Tarehe 23 mwezi aprili mwaka huu majira ya saa mbili
usiku nilipokea ujumbe wa maandishi katika simu yangu kutoka kwa jamaa yangu
mmoja akinishtua niangalie habari katika chaneli ya ITV. Wakati huo mimi
nilikuwa naangalia katika chaneli nyingine. Bahati mbaya sikuweza kukiona
kipande cha habari hiyo.
Hamadi!! Nilifanikiwa kuiona habari hiyo, ingawa
nilichokiona sikuamini macho yangu. Nilidhani naota. Siku ya pili yake
ilinibidi niingie katika youtube ili kuthibitisha kile nilichokiona kama ni
kweli au zilikuwa ni ndoto.
Habari niliyoiona iliniumiza sana kana kwamba ni
mimi ndiyo nilitendewa kitendo kile. Nilishuhudia kijana mmoja anayeonekana
kuwa na akili timamu kabisa akimkunja askari wa usalama barabarani aliyekuwa
akitimiza wajibu wake na kumnyang’anya ufunguo wa gari.
Kitendo kilichofanywa na kijana Yule ambaye sijui
nimuite kwa sifa ipi ili imfae ni cha udhalilishaji wa hali ya juu kwa binadamu
na kwa jeshi la polisi kwa ujumla wake. Nilitafakari na sikupata jibu. Ni nani
asiyejua umuhimu na unyeti wa jeshi la polisi katika uhai wa jamii yoyote ile.
Ni nani anayeweza kushabikia pindi anapoona jeshi la polisi linagaragazwa?
Katika siku za hivi karibuni vitendo vya
kuwadhalilisha polisi na jeshi la polisi vimekuwa vikiongezeka sana. Miaka
michache iliyopita, mfanyakazi katika ubalozi wa nchi moja ya Ulaya alifikia
hatua ya kumtemea mate askari wa usalama wa barabarani kwa kuwa tu askari huyo
alimsimamisha baada ya raia huyo wa kigeni kwenda kinyume na sheria
zinazoongoza matumizi ya barabara. Si hayo tu, bali pia mwaka 2010 tulishuhudia
mgombea mmoja wa ubunge akimkata mtama mkuu wa polisi wa wilaya moja katika
moja za wilaya hapa nchini.
Ni vigumu sana kupita mwezi mmoja kama hujasikia
askari wa polisi ameshambuliwa na watu wakati akitimiza wajibu wake. Wapo
wanaouawa na mbaya zaidi wananchi wanathubutu hata kuvamia vituo vya polisi na
kuvichoma moto.
Tumeshuhudia kuchomwa moto kwa kituo cha Hedaru
ambapo mali na nyaraka za serikali ziliteketezwa, lakini pia tumeshuhudia
mauaji ya askari wakiwa wanatekeleza kazi zao. Wananchi pia walimuua askari
mkoani Tabora mwaka 2011 wakati akiwa katika operesheni ya kuteketeza mashamba
ya Bangi.
Huwa najiuliza, je ujasiri huu wa raia katika
kuwadhalilisha polisi, unatoka wapi? Inakuwaje kila anayesaka umaarufu mbele ya
watu basi hakuna pa kuupatia zaidi ya polisi? Ukienda katika mikutano ya
wanasiasa, ni vigumu kukuta mkutano umemalizika bila kuwatupia madongo polisi.
Wasanii hasa wa vichekesho (comedians) huwa hawaamini kama kazi yao imekamilika
kama hawataweka kejeli kwa jeshi la polisi.
Udhalilishaji huu kwa sasa unachupa mipaka hadi sasa
vibaka nao, wanadhani wanaweza kuwachezea polisi.
Tunaweza kutafakari kwa pamoja. Kama inatokea mtu
mwenye akili timamu anaweza kumdhalilisha askari mwenye sare kwa kumkunja
mchana kweupe mbele ya kadamnasi, atashindwa vipi kumpiga na hata kumchania
sare au kumnyang’anya silaha pale atakapokutana nae vichochoroni?
