Wednesday, October 17, 2012

Kutofahamiana Kati Ya mtoto Na wazazi, Kunasababisha Matatizo Na: Meshack Maganga-Iringa

 Serikali ya Tanzania kupitia Sera ya Elimu ya mwaka 1995, iliruhusu watu binafsi, mashirika na taasisi mbalimbali kuanzisha shule zake. Marekebisho katika sera hii yamewanufaisha wengi mathalani kwa kuongeza ajira, idadi ya shule, nafasi za elimu na kuinua kiwango cha elimu nchini. Pia ushindani katika kutoa elimu umeongezeka na hivyo kuchochea kasi ya ukuaji wa maendeleo kwa ujumla.
 Kwa sasa shule nyingi zinazomilikiwa na watu au mashirika binafsi zinatamba kwa kuwa na miundombinu bora, vyombo vya usafiri, zana muhimu za kufundishia na kujifunzia na pengine walimu wa kutosha wenye sifa zinazostahili. Kwa hakika ni jambo la kujivunia kwa kuwa na shule kama hizi hapa nchini. 

 Katika hali ya ulimwengu wa sasa ambapo wazazi wengi wametingwa sana na majukumu ya kujitafutia kipato ili kuweza kukabiliana na mahitaji na changamoto za maisha ya kila siku, shule za bweni kwa watoto wadogo zimeonekana kuwa mkombozi.

 Hii inatokana na ukwe;li kwamba mara nyingi baba anaweza kutingwa na kazi ofisini au akatakiwa kuwa safarini na wakati huohuo mama naye akawa na majukumu ya kiofisi au kibiashara katika sehemu nyingine mbali na nyumbani. Hili linawafanya wazazi hawa kufikia muafaka, kwamba shule za bweni ni muafaka kwa watoto wao wadogo.

 Katika shule hizo, wazazi wanaamini, watoto watalelewa vema, kwa upendo na zaidi watapatiwa elimu nzuri. Kwa kuyatambua haya, wazazi hawa hugharimia fedha nyingi kuweza kumudu ada inayotakiwa na aghalabu katika shule hizi ni watoto wa watu wenye uwezo wa kipato kikubwa katika jamii wanaoweza kusoma katika shule hizo. Si rahisi kwa wanaojiita walalahoi kumudu gharama hizi japo wengi wangependa watoto wao pia wasome katika shule hizo. Katika kuuangalia mfumo huu kwa juu juu, hasa kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka 12 kuwa katika shule za bweni hapaonekani kama kuna tatizo, lakini kwa upande mwingine lipo tatizo kubwa katika mfumo huu.

 Ni lazima tujue kwamba ukaribu kati ya mzazi na mtoto na hasa mtoto anapokuwa na umri mdogo ni jambo muhimu sana. Kwa kuwatenga watoto kutoka katika familia zao katika umri mdogo na kuwapeleka katika shule za bweni ni kuuingilia ukaribu unaotakiwa kujengwa kati ya wazazi na watoto. Watoto hukua na kuwa watu wazima lakini utu uzima wao huwa umejengewa misingi imara kutokana na yale wanayojifunza utotoni kutoka kwa wazazi wao pamoja na jamii inayowazunguka.

Hakuna shaka kwamba sisi kama wazazi tungependa sana watoto wetu watutambue nasi tuwatambue vema. Tungependa sana tuzifahamu hisia zao nao pia wazitambue hisia zetu. Tungependa watoto watambue kukasirika kwetu na kufurahi kwetu na kwa upande mwingine sisi kama wazazi tuweze kutambua viashiria vya hisia za watoto wetu kwani katika maono yetu ndipo ulipo utu wetu halisi.

 Ili tuweze kufanikiwa katika hili, ni muhimu sisi wazazi kuwa na watoto wetu kwa ukaribu kwa muda wa kutosha hasa hasa katika miaka ya awali ya uhai wao. Mtoto anapomtambua mzazi wake katika maisha ya mwanzo ya uhai wake, uhusiano wa damu ulio kati yao unaimarika.

Wanachukuliana na kupendana kwa upendo usioweza kuelezewa kwa maneno rahisi. Watu hawa wataheshimiana na kuthaminiana katika maisha yao yote. Upendo na uhusiano wa jinsi hii hauwezi kujengwa iwapo mtoto anatengwa na familia yake akiwa na umri wa miaka mine na kupelekwa katika shule za bweni.

Utengano huu unamfanya mzazi asiweze kumfahamu vema mtoto wake na hali kadhalika mtoto asimfahamu vema mzazi wake. Matokeo yake mzazi na mtoto wanakuwa ni mtu na mgeni kwa mwenzake, kila mmoja anamhofia mwenzake.

 Tujaribu kujiuliza iwapo mtoto ataanza kusoma shule ya bweni akiwa na umri wa miaka minne katika shule ya awali, katika umri wa miaka sita akaendelea na shule ya msingi ya bweni na katika umri wa miaka 13 akaendelea na shule ya sekondari ya bweni, vivyo hivyo mwanafunzi huyu ataendelea na safari yake ya kutafuta elimu mpaka afikie chuo kikuu. Matokeo yake kijana huyu ambaye ni mtu mzima sasa, atabaki kuwa mgeni kwa wazazi wake.

Hii ni kwa sababu amejengewa msingi madhubuti wa kutowafahamu kwa undani wazazi wake. Siyo kwamba walimu na wafanyakazi wengine wanaowalea watoto hawa wadogo katika shule za bweni, wanashindwa kuwafundisha, la hasha! Tatizo linatokana na ukweli kwamba, uhusiano kati ya mzazi na mtoto si jambo linaloweza kufundishwa kwa nadharia katika vyumba vya madarasa.

