Monday, October 8, 2012

Ban: Mzozo wa Syria ni hatari

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema hali ya mvutano inayozidi kuongezeka kwenye mpaka baina ya Syria na Uturuki ni hatari kubwa, na kuomba pande zinazohusika kuacha kupeleka silaha kwa serikali na waasi. 

Akizungumza kwenye mkutano wa kimataifa juu ya demokrasia ambao unaendelea mjini Strasbourg Ufaransa, Ban Ki-moon amesema hali nchini Syria imekuwa mbaya kwa kiwango cha kutisha, na kuonya kwamba mgogoro unaoendela nchini humo unatishia kuenea hadi nchi jirani na eneo zima kwa ujumla. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa ameelezea wasi wasi mkubwa alionao kutokana na kuendelea kumiminika kwa silaha nchini humo, na kutoa wito kwa pande zinazohusika kuacha kutoa silaha kwa serikali na waasi.

 Ban ameuambia mkutano huo kwamba mpatanishi wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu kuhusu Syria Lakhdar Brahimi, hivi karibuni atarudi kwenye eneo la mashariki ya kati, kujaribu kuendeleza juhudi za kimataifa kutanzua mgogoro wa Syria.

Mvutano kati ya Uturuki na Syria 

Kauli ya Bwana Ban Ki-moon inakuja siku moja baada ya Uturuki kurusha makombora ndani ya Syria, kujibu mashambulizi yaliyotokea upande wa Syria dhidi ya mji wa mpakani wa Uturuki wa Akcakale. 

Waziri mkuu wa Uturuki Tayyip Erdogan alitetea hatua iliyochukuliwa na nchi yake, akisema walichokifanya ni wajibu wao. ''Unapaswa wakati wowte kuwa tayari kupigana vita kama ni lazima. Kama huwezi, basi wewe siyo taifa. Wahenga walisemaje, kwamba ukitaka amani, kaa tayari kupigana vita.'' Amesema Erdogan. 

Wakati hayo yakiarifiwa, nchini Syria kwenyewe moto unazidi kuwaka. Majeshi ya serikali yamefanya mashambulizi makali dhidi ya ngome za waasi katika mikoa ya Daraa na Homs, na pia katika mji mkubwa kibiashara wa Aleppo. Miungurumo ya silaha kubwa imesikika wakati wa mapambazuko leo hii, na watu takribani 23 wameripotiwa kuuawa katika mashambulizi hayo. 

Serikali yajitutumua 

Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria lenye makao yake nchini Uingereza, limesema kuwa miongoni mwa hao, 20 wameuawa katika mji wa Karak-al-Shariq ulio kusini mwa mkoa wa Daraa, ambao umeshuhudia mapigano makali nyakati za alfajiri. Shirika hilo limesema kuwa waasi watano walikuwa miongoni mwa waliouawa, na kuongezua kuwa idadi kubwa ya vifo imetokana na shambulizi lililofanywa na jeshi la serikali dhidi ya gari iliyokuwa ikiwapeleka majeruhi hospitalini.

Mkurugenzi wa shirika hilo la kuchunguza haki za binadamu, Rami Abdel Rahman amesema kwamba waasi walikuwa wakijaribu kuhimili mashambulizi makali yaliyoanzishwa na serikali siku tatu zilizopita, katika juhudi za kuuchukua mji wa Karak-al-Shariq. Jana, bomu lililotegeshwa ndani ya gari liliripuka kwenye kituo cha polisi katika mji mkuu Damascus, na kumuua afisa mmoja wa polisi, hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la habari la Syria, SANA. 

Waasi wadai kusonga mbele 

Wakati huo huo, waasi wamedai kuyateka maeneo mengine zaidi sehemu ya kaskazini mwa nchi, karibu na mpaka baina ya Syria na Uturuki. Shirika la kuchunguza haki za binadamu nchini Syria limesema kwamba miji mingi iliyo karibu na mpaka huo, sasa inadhibitiwa na waasi. Msemaji wa waasi Abu Omar al Halabi ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwa njia ya simu, kwamba wameweza kuviteka vituo viwili vya ukaguzi mjini Aleppo, kutoka mikononi mwa serikali. Upinzani nchini Syria unasema kwamba watu 31,000 wamekwishauawa nchini humo tangu mgogoro huu ulipoanza miezi 19 iliyopita.

Kutoka DW 

No comments: