Shukurani njema zote anastahiki Allah Ambaye ametuwezesha kuwa hai tukiwa na afya njema. Tunamuomba Allah atuwafikishe kufanya mema na aujaalie uhai wetu wote uwe kwa ajili ya kumtumikia Yeye katika Dini hii ya Kiislamu. Rehema na amani ya Allah zimwendee kipenzi chetu, mtukufu wa viumbe Mtume Muhammad (Sallallaahu ‘alayhi wasallam), masahaba zake, jamaa zake na wale wote waliomfuata kwa wema mpaka Siku ya Malipo.
Ama baada ya hayo,Jumuiya ya Maimamu Zanzibar (JUMAZA) inachukua fursa hii kutoa taarifa rasmi kwa vyombo vya habari kufuatia tukio la kupigwa risasi na kuuwawa kwa Padri Mushi wa Kanisa Katoliki Parokia ya Mjini jana tarehe 17/2/2012 Beit – El – Ras.
JUMAZA kwa mshtuko mkubwa imepokea kwa masikitiko taarifa ya kuuwawa kwa Padre Mushin na inalaani kwa nguvu zote kitendo hicho cha kiharamia ambacho kinaashiria kuitia doa Zanzibar kisiwa cha amani na ukarimu tokea enzi na enzi. Kufuatia kadhia hii JUMAZA inawataka Wanzanzibari wote wa dini na madhehebu zote kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu na kuendelea kutunza amani na mshikamano tulionao chini ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kutotoa mwanya kwa watu au vikundi ambavyo vina nia mbaya ya kutaka kuleta kutokuelewana kwa wananchi kwa malengo yao binafsi.
Aidha JUMAZA inaungana na kauli iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuliagiza Jeshi la Polisi nchini kufanya uchunguzi wa kina na waharaka ili kubaini nani waliohusika na tukio hili na hatimaye sheria ichukue mkondo wake.
Aidha JUMAZA inaliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kiuadilifu na usioambatana na shindikizo la mtu au kikundi chochote ili hatimae ukweli halisi ujulikane na bila ya kuwadhuru wasiohusika.
JUMAZA inakemea vikali kauli za baadhi ya vyombo vya habari vinavyonasibisha waislamu na tukio hili na kuvitahadharisha vyombo vya habari ikwemo magazeti na redio hizo kutoanza kutoa taarifa ambazo kwa makusudi zinaweza kupandikiza chuki na uhasama katika jamii na hatimae kuotesha mizizi ya fitna na kupelekea Taifa kuingia kwenye machafuko bali viachiwe vyombo vinavyohusika kufanya uchunguzi wake na kutoa taarifa sahihi. Aidha JUMAZA inaziomba Serikali zote mbili kuwa waamgalifu sana katika kipindi hiki kwa kujizuia kutoa maneno yanayoashiria kuhusisha tukio hili na upande fulani wakati bado uchunguzi unaendelea.
Imesaniwa na:
KATIBU WA JUMAZA
MUHIDDIN ZUBEIR MUHIDDIN.
No comments:
Post a Comment