Sunday, November 25, 2012

Lowassa, Kinana washambulia Arusha

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa jana waliongoza mashambulizi dhidi ya Chadema na wakisema kuwa lazima Jimbo la Arusha Mjini walirejeshe mikononi mwao. 

Pia, viongozi hao wamewapokea waliokuwa madiwani watano Chadema wakavuliwa uanachama na sasa wamejiunga na chama hicho. Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jana kuutambulisha uongozi mpya wa chama hicho, Lowassa alisema kuwa kama uchaguzi wa Jimbo la Arusha Mjini utarudiwa CCM itapata ushindi wa kishindo. 

“ Nashangaa kwa nini Chadema bado iko Arusha. Ninachoweza kusema, tusubiri Mahakama ya Rufaa itakavyoamua, kama uchaguzi utarudiwa tutalikomboa jimbo hili,” alisema Lowassa huku akishangiliwa na wananchi na kuongeza: “Nawaelewa kwa nini mnanishangilia.” Kwa upande wake, Kinana alitaka wanachama wa chama hicho kuachana na makundi ambayo yanaendelea kukiathiri chama hicho.

Alisema katika miaka ya hivi karibuni CCM ilikuwa imepoteza mwelekeo, hali iliyowafanya Watanzania kukata tamaa na viongozi wao na wengine wakaamua kujiunga na vyama vya upinzani. Kinana ambaye aliwahi kuwa Spika wa Bunge la Afrika Mashariki alisema kuwa hatua ya viongozi wa chama na Serikali kujisahau iliwafanya wananchi wakose mtu wa kumlilia. “Leo (jana) mmenipa faraja kweli. 

Maeneo mengi nilipokewa na hata mikutano yangu kuhudhuriwa na umati mkubwa watu, lakini leo Arusha mmenipa nguvu ya ajabu kwa umati huu. “Hakika, kwa umati huu ninapenda kujiona kuwa Rais Jakaya Kikwete hakukosea uteuzi wake kwangu. Nitafanya kazi kwa moyo wa kujituma zaidi. Hakuna kati yetu asiyejua katika siku za hivi karibuni chama chetu kilipoteza mwelekeo na hata kuonekana ni watu wa ajabu kwa wanachama na wananchi kwa ujumla. Aliwaonya viongozi wa CCM ambao watashindwa kuwajibika kumaliza matatizo ya wananchi, basi wajipime kabla hatua hazijachukuliwa dhidi yao.“CCM inahitaji kuwa na viongozi ambao wapo tayari kushuka chini na siyo kufunga vioo vya gari, kwa sababu eti wewe ni ‘mheshimiwa.’ Hili sitalikubali ndani ya chama chetu,” alisema Kinana.

Mamia wampokea Kinana 
Awali msafara wa magari ukiongozwa na mamia ya pikipiki zilizokuwa katika mapokezi ya Kinana na viongozi wengine, ulisababisha baadhi ya shughuli kusimama kutokana na msongamano barabarani. Kinana aliyewasili katika Uwanja wa Ndege wa Arusha saa 4.00 asubuhi alipokewa na viongozi wa chama na Serikali akiwamo Lowassa. 

Baada ya kuwasili, Kinana alikumbatiana na Lowassa ikiwa ni ishara ya furaha na upendo baina yao. Wakati msafara huo ukielekea katika Wilaya ya Arumeru, ukiongozwa na pikipiki zilizopambwa na bendera za CCM, vijana wanaodaiwa kuwa ni wa Chadema walikuwa katika vikundi barabarani wakionyesha vidole viwili ambayo ni alama ya chama chao. 

Kinana alifungua matawi kadhaa na kuzungumza na wananchi na kurudia maneno yake ya kuwataka viongozi wa CCM kutokaa ofisini, bali wanatakiwa kwenda kwa wanachama katika ngazi za chini. 

Madiwani wa Chadema warejea CCM 
Katika mkutano huo, madiwani wa Chadema walitangaza kujiunga na CCM huku wakipinga hatua ya Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Willibrod Slaa kuwa alikuwa akitaka kuwafunga baada ya kuwatimua ndani ya chama hicho. 

Madiwani hao ambao walitimuliwa na Chadema kutokana na kitendo chao cha kumtambua Meya wa Jiji la Arusha Gaudence Lyimo wa CCM ni Rehema Mohamed, Simba Salum wa Kata ya Kati na Frank Joseph Takachi wa Kata ya Olasiti. 

Akizungumza katika mkutano huo, aliyekuwa Diwani wa Viti Maalumu wa Chadema, Rehema Mohamed alisema uamuzi wake wa kupinga kufanya kazi na Lema kutokana na misimamo yake ilikuwa ni moja ya sababu ya kumfanya afukuzwe uanachama. 

“Nililala ndani kwa mwezi mmoja kwa kuipigania Chadema lakini kumbe hakuna kitu, ila leo hii shukurani yao ni kutaka kutufunga kwa kutufungulia kesi ya uongo. Kwa hali hiyo nitaendelea kulia na kumwomba Mungu kama njia ya kunifungua katika kongwa la majuto.

Lema apita mitaa ya mkutano 
Wakati mkutano huo ukiendelea, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alikatiza katika maeneo ya uwanja huo huku gari lake likisukumwa na wapambe wake wa Chadema. Gari hilo lilikuwa likisukumwa na wapambe wake ambao walikuwa wamebeba bendera za Chadema, huku wakipiga kelele za kumshangilia na kuwabeza CCM.

Mawaziri
Mkutano huo ulihudhuriwa na mawaziri watano wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano na Uratibu), Stephen Wassira ambaye alisema kuwa katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Lema Jimbo la Arusha Mjini lilipoteza biashara ya watalii na uchumi wake kuyumba. 

Alisema ili kutoa fursa zaidi kwa wakazi wake ni lazima kila mwananchi atambue wajibu wake katika kuilinda na kuipigania Arusha kama mlango wa biashara ya utalii nchini. Kwa upande wake Waziri wa Biashara na Viwanda, Dk Abdallah Kigoda alisema Kiwanda cha General Tyre cha jijini Arusha kitafunguliwa Desemba mwaka 2013 na kutoa ajira kwa vijana wengi wa Mkoa wa Arusha. 

Naye Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema mipango ya Serikali ni hadi kufikia mwaka 2014 asilimia 30 ya Watanzania watakuwa wameunganishwa katika umeme wa gridi ya taifa. “ Ndiyo maana tumepunguza bei ya kuunganisha umeme lengo ni kutaka kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata nishati hiyo kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla. 

Mwananchi

No comments: