Monday, December 31, 2012

Kutamani Maendeleo Bila Juhudi, Ni Kutaka Kuvuka Bahari Ya Hindi Kwa Mtumbwi Uliotoboka.

Na:Meshack Maganga-Iringa
Ndugu zangu, 
Inasemwa na wanataaluma kuwa, elimu ndio njia ya uhakika ya kumuweka mtanzania wa kawaida kwenye daraja la kati kuliko njia nyingine nyingi zinazofahamika. Kwa mantiki hiyo inafaa zaidi watanzania wengi wapate elimu yenye lengo la kuwakomboa, kifikra na kiujuzi na hatimaye waelimike kwa lengo la kuwasaidia kwa maana ya kuwatumikia wananchi wenzao wengi.
Nilisoma moja ya makala ya ‘mentor’ wangu  Maggid Mjengwa yenye kichwa  ‘Tunawapitsha Watu Wetu Kwenye Njia Yenye Matope Kwanini’? kwenye makala hiyo  amemnukuu Marehemu Mzee Jongo aliyepata kusema , Kusoma si kuufuta ujinga,bali ni kuupunguza. Halafu akaendelea kwa kusema, kila binadamu ana ujinga wa jambo moja au mia moja,kuwa na ujinga wa jambo si kosa. Nina ongezea kwa kusema mwanadamu asiye jitambua na kuishi maisha kama nakala ya gazeti ana matatizo.
Je vipi kuhusu binadamu, kwanini binadamu fulani anaishi, kwanini Fulani alizaliwa duniani? Kwa maswali hayo kila mmoja atapata picha kuwa hakuna binadamu aliyeletwa duniani bila malengo au madhumuni fulani, hivyo basi kila binadamu ana malengo au madhumuni fulani ya kuishi duniani. Hakuna kiumbe chochote kilichopo duniani kisicho na madhumuni fulani ya kipekee.
Je ni binadamu wangapi wanaishi maisha yaongozwayo na malengo? Maisha yasiyoongozwa na malengo hayana maana yoyote, maisha huwa na maana pale yanapoongozwa na malengo.Na binadamu yeyote anayeishi  maisha yanayoongozwa na malengo huleta tofauti kubwa katika maisha na dunia nzima.
Tunaishi katika utamaduni uliojaa vitu na anasa ambazo kwazo mafanikio yetu hupimwa kwa vitu tunavyovifanya au mali tunayochuma. Kutokana na hali hii maisha yetu ya kila siku yanakabiliwa na mambo ya kufanikisha na malengo ya kutimizwa. 

Mawazo yetu wakati wote yanalenga vitendo. Ukitazama sekta zote, viwandani maofisini, mashambani, mashuleni, vyuoni na hata majumbani mwetu, msisitizo mkubwa unawekwa katika malengo na namnaya kuyafikisha malengo hayo. Lakini malengo yenyewe ni ya kupata vitu vinavyoshikika. Kwa mfano, kutengeneza bidhaa mpya, kuongeza soko la bidhaa zao n.k. Vyuoni huweka malengo ya kuanzisha program mpya, au kuongeza nafasi za hosteli, n.k. kuwasomesha watoto waliopo, kujenga nyumba, kununua gari n.k. 

Hata hivyo, watu hupishana katika malengo. Baadhi ya watu wanaamini kufanikiwa ni kuchuma au kulimbikiza mali. Wengine kwao kufanikiwa ni kupata watoto, wengine kusoma hadi kupata digrii ya Chuo Kikuu, wengine kufanikiwa ni kuokoka,na wengine mafanikio ni kuhama kutoka kanisa moja kwenda jingine wengine ni kujiunga na mtandao wa kijamii kama ‘face Book,wengine mafanikio ni kula nyama kila siku n.k.

Mshauri namba moja wa mambo ya kijamii na mafanikio, Kopmeyer, katika kitabu chake ‘Thoughts To Build On’,na ‘Here Is Help’ anasema,  mafanikio yanaanza na mambo matatu. Kwanza, Lazima mtu awe na  utashi utakaomfanya aamini kwamba nayeye anaweza kufanikwa. Hamasa hii  ndiyo chachu ambayo hufananishwa na   roketi iendayo mwezini, yaani lengo analokusudia.

Pili, Lazima mtu awe na hamasa ya kutafuta taarifa anazohitaji kujua na kuzifanyia kazi ili aweze kujihakikishia mafanikio. Lakini shughuli yoyote ile hata iwe inahamasisha kiasi gani inaweza kuwa na matokeo mazuri au mabaya. Kwa hiyo, kabla mtu hajakurupuka na kuanza kukimbia kuelekea upande usiofaa, Lazima ahakikishe Nia na utashi  wake umemhamasisha yeye kwa kiasi cha kutosha cha kumfanya awe tayati kulipa gharama ya mafanikio yake ili kufikia malengo aliyojiwekea kabla ya kuanza kufanya lolote. Lazima kuwepo  na lengo - na lengo lenyewe Lazima liwe limeamuliwa kabla ya kuanza hatua za kulifikia. Vinginevyo atakuwa amekusanya taarifa ambazo hatazitumia baadaye.

