Taarifa kutoka Zanzibar zikiripotiwa na mwanahabari Donisia Thomas wakati kipindi cha Patapata cha WAPO radio FM kinaendelea, zinasema kuwa Padre Evaristus Mushi wa Kanisa la Parokia ya Minara Mirefu huko Zanzibar amepigwa risasi majira ya saa moja asubuhi -na watu wasiofahamika- na kufariki dunia.
Taarifa za kufariki kwake zimethibitishwa na madaktari kutoka hospitalini alikopelekewa katika harakati za kuuokoa uhai wake.
Padre Mushi aliuawa akiwa anashuka kwenye gari lake tayari kuingia Kanisani kwa ajili ya kuendesha misa ya kawaida ya Jumapili katika kanida la Mtoni, mjini St. Joseph. Inaelezwa kuwa gari lisilofahamika lilifika na kufyatua risasi zilizomlenga Padre Mushi sehemu ya kichwani na hivyo kumsababisha majeraha yaliyokuwa yakivuja damu nyingi.
Mwanahabari anasema tukio hilo limezua taharuki kubwa miongoni mwa waumini ambao wamekataa kuahirisha ibada iliyokuwa iendeshwe na Padre huyo na kusema ikiwa kusudio ni kuwaangamiza Wakristo wote, basi na waangamizi wafike Kanisani wawaangamize wakiwa pamoja.
Jeshi la Polisi limeshafika katika eneo la tukio na kuanza uchunguzi.
Wakizungumza kuhusu hilo, raia wamesema hawana imani na Polisi wala Madaktari na hawatarajii jipya zaidi ya ripoti kuwa suala hili ni la uhalifu kwa kuwa tukio kama hili liliwahi kutokea mwishoni mwa mwaka jana kwa Padre Ambrose kupigwa risasi na taarifa zilisema lilikuwa ni tukio la kihalifu na kwamba risasi hazikutumika jambo ambalo halikuwa kweli kwani Padre Ambrose alikutikana na risasi alipohamishiwa katika hospitali ya Taifa, Muhimbili.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali fuatilia vyombo mbalimbali vya habari.
No comments:
Post a Comment