Uchunguzi mpana wa upangaji wa mechi za kandanda umegunduwa kuwepo kwa shaka juu ya matokeo ya zaidi ya michuano 680, ikiwemo ile ya kutafuta tiketi ya kushiriki fainali za kombe la dunia na ubingwa wa Ulaya.
Michezo mengine iligundulika kuwa na shaka ni pia na michezo miwili ya ligi ya mabingwa wa Ulaya - Champions League. Uchunguzi huo umepata ushahidi kwamba genge moja la kihalifu lenye makao yake nchini Singapore linahusika kwa karibu na upangaji wa michuano hiyo ya kandanda. Uchunguzi huo wa Shirika la polisi la Ulaya EUROPOL, umegundua pia kuwepo kwa shaka shaka katika michuano barani Ulaya na mengine 300 nje ya bara hilo, hasa Afrika, Asia na Amerika kusini na kati.
Shirika hilo limekataa kutaja majina ya watuhumiwa, michuano husika, wachezaji na maafisa au waliopanga matokeo, likisema hilo litahujumu uchunguzi unaoendelea katika ngazi za kitaifa. Kwa hivyo haikuweza kufahamika ikiwa taarifa hizi ni mpya au zilikwishatajwa katika kesi zilizofanyika sehemu mbali mbali barani Ulaya kuhusu upangaji matokeo.
Mkurugenzi wa EUROPOL Rob Wainwright aliwaambia waandsishi habari kwamba," Hii ni siku ya huzuni kwa kandanda la Ulaya." Alisema wahalifu wamekuwa wakijikingia fedha kwa rushwa katika soka, katika kiwango ambacho kina tishia mchezo huo.
Shirika la EUROPOL linasema maafisa wa michuano 425, maafisa wa kilabu, wachezaji na wahalifu kutoka nchi zipatazo 15 walihusika katika kupanga matokeo ya michuano ya kandanda, tangu mwaka wa 2008.
Mechi ya kati ya Liechtenstein na Finland pia imetiwa dosari
Uchunguzi wa awali uligundua pambano la kuwania nafasi ya kuingia fainali za kombe la dunia kati ya Liechtenstein na Finland Septemba 2009 lilipangwa matokeo na muamuzi kutoka Bosnia, ambaye Umoja wa vyama vya kandanda barani Ulaya-UEFA ulimfungia maisha. Mwaka jana, UEFA ukamfukuza mchezaji wa Malta aliyehusishwa katika kupanga matokeo katika mchuano ya ubingwa wa Ulaya kati ya Norway na Malta mwezi Juni.
Baadhi ya mashabiki wa kandanda
Mkurugenzi wa usalama wa Shirika la kandanda la kimataifa-FIFA Ralf Mutschke, alisema ripoti hiyo inatoa mwangaza wa kuwepo haja kwa maafisa wa kandanda na polisi kushirikiana katika kupambana na rushwa katika kambumbu.
Mutschke alisema wakati FIFA inaweza kuwafungia wachezaji, waamuzi na maafisa wa vilabu, lakini haina nguvu za kuwaadhibu watu ambao hawahusiki moja kwa moja na mchezo huo.
Uchunguzi wa Shirika la EUROPOL, uligundua kiasi ya euro milioni 8 zilizopatikana kama faida kutokana na kamari katika kandanda na euro milioni mbili katika kuwahonga wachezaji na maafisa. Tayari uchunguzi huo umesaidia kufunguliwa mashitaka.
Dw
No comments:
Post a Comment