CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetangaza kuwa Katibu Mkuu wake, Dk Willbrod Slaa atapewa fursa ya kuwania nafasi ya Urais kwenye uchaguzi mkuu ujao, mwaka 2015.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza hatua hiyo jana, alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara katika Uwanja wa Mpira, mjini Karatu mkoani Arusha, huku yeye akijiweka kando kuwania nafasi hiyo.
Hata hivyo, Dk Slaa mwenyewe alipoulizwa iwapo ana nia ya kugombea urais mwaka 2015, alisema: “Kwani mwaka 2010 nilijitangaza mwenyewe?, Iwapo wanachama wa Chadema watanipendekeza, nitafikiria kufanya hivyo.”
Katika maelezo yake Mbowe alisema: “Kama Mwenyezi Mungu atampa uhai na afya njema hadi mwaka 2015, Dk Slaa anatosha na Chadema, tutampa fursa nyingine ya kupeperusha bendera ya chama kwenye nafasi ya urais.”
Huku akishangiliwa na umati wa wana chama wa Chadema Mbowe aliongeza: “Ninataka wanaotumia ugombea Urais kama kete ya kuleta mtafaruku ndani ya Chadema watambue hivyo.”
Alibainisha kuwa, binafsi hana nia ya kuwania urais na badala yake atatumia nguvu, uwezo na kila kilicho ndani ya uwezo wake, kukijenga Chadema ili kushinde uchaguzi na kushika dola.
Mbowe alisema kwa muda mrefu kumekuwapo mbinu na jitihada za kumgombanisha yeye na Dk Slaa kuhusu nafasi ya urais na kutamba kwamba njama hizo kamwe hazitafanikiwa.
Mwenyekiti huyo wa Chadema alitumia pia mkutano huo kutangaza kumalizika kwa mgogoro uliokuwapo kati ya viongozi wa chama hicho wilayani Karatu.
Hata hivyo, awali katika mahojiano maalumu na gazeti hili, Mbowe alisema: “ Kikao cha CC (Kamati Kuu), kitakachofanyika Januari mwakani ndicho kitakachoweka utaratibu rasmi wa watu wanaotaka kuwania kiti cha udiwani, ubunge na urais mwaka 2015 na kutangaza nia zao na vigezo vya uteuzi.”
Alisema chama hicho kinakusudia kuwapa nafasi wenye nia kujitokeza mapema, ili kutoa fursa ya kuwaelewa, kuwaandaa, kuwapa mafunzo, kuwaeleza majukumu na wajibu wao, kuwaeleza sera, misimamo na malengo ya chama hicho.
Mbowe alisema kuwa mpango huo utakihakikishia Chadema wagombea wenye uwezo na uhakika wa kushinda mwaka 2015.
“Nia ya mpango huu ni kuepuka watu wanaodandia kuomba uteuzi wa kugombea dakika za mwisho,” alisema Mbowe.
Aliweka wazi kuwa chama hicho kitakuwa makini katika uteuzi wa nafasi ya urais kwa sababu ni nafasi nyeti, isiyohitaji kujaribu wala mzaha.
mwananchi
No comments:
Post a Comment