Lakini pia, tunaweza kujiuliza! Kama anaweza
kumkunja polisi namna ile, je ikitokea amekasirishwa na raia mwenzake atampa
adhabu gani?
Cha ajabu ni kuwa, watu hawa wanaolidhalilisha jeshi
la polisi, wanashindwa kufahamu kuwa ujasiri wote walionao unatokana na kazi
nzuri inayofanywa na jeshi la polisi katika kuhakikisha kunakuwepo na amani na
usalama katika nchi yetu.
Watu hawa wanadhani vitendo wanavyovifanya kwa
askari wetu labda vitawajengea woga katika kutimiza majukumu yao. Wanasahau
kuwa hizo ni changamoto katika kazi na kwamba vitendo hivyo ndo vinajenga na
kuamsha ari ya askari katika kupambana na uhalifu wa aina yoyote katika jamii
yetu.
Wanasahau kuwa kama usalama usingekuwepo,
inawezekana hata huo muda wanaoutumia katika kuwadhalilisha askari na jeshi
zima la polisi wasingeupata.
Baadhi yetu wananchi hatuelewi dhana ya polisi jamii
na pia dhana nzima ya Utii wa sheria bila Shuruti. Tunadhani, Utii wa Sheria
bila Shuruti kunatokana na polisi kushindwa kutumia maguvu. Uhuru tunaopewa na
jeshi la polisi tunautafsiri kama uoga na kushindwa kutimiza majukumu kwa jeshi
hilo.
Tunasahau kuwa lengo la utii wa sheria za nchi bila
shuruti ni kupunguza uhalifu na matumizi ya shuruti katika usimamizi ya utiifu
wa sheria za nchi. Lakini pia utaratibu huu pia unasaidia kupunguza gharama
katika oparesheni za kupambana na uhalifu.
Watu hawa wanapendelea jeshi la polisi linalotumia
maguvu kama polisi wa kikoloni, ambapo polisi na raia walikuwa na mahusiano ya
kiuadui. Raia alipokuwa akimuona polisi hata kama hana kosa, alikuwa akitimua
mbio.
Askari naye ni binadamu. Anatakiwa apewe haki zake
zote na heshima yake kama binaadamu. Kumdhalilisha askari ni kuidhalilisha
serikali.
Binafsi nimekuwa nikifuatilia sana ripoti za kituo
cha Sheria na haki za binaadamu (LHRC). Katika taarifa zake za haki za
binaadamu, sijawahi kukuta mahali walipoelezea ukiukwaji mkubwa wa haki za
binaadamu unaofanywa na wananchi wakora kwa askari wetu. Swali za kujiuliza ni
hili! Je, hawaoni ukiukwaji wa haki dhidi ya polisi? Au wanaona lakini
wanafumbia macho ili polisi wachukue hatua katika kujihami na wao wapate cha
kusema?
Wanaharakati ambao ninaamini kwa sauti waliyonayo
wanaweza kukemea utovu wa nidhamu unaofanywa na raia dhidi ya askari. Watumie
nafasi waliyonayo katika jamii katika kuhakikisha kuwa wananchi, wanaheshimu
sheria kwa kuwaacha askari na watumishi wengine wafanye kazi zao walizokabidhiwa
na umma.
Nimalizie makala haya kwa kuwaomba askari
wasifadhaike kwa matukio yanayofanywa na raia wachache wasiothamini kazi nzuri
ya polisi. Raia wema tupo nyuma yenu na tunathamini na kutambua kazi zenu.
Endeleeni katika kuilinda nchi yetu. Zidisheni mapambano dhidi ya
wahalifu popote pale walipo bila woga wala huruma. Pia niwapongeze askari wetu
kwa uvumilivu mkubwa walionao, hii ni ishara kuwa wamefunzwa na wameiva. Na
kwamba wapo tayari kukabiliana na changamoto yoyote inayojitokeza kwao kwa sura
yoyote ile.
No comments:
Post a Comment