Wednesday, December 26, 2012

Maandamano ya wasunni yarindima Iraq

Maandamano mapya dhidi ya waziri mkuu wa Iraq yanafanyika katika miji ambayo zaidi inakaliwa na wasuni na kusababisha barabara kuu ya kuelekea katika nchi za Syria na Jordan kufungwa 

Katika maandamano hayo zimesikika sauti za wanaotaka umma kuchukua silaha dhidi ya serikali iliyoko madarakani. 

Maelfu ya watu wanashiriki maandamano hayo katika miji ya Ramadi na Samarra ambayo ni miji mikuu ya mikoa inayokaliwa na idadi kubwa ya waislamu wa madhehebu ya Sunni katika eneo la kati na Magharibi ya Iraq. 

Waandamanaji wanapinga kile ambacho wanakitaja kuwa ulengwaji wa jamii zao na maafisa pamoja na vikosi vya usalama kutoka katika serikali inayoongozwa na madhehebu ya washia. 

Aidha maandamano hayo yanahudhuriwa pia na waziri wa fedha Rafa al-Essawi ambaye takriban walinzi wake tisa walikamatwa kwa tuhuma za kuhusika na ugaidi mwezi huu. 

Waziri huyo ametoa ahadi ya kumpeleka mwakilishi wa waandamanaji hao kuwasilisha kilio chao katika serikali mjini Baghadad.

Hata hivyo waandamanaji ambao wanasadikiwa kuwa ni maelfu ya watu waliokusanyika Jumatano na kuifunga barabara kuu inayouunganisha mji mkuu wa Iraq Baghadad na Jordan na Syria wamesikika wakipaaza sauti za kutaka mapinduzi nchini humo.Wanasema kwamba hawatakubali mashauriano yoyote na serikali na wataendelea kubakia mitaani hadi pale madai yao yatakaposikilizwa. 

Ali Hatem Suleiman kiongozi wa maandamano hayo ametoa hotuba yake katika maandamano ya mjini Ramadi na kusema kwamba wanachokitaka ni kufutwa kwa sheria ya kupambana na ugaidi ambayo inatajwa kuwalenga tu waislamu wa madhehebu ya Sunni.

Halikadhalika hali kama hiyo ya maandamano imeutikisa mji wa Samarra mji mkuu wa mkoa wa Salaheddin kaskazini mwa Baghadad ambako waandamanaji wamesikika wakitoa kauli za kumtaja Maliki kuwa kiongozi muoga na wakala wa Iran. 

Itakumbukwa kwamba wasiwasi wa mvutano wa kimadhehebu ni suala muhimu katika nchi ya Iraq ambayo imekumbwa na miaka chungunzima ya ghasia za kinyama zilizosababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine wengi kulazimika kuzikimbia nyumba zao. 

Mara zote waarabu kutoka madhehebu ya Sunni wamekuwa wakimuangalia Nuri al Maliki na serikali yake ya umoja wa kitaifa kama ni kibaraka wa nchi jirani ya Iran.Maandamano ya Jumatano yamefuatia mikutano kadhaa ya siku ya Jumapili ambako waandamanaji wakiwemo maafisa kadhaa na viongozi wa kidini na kikabila mjini Ramadi waliifunga barabara hiyo kuu.

No comments: