Wednesday, October 17, 2012

Sheikh Ponda Akamatwa

S.H. KOVA – DCP KAMANDA WA POLISI KANDA MAALUMU YA POLISI DAR ES SALAAM AKIZUNGUMZA NA WAANDISHI WA HABARI KATIKA KITUO KIKUU CHA POLISI KATI LEO
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam limemtia mbaroni Katibu wa Jumuiya tajwa hapo juu maarufu kama PONDA ISSA PONDA kwa makosa mbali mbali ya kuchochea vurugu na uvunjaji wa amani jijini Dar es Salaam.

Aidha hivi karibuni Sheikh Ponda Issa Ponda aliongoza kundi la wafuasi wake na kuvamia kiwanja No. 311/3/4 BLOCK “T” eneo la Chang’ombe katika Manispaa ya Temeke mali ya Kampuni ya AGRITANZA ambayo ipo chini ya Kurugenzi ya Kampuni hiyo. Mnamo tarehe 12/10/2012 Ponda Issa Ponda aliwaongoza wafuasi wake walioteka eneo hilo wakidai kwamba wanakomboa mali za Waislamu, zilizouzwa na BAKWATA, uchunguzi wa awali umeonyesha kwamba kiwanja hicho kina hati miliki No. 93773 uliotolewa na Wizara ya Ardhi pamoja na mikataba mbali mbali ya kuuziana au kubadilishana kati ya BAKWATA na Kampuni tajwa hapo juu. 

Pia uongozi wa BAKWATA umeleta mashahidi kuthibitisha uhalali wa kiwanja hicho kumilikiwa na Kampuni tajwa. Hivyo watu wote waliovamia eneo hilo wakiongozwa na Sheikh Ponda wanakabiliwa na shtaka la kuingia kwa jinai pamoja na uharibifu wa mali katika eneo hilo. Sambamba na kukamatwa kwa Sheikh Ponda tarehe 16/10/2012 saa 4.00 usiku karibu na eneo la maficho yake ambapo aliletwa na pikipiki.

WATU 38 WAMEKAMATWA KWA KOSA LA KUINGIA KWA JINAI NA UHARIBIFU
Wakati huo huo sambamba na kukamatwa kwa Sheikh Ponda Issa Ponda, Polisi walifanya operesheni maalumu ya kuwaondoa wavamizi katika kiwanja tajwa hapo juu kinachomilikiwa na Kampuni AGRITANZA. Watu wapatao 38 walikutwa katika eneo la kiwanja hicho ambacho kati ya hao (7) ni wanawake na 31 ni wanaume.

Operesheni hiyo ilifanyika tarehe 17/10/2012 usiku wa manane kuanzia saa tisa hadi saa kumi na nusu usiku kwa muda wa dakika 90. Katika eneo hilo vilikutwa vielelezo mbali mbali vikiwemo visu na mapanga na pia nyenzo mbali mbali za ujenzi, pamoja na vifaa vya ujenzi, vielelezo hivyo vimehifadhiwa katika kituo cha Polisi tayari kwa ajili ya ushahidi mahakamani. 

SHEIKH PONDA KUSABABISHA VURUGU NA VITISHO
Katika siku za hivi karibuni Sheikh Ponda Issa Ponda amekuwa akiwaongoza wafuasi wake chini ya Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania kwa kufanya maandamano kinyume cha Taratibu na kuhamasisha umwagaji damu jijini Dar es Salaam na nchini Tanzania kwa ujumla. Kwa ujumla Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania inayoongozwa na Sheikh Ponda haijasajiliwa kisheria, lakini wanatuhumiwa kwa uchochezi wa hali ya juu ambapo licha ya kufanya maadamano kinyume na sheria pia siku ya tarehe 12/10/2012 walisababisha kuvunja kwa makanisa zaidi ya manane, uharibifu wa magari na wizi au upotevu wa vifaa katika makanisa, yote hayo yameongozwa na Sheikh Ponda na madhara yake ni makubwa. 

Sheikh Ponda amekuwa mstari wa mbele kupambana na vyombo vya dola pamoja na kuingilia uhuru wa Mahakama kwa kudai watuhumuwa waliokamatwa kwa uvunjaji wa makanisa na kufikishwa mahakamani waachiwe mara moja kabla siku saba na kadhalika. Uchunguzi wa watuhumiwa wote 39 unaendelea na kufikishwa mahakamani mara baada ya kupitishwa na wakili wa Serikali kuthibitisha mashitaka. 
S.H. KOVA – DCP 
KAMANDA WA POLISI 
KANDA MAALUMU YA POLISI DAR ES SALAAM

No comments: