MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),
Dk. Edward Hoseah amesema hawezi kusalimu amri katika nafasi yake kwa
sababu yeye ni mpiganaji.
Dk. Hoseah alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa wiki hii alipokuwa akizungumza
katika kipindi cha ‘Dakika 45’ kinachorushwa hewani na kituo cha
Televisheni cha ITV alipoulizwa kuwa haoni kauli yake aliyoitoa hivi
karibuni wakati akizungumza na wakuu wa madhehebu ya dini kuwa rushwa ni
janga la kitaifa inaonyesha kuwa ameshindwa kazi.
“La hasha, siwezi kusalimu amri kwa sababu mimi ni mpiganaji nawe
unafahamu. Nilisema rushwa ni janga la kitaifa kwa kwa sababu kubwa
tatu; kwanza haibishaniwi kuwa rushwa bado ni kero, kero kwa wananchi wa
kawaida, kero kwa maana ya taifa, kero kwa maana bado ni tatizo na
hivyo kuna haja kabisa ya kuongeza bidii zaidi kuliko bidii zilizopo ili
kuifanya rushwa iweze kushughulikiwa ipasavyo,” alisema Dk. Hoseah.
Alisema pia kumekuwepo na majanga mengine nchini, akatolea mfano janga
la ukimwi na kwamba taifa limeweka msisitizo mkubwa kwenye kampeni,
uwezeshwaji na wananchi kushirikishwa na kuamka hivyo kwa mantiki hiyo
alidhani katika mtazamo wake kwamba rushwa ikifanywa kwa mrengo wa namna
hiyo (janga la kitaifa) anafikiri itapungua kwa kiasi kikubwa kuliko
ikaachiwa TAKUKURU peke yake kana kwamba ni tatizo lake pekee.
“Janga la taifa ni kama mnavyoona ukimwi, kila mtu sasa ashiriki, kila
mtu aogope kutoa rushwa, tatu; ili kutatua tatizo ambalo ni janga lazima
wananchi na jamii washirikishwe na ndiyo maana utatambua kuwa
nilizungumza haya wakati naongea na wakuu wa madhehebu ya dini na
wamenielewa sana na hasa nilipotamka kuwa ni janga la taifa,” alisema
Dk. Hoseah.
Alieleza kuwa viongozi hao wa dini wamekubali kuchukua sehemu yao ya
kuhakikisha kwamba wanawahubiri waumini wao kwamba rushwa ni dhambi na
namna gani ya kuachana kabisa na rushwa.
Pamoja na mambo mengine, alisema Tanzania ni nchi na Mwenyezi Mungu
ameibariki hivyo Watanzania wanapaswa kutambua hiyo kwamba nchi yao ni
kubwa yenye misitu, hali ya hewa nzuri, maziwa makubwa hivyo wasijisahau
wakaliacha tatizo la rushwa likatawala maisha yao yote.
No comments:
Post a Comment