WAMTAKA ACHUKUE HATUA DHIDI YA MAUAJI YA RAIA KINYUME CHAKE SERIKALI INAHUSIKA
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete kikimtaka achukue hatua dhidi ya matukio kadhaa ya mauaji ya raia yaliyotokea kwa nyakati tofauti katika mikutano yake ya hadhara kwenye Mikoa ya Singida, Tabora, Arusha, Morogoro, Iringa.
Hatua kilichopendeza ni pamoja na kuwawajibisha viongozi wenye dhamana; Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Polisi, IGP Said Mwema; Mkuu wa Operesheni Maalumu Polisi, Paul Chagonja, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda.
Barua hiyo ya Septemba 10, mwaka huu iliyoandikwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe baada ya kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho, imemtaka Rais Kikwete kuwafukuza kazi watendaji hao katika Serikali yake kwa kuwa wameshindwa kazi.
Kimesema kwamba mauaji mengi miongoni mwa hayo, yametokea bila hatua stahiki za kisheria kuchukuliwa na kusema kwamba ukimya huo unaweza kutoa picha potofu kwa umma kwamba Serikali yake inaunga mkono au imewatuma polisi au watu wengine waliosababisha mauaji hayo.
Matukio ya vifo ambayo chama hicho kimetaka yachunguzwe ni pamoja na lile la Januari Mosi, mwaka jana mkoani Arusha, Igunga (Novemba, mwaka jana) na Arumeru Mashariki (Aprili, mwaka huu).
Mengine ni lile la Iramba lililotokea Julai 14, mwaka huu, Morogoro (Agosti 27, mwaka huu) na Iringa Septemba 2, mwaka huu ambalo hata hivyo, shauri lake limeshafikishwa mahakamani.
Kimedai kwamba katika Uchaguzi mdogo wa Arumeru Mashariki, Kiongozi wa Kata wa chama hicho, Msafiri Mbwambo alichinjwa huku chanzo cha kifo hicho kikielezwa kuwa ni masuala ya kisiasa.
Pia kilielezea mauaji yaliyotokea katika Kijiji cha Ndago, Wilaya ya Iramba, Singida na kudai kwamba kikundi cha watu kilivamia mkutano wa Chadema kwa mawe na kwamba licha ya polisi kuwapo eneo hilo, hawakuchukua hatua zozote.
Chama hicho pia kimekumbusha mauaji ya mfuasi wake mkoani Morogoro, Ally Zona kikisema kifo hicho pia kina utata kwani taarifa ya polisi imesema alikufa kwa kugongwa na kitu kizito wakati chama hicho kikidhani kwamba alipigwa risasi.
Kimesema pamoja na matukio yote hayo, viongozi wote hao hawakuchukuliwa hatua zozote za kuwajibika kwa matukio hayo.
Pia Chadema kimeonya kuwa hali hiyo ikiachwa inaweza kujenga dhana potofu kwa wananchi kuwa Jeshi la Polisi liko mikononi mwa CCM na kazi yake ni kulinda masilahi ya chama hicho kwa gharama yoyote ile jambo ambalo Mbowe alisema ikiwa Rais Kikwete atachukua hatua za kinidhamu dhidi ya viongozi hao, atakuwa ameudhihirishia umma kwamba Serikali yake haifumbii macho mauaji yanayofanywa na vyombo vya usalama nchini.
Kimemtaka Rais Kikwete kuunda tume ya kijaji au kimahakama kuchunguza vifo vilivyotokea katika mikusanyiko, mikutano, maandamano au mazingira ya kisiasa yanayokihusisha Chadema.
Ikulu yajibu
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alipoulizwa juu ya barua hiyo alisema haijafika ofisini kwake, huku akisisitiza kuwa kama imeandikwa kwa Rais si lazima ifike kwake.
“Sijaiona, ila kama wamemwandikia Rais barua sidhani kama itakuja kwangu. Itakwenda kwake moja kwa moja,” alisema Balozi Sefue.
Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye hakutaka kuzungumzia hatua hiyo ya Chadema akisema, “Siwezi kusema chochote kwa kuwa barua yenyewe sijaiona pia ni barua ya Rais.”
Kauli ya Bavicha
Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), limemtaka Rais Kikwete kuunda tume huru yenye wataalamu wa sheria ili kuchunguza mauaji, utekaji, vurugu na unyanyasaji wa wananchi unaotokea kwenye mikutano ya siasa hasa inayokihusisha chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Morogoro baada ya kikao cha baraza hilo taifa, Mwenyekiti wa Bavicha, John Heche alisema kwamba kama Rais Kikwete atashindwa kufanya hivyo, baraza lake kwa kutambua kuwa matukio mengi ya mauaji yamehusisha vijana, litahamasisha maandamano nchi nzima na kuishtaki Serikali yake.
Habari hii imeandikwa na Fidelis Butahe na George Njogopa, Dar na Hamida Sharif, Morogoro.(MWANANCHI) www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment