Friday, March 29, 2013

Taarifa ya Jeshi la Polisi kuelekea kwenye sikukuu ya Pasaka

JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI
JESHI LA POLISI TANZANIA

Anuani ya Simu
“MKUUPOLISI”

Ofisi ya  Inspekta  Jenerali wa Polisi,
Simu : (022) 2110734  
                                                                                    
Makao Makuu ya Polisi,
Fax Na. (022) 2135556
S.L.P. 9141,

28/03/2013

TAARIFA YA JESHI LA POLISI  KWA VYOMBO VYA HABARI

1.     KATIKA KUELEKEA SIKUKUU YA PASAKA, INAYOTARAJIWA KUADHIMISHWA KUANZIA TAREHE 29 MACHI  HADI  TAREHE 1 APRILI, 2013.  JESHI LA POLISI LINAPENDA KUWAONDOA HOFU WANANCHI WOTE KUWA LIMEJIPANGA KIKAMILIFU KATIKA KUIMARISHA USALAMA WA RAIA NA MALI ZAO KWA KIPINDI CHOTE CHA SIKUKUU NA BAADA YA SIKUKUU, HIVYO WANANCHI WASHEREKEE SIKUKUU  KWA AMANI  NA UTULIVU, PASIPO VITENDO AMA VIASHIRIA VYOVYOTE VYA UVUNJIFU WA AMANI.

2.    IKUMBUKWE KUWA, WANANCHI WENYE IMANI YA KIKRISTO NA HATA MADHEHEBU MENGINE HUTUMIA MUDA HUO KWENDA KUABUDU PAMOJA NA MUENDELEZO WA SHEREHE HIZO KWENYE MAENEO MBALIMBALI YA STAREHE. UZOEFU UNAONYESHA KUWA BAADHI YA WATU HUTUMIA KIPINDI HICHO CHA SIKUKUU KUFANYA MATUKIO YA UHALIFU KUTOKANA NA MIKUSANYIKO HIYO YA WATU KATIKA MAENEO MBALIMBALI.

3.   JESHI LA POLISI LINAPENDA KUWAONDOA HOFU WANANCHI NA WAUMINI  WOTE KUWA,  ULINZI UMEIMARISHWA KWENYE MAENEO YOTE YA KUABUDIA, FUKWE ZA BAHARI, SEHEMU ZA STAREHE NA MAENEO MENGINE YOTE AMBAYO YATAKUWA NA MIKUSANYIKO MIKUBWA YA WATU.AIDHA, TUNAPENDA KUWATAHADHARISHA WALE WOTE AMBAO WATAKUWA WAKITUMIA BARABARA, KUWA MAKINI KWA KUZINGATIA SHERIA ZA USALAMA BARABARANI NA HASA KWA MADEREVA KUEPUKA KWENDA MWENDO KASI NA KUTUMIA VILEVI WAWAPO KAZINI.

4.     VILEVILE, JESHI LA POLISI LINAWATAKA WANANCHI KUONDOA HOFU NA KUWAPUUZA  WATU WACHACHE AMA KIKUNDI CHA WATU WANAOTUMIA KIPINDI HIKI CHA SIKUKUU KUWATIA HOFU KWA KUSAMBAZA MESEJI ZA VITISHO KWA WATU MBALIMBALI KWA LENGO LA KUVURUGA AMANI NA UTULIVU KATIKA KIPINDI HIKI CHA SIKUKUU. KITENDO HICHO CHA KUSAMBAZA MESEJI ZA VITISHO KWA WANANCHI NI UHALIFU KAMA UHALIFU MWINGINE NA WAKIBAINIKA HATUA ZA KISHERIA ZITACHUKULIWA DHIDI YAO.

5.     KATIKA KUHAKIKISHA USALAMA KWENYE KUMBI ZA STAREHE, WAMILIKI WA KUMBI HIZO WAZINGATIE UHALALI NA MATUMIZI YA KUMBI ZAO KATIKA UINGIZAJI WA WATU KULINGANA NA UWEZO WA KUMBI HIZO, BADALA YA KUENDEKEZA TAMAA YA FEDHA KWA KUJAZA WATU KUPITA KIASI. VILEVILE, WAZAZI WAWE MAKINI NA WATOTO WAO NA HASA DISKO TOTO, ILI KUEPUKA AJALI NA MATUKIO MENGINE YANAYOWEZA KUSABABISHA MADHARA JUU YAO.

6.     JESHI LA POLISI LINATOA TAHADHARI KWA WANANCHI WOTE KWAMBA, WATOKAPO KWENYE MAKAZI YAO WASIACHE NYUMBA WAZI AMA BILA MTU NA WATOE TAARIFA KWA MAJIRANI ZAO, NA PALE WANAPOWATILIA MASHAKA WATU WASIOWAFAHAMU WASIKAE KIMYA BALI WATOE TAARIFA KWA JESHI LA POLISI AU VIONGOZI WAO WA SERIKALI YA MTAA, SHEHIA, KIJIJI AU KITONGOJI ILI HATUA ZA HARAKA ZIWEZE KUCHUKULIWA.

7.     MWISHO, NAPENDA KUWAHAKIKISHIA WANANCHI KWAMBA, JESHI LA POLISI LINATEKELEZA MAJUKUMU YAKE KWA KUZINGATIA SHERIA ZA NCHI NA HIVYO HALITAWAJIBIKA KUMWONEA HURUMA AMA UPENDELEO MTU YEYOTE ATAKAYEENDA KINYUME NA SHERIA ZA NCHI.

NAWATAKIENI WATANZANIA WOTE PASAKA NJEMA.
    
IMETOLEWA NA:
ADVERA SENSO
MSEMAJI WA JESHI LA POLISI (T)

No comments: