Sunday, September 23, 2012

Iran yaionya Israel

KAMANDA wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), katika kujibu vitisho vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Iran, amesema kuwa Israel ikiihujumu Iran basi huo utakuwa mwanzo wa kuangamia kwake.

Akizungumza mjini Tehran, Meja Jenerali Mohammad Jafari amesema ‘vita dhidi ya Iran hatimaye vitajiri lakini bado haijabainika vitakuwa lini na wapi.’ Amesisitiza kuwa Iran iko tayari kukabiliana na tishio lolote dhidi yake. 

Kamanda huyo ameongeza kuongeza kuwa Israel ambayo ni ‘donda la saratani’ imeamua kuwa njia pekee ya kukabiliana na Iran ni kuanzisha vita. Aidha amewataja viongozi wa Israel kuwa wajinga sana na kwamba mabwana zao wanapaswa kuwazuia. 

Meja Jenerali Mohammad Jafari amesema Mapinduzi ya Kiislamu yamechukua mkondo wa kasi katika kufikia malengo yake jambo ambalo Wazayuni wameshindwa kulistahamili na kwa hivyo wanataka kuanzisha vita. Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Jeshi la Iran lina uwezo kamili wa kukabiliana na adui. 

Utawala haramu wa Israel umekuwa ukitoa vitisho vya kushambulia kijeshi vituo vya nyuklia vya Iran kabla ya uchaguzi wa rais wa Marekani utakaofanyika Novemba 6. Ikumbukwe kuwa mpango wa nyuklia wa Iran wenye malengo ya amani unafanyika kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

No comments: