Brahimi akutana na Assad,aionya dunia
Mjumbe wa kimataifa nchini Syria Lakhdar Brahimi ameonya baada ya kukutana na rais Bashar al-Assad Jumamosi(15.09.2012) kuwa mzozo unaozidi kukua nchini Syria unatishia eneo lote la mashariki ya kati pamoja na dunia.
Urusi , ambayo ni mshirika mkubwa wa Syria, imesisitiza kuwa " haing'ang'anii " kiongozi fulani nchini Syria, lakini imeonya kuwa itazuwia azimio lolote jipya la baraza la usalama la umoja wa mataifa lenye lengo la kumshinikiza Assad, mshirika wa muda mrefu wa Urusi.
"Mzozo huu ni hatari na unazidi kuwa mbaya , na ni kitisho kwa watu wa Syria , eneo zima la mashariki ya kati na dunia, amesema Brahimi aliyeteuliwa hivi karibuni , na kuchukua nafasi kama mjumbe mpya mapema mwezi huu nafasi iliyoachwa wazi na katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa Kofi Annan.
Assad ataka majadiliano
Assad , akinukuliwa na televisheni ya taifa , amesema majadiliano baina ya Wasyria ni muhimu kuweza kuleta suluhisho na kutoa wito kwa mataifa ya kigeni kuacha kuwapatia silaha mahasimu wake.
"Tatizo kubwa nchini Syria ni lile ya kuchanganya siasa na kazi inayofanyika kwa mapambano," amesema. Kazi ya kisiasa inaendelea , hususan kwa kutoa wito wa kufanyika majadiliano kati ya Wasyria yaliyo katika misingi ya matakwa ya Wasyria.
"Mafanikio ya hatua hii ya kisiasa inategemea utoaji wa mbinyo kwa nchi ambazo zinafadhili na kuwapa mafunzo magaidi, na ambazo zinaingiza silaha nchini Syria, hadi pale zitakapositisha hatua hiyo", amesema Assad. Miezi 18 tangu kuanza kwa mzozo huo ambao umekuwa hatari na ambao hauonekani kufikia mwisho, Assad amesema serikali yake itatoa ushirikiano kwa juhudi za kweli za kuutatua mzozo huo, iwapo juhudi hizo haziegemei upande mmoja na ni huru.
Brahimi, mwenye umri wa miaka 78, mtu ambaye ni mkongwe katika masuala ya utatuzi wa mizozo, raia wa Algeria, pia amekutana na waziri wa mambo ya kigeni wa Syria Walid Moallem na viongozi wa upande wa upinzani ambao unavumiliwa rasmi na serikali ya Syria tangu alipowasili mjini Damascus siku ya Alhamis.
Suluhisho litatoka kwa Wasyria wenyewe
"Kuna haja ya pande zote kuunganisha juhudi zao ili kutafuta suluhisho la mzozo huu, kutokana na umuhimu wa Syria katika eneo hili, na ushawishi wa mzozo huu katika eneo lote" , Amesema Brahimi.
"Suluhisho pekee linaweza kupatikana kutoka kwa Wasyria wenyewe".
Amesema kwa sasa , "hana mpango", kuweza kupambana na mzozo huu, lakini mkakati utaundwa baada ya kusikiliza pande zote za ndani, kimkoa na kimataifa.
Brahimi ameonya alipowasili kuwa mzozo huo , unaendelea kuwa mbaya. Yuko katika ziara yake ya kwanza mjini Damascus tangu alipochukua nafasi ya Annan , ambaye amejitoa baada makubaliano ya amani ambayo amekuwa mpatanishi kushindwa.
Brahimi siku ya Ijumaa(14.09.2012) alikutana na viongozi wa makundi ya upinzani nchini Syria ambao wamesema wanaleta mawazo mapya , katika juhudi za kuleta amani . Alikutana na makundi ya upinzani ambayo yanavumiliwa na utawala wa Assad kama vile National Coordination Committee , kamati ya uratibu wa taifa kwa ajili ya mabadiliko ya kidemokrasia, ambayo inajumuisha makundi ya Waarabu wazalendo, Wakurdi na wasoshalisti.
www.dw.de
No comments:
Post a Comment