 Hivi sasa kuna wahitimu wa vyuo vikuu,'wadada', 'wamama' wazima wanaotoka vyuo vikuu ambao hata kupika uji tu ama chakula hawafahamu kabisa,au kutokana na ka-elimu alikokapata na akajua kuongea sentensi tatu za kigereza anajisahau,pengine yote hii ni malezi. Niliyoongelea hapo juu. Ni sharti watu hawa, mzazi na mtoto, waishi pamoja kwa muda wa kutosha ndipo watakapoweza kufahamiana. Muda wa likizo anaoupata mtoto ni mfupi mno kuweza kutosheleza zoezi hili.

 Kujuana tabia na zaidi mtoto kuiga baadhi ya mambo kutoka kwa wazazi wake ni jambo linalohitaji muda wa kutosha na na pengine mtoto huweza kuiga na kufanya yale wazazi wake wanayopenda ayafanye bila yeye kujitambua. Kwa vyovyote vile, umuhimu wa mtoto mdogo kukaa na wazazi wake kwa muda wa kutosha utabaki palepale.

 Kusomeshwa katika shule za bweni mtoto akaweza kuzungumza lugha ya Kiingereza kwa ufasaha na kuyamudu masomo kwa kiwango kikubwa,anachokitaka mzazi, si vitu pekee vinavyomjenga mwanadamu. Kuna hatari kubwa ya kuwa na wasomi wengi siku za usoni ambao wametawaliwa na vitabu na elimu ya darasani iwapo tutaliacha ombwe hili bila kulitafutia ufumbuzi. Na iwapo mkataa kwao ni mtumwa, basi hueenda tukawa tunaendelea kutengeneza watumwa wengi zaidi kupitia shule za bweni kwa watoto wadogo.

Mwandishi Mwingereza wa riwaya za kusisimua katika karne iliyopita, Renĕ Raymond, maarufu kwa jina lake la kiuandishi kama James Hadley Chase, aliwahi kuandika katika riwaya aliyoiita The Whiff of Money, kisa cha kusisimua ambapo mtoto aliyelelewa shuleni alijenga chuki dhidi ya wazazi wake.

 Katika kisa hicho, mgombea urais nchini Marekani aliyekuwa na matumaini makubwa ya kuukwaa urais wa nchi hiyo, harakati zake ziliiingia dosari katika hatua za mwisho baada ya binti yake aliyekuwa amempeleka katika shule za bweni nchini Uswisi tangu akiwa mdogo, kuamua kucheza picha za utupu na kuwapatia filamu hiyo wapinzani wakubwa wa baba yake ili waweze kumchafua baba yake na kumzuia kuingia ikulu.

Chase, kwa kutumia mhusika asiyeshindwa katika riwaya zake nyingi, Mark Girland, anaonyesha kwamba binti huyo anaponaswa nchini Ujerumani na kuulizwa sababu ya kucheza picha hizo za aibu, binti huyo anaeleza kwamba amefanya hivyo ili kuwakomoa wazazi wake ambao siku zote hawakuonyesha mapenzi kwake zaidi ya kumtelekeza katika shule za kifahari huku wao wakiyapa kipaumbele mambo ya kisiasa.

Ni kisa cha kubuni lakini bado kinabeba ukweli kwamba kutofahamiana kwa undani kati ya mtoto na wazazi, kunasababisha matatizo makubwa ndani ya familia na jamii.

Ni dhahiri kwamba wazazi hawa wangelikuwa wamekaa na binti yao kwa muda wa kutosha hasa akiwa mdogo, mtoto huyu angeliweza kuitambua mapema ndoto ya wazazi wake ya kwenda ikulu na bila shaka angelikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha kwamba wazazi wake wanatimiza azima yao. Vilevile wazazi nao wangeliweza kuzitambua hisia za binti yao mapema na kuzielekeza katika njia sahihi. Kupata watoto, kwa walio wengi ni jambo la baraka na ni jambo la kujivunia.

 Kwa walio wengi pia, suala la kuanzisha familia hupangiliwa na wala si jambo linalotokea kwa bahati mbaya. Hivyo basi, kwetu sisi tulio wazazi ama walezi ni lazima tubebe wajibu wa kuwalea na kuwaelekeza watoto wetu katika njia sahihi. Mbali ya kukabiliwa na majukumu ya kimaisha, ni lazima tutenge muda wa kutosha wa kukaa na watoto wetu wadogo. Kuwaaachia watu wengine majukumu ya kutufanyia kila kitu juu ya watoto wetu ni kukwepa jukumu letu la msingi kwa kiasi fulani. Ukimfahamu mtoto wako kwa undani utakuwa na nafasi nzuri ya kujua namna ya kumsaidia anapoendelea kukua kuelekea utu uzima.

Lakini hatutaweza kufanikiwa katika hili tusipotenga muda wa kutosha tukaweza kufahamiana hasa katika utu wetu wa ndani.

Yapo majukumu tutakayosaidiwa na walimu, waganga, walezi na jamii kwa ujumla katika makuzi ya watoto wetu, lakini pia bado lipo jukumu kubwa ambalo litabaki kuwa wajibu wa mzazi nalo ni kustawisha uhusiano wa damu uliopo baina yetu kwa kuendelea kufahamiana zaidi na zaidi.
                                                              meshackmaganga@gmail.com

No comments: