Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amemtumia
salamu za rambirambi Rais Mstaafu wa Zambia Mheshimiwa Kenneth Kaunda
kuomboleza kifo cha mkewe, Mama Betty Kaunda (pichani), ambaye alifariki dunia Jumanne wiki hii akiwa na umri wa miaka 84.
“Nimesikitishwa
na kushtushwa sana na taarifa za kifo cha Mama Betty Kaunda
kilichotokea wiki hii mjini Harare, Zimbabwe, ambako alikuwa
anamtembelea binti yake, Mama Musata Kaunda Banda.
Mama Betty Kaunda alikuwa shujaa wa Bara letu na mama wa mfano siyo kwa
wananchi wa Zambia bali kwa Waafrika sote. Kifo chake ni pigo siyo kwako
tu
Mheshimiwa Rais, ama kwa wanafamilia, ama hata kwa wananchi wa Zambia
bali kwa
Waafrika wote”.
Rais
Kikwete amesema katika salamu zake hizo, “Kwa miaka yote alipokuwa mke
wa Rais wa Zambia tokea Oktoba 1964 hadi Novemba 1991, Mama Betty Kaunda
alikuwa nguzo ya
familia na nguzo yako Mheshimiwa Rais katika mapambano ya kuleta uhuru
wa
Zambia na katika harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika. Mchango wake
hautasahauliwa na pengo la kifo chake litabakia nasi kwa miaka mingi”.
“Mzee wangu Mheshimiwa Rais Kaunda nakutumia wewe salamu za dhati ya moyo wangu
kufuatia kifo cha mama yetu na kupitia kwako kwa wanafamilia wote kwa
kuondokewa na mhimili mkubwa wa familia.Naungana nanyi kuomboleza kifo cha mama
yetu na pia naungana nanyi kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aiweke
pema peponi roho ya Marehemu Betty Kaunda. Amen”.
Mama Kaunda ambaye ameacha watoto wanane, wajukuu 30 na vitukuu 11, alizaliwa
Novemba 1928 katika Jimbo la Kaskazini mwa Zambia wakati huo ikiitwa Northern
Rhodesia, akaolewa na Mzee Kaunda mwaka 1946 na karibuni walisherehekea miaka
66 ya ndoa yao mjini Lusaka, Zambia.
Imetolewa
na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
21 Septemba, 2012 |
No comments:
Post a Comment