Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Dk. Edward Hoseah amelipuka na kuhoji kwanini anaambiwa ashughulike baadhi ya makosa ya rushwa na mengine hapana.
Kauli hiyo imeonekana kusigana na Jaji Kiongozi, Fakihi Jundu, kuhusu haki ya Taasisi hiyo kupewa mamlaka ya kushitaki watuhumiwa wa rushwa kubwa.
Malumbano hayo yalizuka baada ya Dk. Hoseah, kusema chombo hicho (Takukuru) kimefungwa mikono kwa kuzuiliwa kushtaki makosa makubwa.
Dk. Hoseah alieleza kukerwa huko mjini Dodoma jana wakati akijibu hoja mbalimbali za wabunge katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wabunge cha Kupambana na Rushwa Afrika, (APNAC), tawi la Tanzania.
“Kwanini unaniambia nishughulikie baadhi ya makosa na mengine hapana…Sheria ambayo inahusiana na Takukuru ambayo mliitunga wenyewe waheshimiwa wabunge section (kifungu) cha 15 ndiyo tunayoruhusiwa kushtaki haya ni makosa ya dagaa wadogo,”
Alisema na kuwafanya wabunge kusikitika.
“Nikija kwa wakubwa mnaniambia stop (simama). Kwa mtu yeyote mwenye akili hizi hoja zinazotolewa kuhusiana na mamlaka ya kushtaki hawezi, mimi sizielewi kabisa zinataka tusipambane na rushwa,”alisema.
Aliwashangaa wanaohoji suala la kuendesha mashtaka ya rushwa kuwa chini yao kwa sababu hata mfumo unaofuatwa nchini Uingereza umebadilika ambapo suala la kushtaki mambo ya rushwa yapo chini ya taasisi husika.
Alisema Katiba inatambua vyombo mbalimbali kama Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) lakini kasoro iko kwa Takukuru ambayo amebaki kuwa mtoto yatima.
“Hivi tukisimama hapa mbona hamtuelewi tu? Sisi tukiuliza tunaambiwa kuwa tusubiri serikali tatu, haya ni majibu mepesi na sasa niwaambie kuwa CAG hawezi kuhojiwa na chombo chochote,”alisema.
Alisema katika kipindi cha miaka sita aliyokaa katika chombo hicho ameinua kwa kiasi kikubwa weledi wa watumishi wake na si kwamba chombo hicho hakina wanasheria wanaoweza kuendesha kesi kubwa za rushwa.
“Si kwamba hatujaweza, wanasheria wa mahakamani ni wale wale wa DPP (Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali) ni wale wale wa Takukuru .Tumesoma wote ina maana majaji wa mahakama kuu wanatofautiana na wale wa rufaa? Hawa ina maana wamesoma (special school) shule maalum,”alisema.
Alisema watalaam hao wote wamesoma shule zile zile na kwamba haiwezekani watumishi wa Takukuru wakawa na uwezo mdogo labda aambiwe kuwa wamesoma shule za vihiyo.
“Kwanini tusipewe, tupeni muone tutakavyofanya kazi. Hawawezi kushindwa kuendesha mashtaka kama elimu sote tunaipata tumesoma huko huko walikosoma wao kwani sisi tumesoma katika shule za vihiyo?” alihoji. Aidha, alimtaka Jaji Kiongozi kuhakikisha masuala ya majaji na mahakimu wanaoendesha kesi kubwa zinazogusa maslahi ya umma wanaifanya kazi hiyo bila kupumzika.
“Wamekuwa wakitafuta sababu nyepesi za kuahirisha kesi mara moja na jaji anasoma masters (Shahada ya Udhamili) Mzumbe kwa hiyo ameshindwa kuja kesi inaahirishwa, unajua anasoma kwanini umpangie kesi ambayo ina maslahi kwa Taifa?” alihoji Dk. Hoseah.
Alitoa sababu nyingine ambazo zinasababisha kesi kuahirishwa kuwa wakili kufika mahakamani na kutoa sababu ya kuwa na kesi nyingine Mahakama Kuu na hivyo jaji anaahirisha kesi.
Alisema Takukuru imekuwa ikigharamikia mashahidi wanaofika mahakamani kwa ajili ya kuleta ushahidi hivyo kuahirishwa kwa kesi hizo kunawasababishia gharama kubwa za kuendesha kesi. Alitoa mfano wa kesi ya aliyekuwa balozi wa Italia, Profesa Costa Mahalu, ambayo ilichukua miaka saba.
MAMBO SITA YA KUZINGATIA
Dk. Hoseah alisema kutokana na uzoefu alioupata kutoka nchi mbalimbali katika masuala ya kupambana na rushwa lazima mambo sita ya kuyatekeleza.
Alisema miongoni mwa mambo hayo ni uongozi ambao unategemea mtu aliyeingia madarakani ana lengo la kupata nini kutokana na nafasi yake ama kuwatumikia wananchi.
“Je, viongozi wetu wote waliingia madarakani kuwatumikia wananchi?... ukishakuta katika system ukitaka kumshtaki mtu ooh kimekuwa vile, ooh unajua kilikuwa vile, hapo huwezi kupambana na rushwa, “alisema.
Alilitaja jambo jingine kuwa ni uwazi katika uwajibikaji ambapo alitoa mfano wa uingiaji wa mikataba mikubwa nchini ambayo ni sera na manufaa
“Si sahihi kusema kwamba watu watanufaika na rasilimali asilimia ngapi?
Usiri uko katika mikataba lakini wananchi wananufaike ama sera nayo inakuwa siri hapana!,” alisema.
Alisema pia ni lazima kuwapo na sheria ya uhuru wa kupata taarifa.
Aidha kuwapo na uwajibikaji wakati mambo yanapoenda ovyo hata kama kiongozi hahusiki na kosa hilo akubali kujiuzulu.
Alisisitiza kuhusu uwapo wa demokrasia ya kweli katika mapambano dhidi ya rushwa. “Demokrasia lazima ionekane kama mtu akitembea anakamatwa na kuwekwa ndani hiyo siyo demokrasia,” alisema.
Alisema lazima kukubali na kusikiliza tofauti za kimawazo kama mtu hakubaliani nalo.
JAJI KIONGOZI NAYE ALONGA
Kauli hiyo ilionekana kutofautiana na ile ya Jaji Kiongozi, Jundu, ambaye alitaka kuendelea kuitafakari hatua ya kuipa mamlaka Takukuru kushitaki watuhumiwa wa rushwa kubwa kwa sababu katika masuala hayo lazima kuwe na mizania (check and balance).
No comments:
Post a Comment