Kila unachokitaka katika maisha kina gharama yake. Gharama hii siyo Lazima iwe katika fedha. Ingawa wakatiwote fedha zinaweza kuhusika. Ni gharama nyingine zinazohitaji ili kuleta mafanikio ndiyo unapaswa kuwa tayari kuzibeba. Gharama hizi ni pamoja na kuwa tayari kujitolea muhanga wewe binafsi katika muda wako, juhudi zako, katika kujifunza, katika kupanga mambo yako, kutafuta ufumbuzi na kufanya yale yanayopaswa kufanywa na katika wakati unaopaswa kufanya. kama anavyodai Komeyer, mara nyingi elimu ya madarasani hushindwa kutoa hamasa ya aina hii.   

Juzi,nilipokuwa Mjini Mbeya, nimekutana na mwanafunzi wa kidato cha sita,alipata kusoma makala zangu siku za nyuma. Kwa muda wake wa ziada analima bustani ya mboga nyumbani kwao kila atokapo shule, hutumia nusu saa kujishughulisha na bustani yake,anatambua umhimu wa muda, anafahamu kwamba bila yeye hakuna mjomba wala mfadhili atakaye mkomboa. Ameweka lengo la kuwa mjasiriamali mwenye malengo, kwa kipindi cha miaka mitano ijayo anategemea kufanya maajabu katika dunia ya wajasiriamali.

Tatu, pamoja nayo  kuna jambo jingine muhimu, nalo linahusu fomyula ya mafanikio. Lazima mtu awe na fomyula rahisi ya kumuwezesha kufikia malengo yake.

 Tanzania, na nchi nyingine za dunia ya tatu kama hii ya kwetu, kuna taasisi nyingi za kifedha ambazo zinasaidia watu wenye kipato cha chini kwa kuwapatia mikopo, lakini wengi wa wanaokopeshwa bado hawana elimu ya utambuzi na wengi wao hawana malengo,hawafahamu tofauti iliyopo kati ya mikopo mizuri na mikopo hatari (good debit and bad debit). Baadhi ya wanaopewa mikopo wananunua nguo na wengine wananunua vifaa vya ndani,na wengine wanaenda mbali na kununu simu,na orodha ni ndefu hapa.

Lakini tujiulize: (1) Je, watu hawa wanaokusudiwa wana nia ya kutosha kuwashawishi kwamba umasikini ni mbaya na ni Lazima waondokane nao? (2) Je, watu hawa wamehamasishwa vya kutosha kiasi cha wao kuamini kwamba wanaweza kupambana na umasikini na kuuondoa wao wenyewe, na kwamba kazi ya serikali au wafadhili ni kuwaunga mkono tu, lakini wao wenyewe ndiyo wanatakiwa kuwa washiriki wakuu? (3) Je, watu hawa wanao ujuzi au stadi zitakazowasaidia kufanya yale wanayotaka kuyafanya ili kuondokana na umasikini? 

Ni dhahili mipango yoyote yenye lengo la kumkomboa mwananchi,  kama vile MKUKUTA, haiwezi kufanikiwa endapo mambo haya matatu hayatazingatiwa ipasavyo. Mitaji ya fedha peke yake, haiwezi kuwaletea mafanikio walengwa bila  kuwepo kwamba mambo haya ambayo kwa mtazamo wangu ni mhimu walengwa wa mikopo na misaada hiyo wakipewa elimu ya kujitambua na kujiamini. 
Kwa mafano, kama mtu anadhani au anaamini, kutokana na sababu yoyote ile, kama vile kulogwa au Mungu ndiyo alivyompangia kwamba umasikini ndiyo stahili yake, huwezi kumsaidia mtu huyu kuondokana na umasikini. Ukimpa mtaji wa fedha atakula na kubaki maskini. Kama mtu anaukataa umasikini lakini hayuko tayari kujituma kufanya kazi kwa bidii, naye huwezi kumsaidia. Kama mtu anaukataa umaskini, na yuko tayari kujituma kwa kufanya kazi kwa bidii, lakini hana ujuzi au stadi wa kufanya anachokusudia kuondoakna na umasikini, pia mtu huyu hawezi kuondokana na umasikini huo.

Tutabuni miradi mingi,yapo mashirika mengi yasiyokuwa ya kiserkali (NGO), tutabuni sera za kila aina zenye ubora usiyo na kasoro hata moja,tutaanzisha vyuo vikuu  kila mkoa na kila wilaya na kila kata, na kozi za kila aina na wanafunzi watapewa mikopo (madeni) lakini bila elimu ya kujitambua na kujifahamu ni kazi bure, ni kutaka kuvuka bahari ya Hindi kwa mtumbwi uliotoboka. Tunao wanafunzi wengi waliohitimu vyuo vikuu miaka nenda rudi hawana kazi, hawana cha kufanya,wamekuwa mzigo kwa taifa na kwa familia,wengi wao wamekuwa washabiki wa siasa za bongo.Wengine wanajivua magamba na wengine wana vaa magwanda.Ili mradi kunakucha. 

Ndiyo- Binadamu aliyeamua kupata kitu fulani maishani hajui sababu za kushindwa na wala hana sababu zinazoweza kumzuia.

Utafiti uliofanywa na Jenny Fulbright, ‘10 Secrets on Successful Entrepreneurship’  anasema mafanikio yapo kwa ajili ya mtu yoyote,  lakini ili mtu afanikiwe Lazima ajue au azingatie mambo 10 yafuatayo... (Itaendelea Jumatatu Ijayo)  

No comments: