha
habari ndani ya CCM.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa baada ya makamu mwenyekiti huyo kupata barua
ya Membe, ameipeleka katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman
Kinana kwa hatua zaidi.
Habari zimeeleza kuwa tayari Kinana ameifanyia kazi barua hiyo kwa
kumwandikia barua Bashe ili ajibu tuhuma zinazomkabili ifikapo kesho
Januari 10.
Nakala ya barua hiyo ya Kinana imetumwa kwa Katibu wa CCM Wilaya ya
Nzega ambako Bashe anatokea akiwa Mjumbe wa Mkutano Mkuu Taifa kupitia
wilaya hiyo.
“Tayari Bashe ameandikiwa barua na CCM kumtaka ajibu malalamiko hayo ya
mwenzake Membe,” kilieleza chanzo hicho cha habari.
Membe hakupatikana kwa siku tatu mfululizo, ili azungumzie suala hilo
baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana na taarifa zilizopatikana
ofisini kwake, zimeeleza kuwa yuko likizo jimboni kwake Mtama, Lindi.
Bashe hakuthibitisha wala kukanusha kupata barua hiyo ya CCM inayomtaka
ajibu madai ya Membe, badala yake akasema: “Membe aliahidi
kunishughulikia na mimi ninangoja anishughulikie.”
Mangula alipotafutwa juzi kuzungumzia suala hilo alisema asingeweza
kusema chochote kwa kuwa alikuwa hajafika ofisini tangu alipokwenda
kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka.
“Sijajua chochote kilichoendelea ofisini kwa sababu nilikuwa kijijini
kwangu kwa ajili ya Sikukuu ya Krimasi na Mwaka Mpya. Nikiingia ofisini
naweza kuwa katika nafasi ya kujua kilichoendelea,” alisema Mangula.
Hata hivyo, alipopigiwa simu jana, iliita bila kupokewa na baadaye
ikazimwa kabisa.
Kinana naye hakupatikana jana baada ya simu yake pia kuita na kupokelewa
na mtu mwingine mara kadhaa ambaye alieleza kuwa alikuwa mkutanoni siku
nzima.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alijibu kwa kifupi na
kukata simu,” Sijapata wala kuona barua ya malalamiko ya Membe kwa
Bashe.”
Mgororo ulikoanzia
Novemba 10, mwaka jana Bashe akizungumza na waandishi wa habari mjini
Dodoma, alimtuhumu Membe akidai kuwa ndiye anayehusika na vipeperushi
vya kumhujumu mwenyekiti wa chama hicho, Rais Jakaya Kikwete vilivyokuwa
vimetawanywa na watu wasiojulikana siku chache kabla ya uchaguzi wa
mwenyekiti na nafasi nyingine kufanyika.
www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment