Friday, November 2, 2012

Israeli yakiri kumuua kiongozi wa PLO

Kwa mara ya kwanza Israeli imekiri kumuua aliyekuwa kiongozi namba mbili wa chama cha ukombozi cha Wapalestina-PLO, Abu Jihad katika shambulio lililofanywa katika makao makuu ya chama hicho mjini Tunis mwaka 1988.

Taarifa iliyochapishwa na gazeti la Israeli la Yediot Aharonot , imeeleza kuwa operesheni hiyo ilipangwa na shirika la ujasusi la Israeli, Mossad na iliendeshwa na kikosi cha makomandoo cha Sayeret Matkal. Abu Jihad ambaye jina lake halisi ni Khalil al-Wazir aliuawa kwa kupigwa risasi Aprili 16, mwaka 1988 katika shambulio lililofanywa kwenye makao makuu ya PLO. Gazeti hilo limesema taarifa hizo zimechapishwa baada ya miezi sita ya mazungumzo kati ya gazeti hilo na maafisa wenye mamlaka wa jeshi la Israeli.

Rais wa Palestina Mahmud Abbas (Shoto) na Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu Operesheni hiyo iliamriwa na Nahum Lev, ambaye katika mahojiano kabla ya kifo chake mwaka 2000, alikiri kuhusika kwake katika operesheni hiyo, ingawa taarifa hiyo haikuchapishwa. Katika mahojiano hayo, Lev alisema alisoma kila ukurasa kuhusu mashtaka dhidi ya Abu Jihad na kwamba kiongozi huyo namba mbili wa chama cha ukombozi cha Wapalestina-PLO, alihusishwa na vitendo vya kikatili na kutisha dhidi ya raia na alipaswa kuuawa. Lev anasema alimuua kwa kumpiga risasi Abu Jihad bila kusita.

Jihad rafiki wa muda mrefu wa Arafat 

Abu Jihad, aliyekuwa rafiki wa muda mrefu na msaidizi wa kiongozi wa zamani wa PLO, Yasser Arafat, alishiriki kikamilifu katika kuongoza vuguvugu la maandamano ya upinzani- Intifada mwaka 1987 hadi 1994 dhidi ya makaazi ya Israeli. Mahmud al-Alul, aliyekuwa msaidizi wa naibu kiongozi wa PLO, ambaye kwa sasa ni afisa wa juu wa chama cha Fatah cha Rais Mahmud Abbas wa Palestina, amesema kwao ilikuwa rahisi kuhisi Israeli ndio ilihusika na mauaji ya Abu Jihad. Ameliambia shirika la habari la AFP, kuwa kiongozi huyo hakuuawa na mwanajeshi, lakini na uamuzi uliofikiwa na serikali ya Israeli na uongozi wake wa kijeshi.

Kiongozi wa zamani wa PLO, Yasser Arafat Alul anasema wakati mauaji hayo yanafanyika Yitzhak Shamir, alikuwa Waziri Mkuu na Yitzhak Rabin akiwa waziri wa ulinzi, ambaye baadae alikuwa waziri mkuu hadi alipouawa na wapiganaji wa mrengo wa kulia mwaka 1995. Ehud Barak, waziri wa ulinzi wa sasa, alikuwa ni naibu mkuu wa jeshi na Moshe Yaalon ambaye kwa sasa ni waziri wa masuala ya kimkakati, wakati huo alikuwa kamanda wa kikosi cha Sayeret Matkal. Alul anasema wanajua wazi kwamba viongozi hao ndio walihusika na mauaji hayo.

Makomandoo waliingia Tunis siku moja kabla ya mauaji 

Taarifa hizo zinaonyesha kuwa makomandoo 26 wa Sayeret Matkal waliwasili kwenye ufukwe wa Tunis jioni ya Aprili 15, mwaka 1988 na kugawanyika katika makundi mawili na kusafirishwa hadi karibu na makaazi ya Abu Jihad. Makomandoo hao waliwaua pia mlinzi wa pili wa Abu Jihad na mtunza bustani wake na Lev anasema anasikitika kumuua mfanyakazi huyo wa bustani, lakini katika operesheni kama hizo ni lazima uhakikishe wapinzani wote wanaangamizwa.

No comments: