Thursday, July 19, 2012

Zito Aanzisha Umoja Wa Wasanii Kigoma...!


 Vicky Kimaro
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini kupitia tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe ameanzisha umoja wa wasanii wa muziki wa Kigoma ambao wamerekodi nyimbo ya pamoja inayoitwa 'Leka Dutigite' wakimanisha 'Tunajidai' ambayo itazinduliwa Julai 17 mkoani Kigoma.

Umoja huo ambao mwenyekiti wake wa muda ni Mwasiti Almasi unajulikana kama 'Kigoma All Stars' na unaundwa na Mkurugenzi wa Asset 'Twanga Pepeta', Asha Baraka, Abdul Nasib 'Diamond Platinum', Ommy Dimpoz, Chege Chigunda, Recho, Baba Levo, Linex, Abdul Kiba, Queen Darleen, Peter Msechu, Hassan Rehani na wengine wengi.

Akizungumzia lengo la kuanzisha umoja huo Zitto alisema amekuwa akiguswa na kilio cha wasanii hasa baada ya msanii wa filamu, Juma Kilowoko 'Sajuki' kuumwa na kukosa fedha za matibabu.

Zito alisema kitendo hicho kilimlazimisha Sajuki kuomba msaada wa fedha kwa wasamaria wema ili akapatiwe matibabu nchini India.

"Inasikitisha sana kuona msanii mkubwa, lakini maisha anayoishi hayalingani na jina lake, nataka ifike mahali wasanii waheshimike, najua mmekuwa mkihangaika kusaka maonyesho kwa sababu ndiyo yanawalipa na  albamu hazilipi, hivyo naomba kuanzia sasa tujipange kufungua kampuni ambayo nyinyi mtakuwa wana hisa,"alisema Zitto huku akishangiliwa na wasanii hao.

Zitto aliwamaliza wasanii pale alipowauliza, "kuna msanii kati yenu amekata NSSF hapa?"aliuliza na kupokelewa na ukimya uliotanda kwa wasanii wote na kisha Linex alisema kwa utani 'Labda Mwasiti' kitendo ambacho kilifanya wasanii wote waangue kicheko kitu ambacho kilimsikitisha mbunge huyo wa Chadema

Wasanii hao walisema hakuna hata mmoja mwenye NSSF kwa vile hawajui utaratibu ukoje na hawana mtu wa kuwaongoza katika suala hilo kitendo ambacho kilimlazimu mbunge huyo kutoa ahadi ya kuwakatia NSSF wasanii hao wa Kigoma na kwamba Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki atawapatia kadi zao atakapoudhuria tamasha la wasanii hao kwa vile ndiyo atakuwa mgeni rasmi.

"Mapato yote yatakayopatikana kutokana na tamasha hili yatachangia NSSF zenu na pia kila msanii hapa kati yenu aangalie wimbo wake mzuri uliotamba auorodheshe ili mtengeneze albamu ya pamoja ambayo itauzwa na mapato yataingia kwenye NSSF,"alisema Zitto na kushangiliwa na wasanii hao.

"Katika suala la Kampuni nitaisajili na itakuwa na mwanasheria ambaye atasimamia kazi zenu, mwisho wa mwaka mtagawana mapato kwa sababu kuna wakati unaweza toa nyimbo isiuze na kuna wakati ukatoa ikauza, mkifanikiwa nyie najua mtakuja kunipa sapoti kwenye kampeni zangu hata nikija nikiwambia bajeti yangu ya kampeni ni Sh 200 milioni najua mtanisapoti bila wasiwasi, lakini kwanza mfanikiwe bila hivyo hamtaweza.

Wasanii hao pia watachangia mfuko wao wa NSSF kupitia mapato yao yanayotokana na nyimbo zao  'ring tone' kwenye simu za mkononi. 

Chanzo:www.mwananchi.co.tz

No comments: