Saturday, March 30, 2013

Mahakama: Uhuru Kenyatta, Rais halali wa Kenya

MAHAKAMA ya Juu imekataa ombi la Waziri Mkuu Raila Odinga wa CORD la kutaka ibatilishe uchaguzi wa Uhuru Kenyatta wa muungano wa Jubilee kuwa rais. Hii ina maana kuwa Bw Kenyatta sasa ataapishwa kuwa rais Aprili 9. 

“Mahakama ya Juu imefikia uamuzi kwa kauli moja kuhusu masuala manne yaliyoibuliwa kwenye kesi za uchaguzi. Uchaguzi ulifanyika kwa njia huru na ya haki na kwa kufuata Katiba na Sheria,” alisema Jaji Mutunga kabla ya kutangaza kuwa Uhuru Kenyatta na William Ruto walichaguliwa kwa njia huru na ya haki kuwa Rais na Naibu Rais wateule. 

“Kesi za Raila na AFRiCOG zimetupwa. Kila mtu ajilipie gharama. Uamuzi wa kina utatolewa katika muda wa wiki mbili.” 

 Kuhusu kesi ya wanaharakati Dennis Itumbi na Moses Kuria kuhusu kura zilizokataliwa, Jaji Mutunga alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa uamuzi.

Alihitimisha kwa kutoa wito kwa Wakenya wadumishe amani. 

“Mahakama imetekeleza jukumu lake. Jukumu sasa ni kwa raia, viongozi wao, mashirika ya kijamii na wanahabari kuhakikisha umoja wa Kenya unadumu,” alisema Jaji Mutunga. 

RAILA AKUBALI KUSHINDWA, AMTAKIA UHURU KILA LA HERI 

WAZIRI Mkuu Raila Odinga amekubali kushindwa baada ya Mahakama ya Juu kutupilia mbali kesi yake kupinga kupinga kuchaguliwa kwa Uhuru Kenyatta. Bw Odinga amemtakia Rais Mteule kila la heri. 

“Hatua yangu ya kwenda mahakamani ilikuwa ishara ya imani yangu katika Mahakama. Haikuwa ni ya kisasi. 

Tulijaribu kadiri ya uwezo wetu. Mawakili wetu wakiongozwa na Oraro walikusanya na kuwasilisha ushahidi mwingi.

“Tunasikitika kwamba Mahakama ilikataa ushahidi kwa msingi kuwa uliwasilishwa kwa kuchelewa au mahakama haikuwa na muda. Mwishowe, Wakenya walipoteza nafasi ya kujua nini kilitendeka.” 

“Mimi na Kalonzo hatuna majuto kwa kuwasilisha kesi kortini. Ni matumaini yangu kwamba serikali ijayo itaheshimu Katiba na kuitekeleza. 

Namtakia Rais Mteule Uhuru Kenyatta na kundi lake kila la kheri. Pia, maseneta, wabunge, wawakilishi wa wanawake na magavana ufanisi. Tusigawanywe na mtukio haya. Natoa wito kwa Wakenya na wafuasi wangu wakumbuke maneno ya Wimbo wa Taifa – “Haki iwe ngao na mlinzi.”

 Source: http://www.wavuti.com

No comments: