Sunday, December 16, 2012

Dk. Slaa awahenyesha CCM

MKAKATI wa kumchafua Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa, unaoratibiwa na baadhi ya viongozi waliotimuliwa kwenye Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), umedaiwa kufadhiliwa na CCM, Tanzania Daima Jumapili limebaini. 

Vijana hao ambao wamedaka kauli ya uzushi ya Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC) Taifa wa CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, kuwa Dk. Slaa anamiliki kadi ya chama hicho na anaendelea kuilipia, wanazunguka mikoani wakimchafua kiongozi huyo wakidai ajiuzulu. 

Licha ya vijana hao kufukuzwa uongozi na wengine kuvuliwa uanachama, lakini bado wameendelea kufanya mikutano na waandishi wa habari wakijipachika nyadhifa za BAVICHA, wakidai kuwa wanaandaa maandamano ya kumng’oa Dk. Slaa. 

Hata hivyo, Tanzania Daima Jumapili limefahamishwa kuwa, mkakati wa vijana hao tayari umefichuliwa na CHADEMA na kubainika kuandaliwa na CCM ili kuendeleza hoja hiyo ya Nape ya kumchafua Dk. Slaa.

Chanzo chetu cha ndani kinaeleza kuwa, kasi ya Dk. Slaa kwa sasa inawatia kiwewe CCM, hivyo chama hicho kupitia kwa Nape kimelazimika kuwatumia mamluki hao kikidhani kinaweza kufifisha nguvu ya CHADEMA mikoani. 

Tayari Dk. Slaa amefafanua hoja ya Nape akieleza kuwa kadi ya CCM ameendelea kubaki nayo kama mali yake na kumbukumbu kwa wajukuu zake, huku akikanusha madai ya kuilipia akisema ni jambo lisilowezekana kisheria. 

Pia mwanasheria maarufu jijini Arusha, Method Kimomogoro, naye alijitokeza kutoa ufafanuzi wa kisheria, akisema kuwa kadi ya chama ni mali ya mwanachama, hivyo ana hiari ya kuirejesha akihama au kubaki nayo.

Kimomogoro aliongeza kuwa, wanaohama na kusalimisha kadi zao, wanafanya hivyo kwa mapenzi yao na kutaka kuonekana, lakini hakuna mahala wanakotakiwa kufanya hivyo kisheria. 

Wakati wasomi mbalimbali wakijitokeza kuipinga hoja ya Nape, kada huyo aliibuka na kujikanyaga kwenye mtandao wa kijamii, akidai kuwa hakumlenga moja kwa moja Dk. Slaa, bali baadhi ya viongozi wa upinzani akiwemo yeye, wanaendelea kumiliki kadi za CCM.

Kwa kile kinachoonekana kuwa propaganda hiyo iliibuliwa makusudi kwa ajili ya kumdhoofisha Dk. Slaa, inadaiwa kuwa CCM imefanya mazungumzo na kuwawezesha kifedha baadhi ya vijana waliofukuzwa BAVICHA ili wabebe ajenda hiyo na kuieneza mikoani, ionekane kuna mgogoro ndani ya CHADEMA.

Tayari vigogo wa juu wa CHADEMA wamethibitisha kuudaka mkakati huo wa CCM ulioasisiwa na Nape na kueleza kuwa, unaratibiwa kwa kutumia fedha za mafisadi.

“Hao wanafanya kazi ya Nape wakidhani wataisaidia CCM…ila kwa kuwasaidia tu kama hawana taarifa kuhusu Dk. Slaa, waje makao makuu tutawaelimisha kuliko uongo huo wanaoufanya,” alisema mmoja wa viongozi wa CHADEMA. 

Naye kada wa chama hicho, Arcado Ntagazwa aliyewahi kuongoza wizara mbalimbali ikiwemo Idara ya Usalama wa Taifa katika utawala wa awamu zilizopita, alisema CCM kamwe hawawezi kufanikiwa kwa ajenda hiyo.

“Unajua tena wenzetu wana fedha za mafisadi, hivyo kutokana na vijana wetu kukosa ajira, wameamua kuwarubuni na kuwazungusha mikoani ili kumpaka matope Dk. Slaa,” alisema. 

Ntagazwa alisema kuwa wala CHADEMA hawahitaji kupoteza muda kuzunguka kukanusha uongo huo wa CCM, na badala yake wawapuuze tu kwa vile hawawezi kumsambaratisha Dk. Slaa. 

Wiki iliyopita, Ntagazwa alizungumza na gazeti hili akisema CCM inababaishwa na nyota ya Dk. Slaa, hivyo viongozi wake na serikali wamejikuta wakibabaika na kufanya vitendo vya ajabu wakidhani wataweza kumzuia. 

Ntagazwa alieleza kushangazwa na kiwewe wanachokipata viongozi wa serikali na CCM kwa Dk. Slaa, ambaye alidai nyota yake inazidi kung’ara kwa wananchi licha ya juhudi kubwa ya kujaribu kumchafua.

“CCM wanamwona Dk. Slaa ni tishio kwao, hivyo katika kubabaisha watu wanadhani watapunguza imani kwake, wameibua mambo ya ajabu na kupoteza muda kama alivyofanya Nape kudai kuwa hajarudisha kadi ya CCM,” alisema.

Alisema kuwa kwa sasa CCM wanashindwa kutambua kwamba mambo yamebadilika, Watanzania wanachuja na kuchambua mambo si kama ilivyokuwa zamani. 

“Hili jambo la kupotoka na kushindwa kusimamia misingi na kuwatetea wanyonge, ndilo Dk. Slaa pia amekuwa akilikemea kwa baadhi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA, ambao wamegeuka kucheza ngoma ya mafisadi wa CCM,” alisema. 

Ntagazwa kwa kujiamini alisema kuwa, katiba za TANU na CCM ziliandikwa vizuri na kuwekwa mambo ya msingi, lakini akasikitika na kuhoji ni pepo gani amewaingilia viongozi wa CCM sasa na kushindwa kusimamia mambo hayo. 

“Wanachokifanya CCM sasa ni tofauti kabisa, yaani sawa na ardhi na mbingu. Wanafanya mambo ya ajabu kwa wananchi na hadi kufikia kuibua mambo ya ajabu kama alivyofanya kijana wao (Nape),” alisema.

Aliongeza kuwa, kwa sasa wanamshukuru Mungu kwani wananchi wanajionea jinsi CCM ilivyoshindwa kurejesha misingi, na badala yake imehamia kushirikiana na serikali kufanya vitendo vya hovyo kwa kutumia polisi na vyombo vingine vya dola.

Mpaka sasa wamejitokeza vijana wawili walioenguliwa ndani ya BAVICHA na kufanya mikutano na waandishi wa habari, wakijipachika vyeo vya ukatibu wa mikoa wa baraza hilo na kudai wataongoza maandamano ya kumng’oa Dk. Slaa.

Vijana hao ni Edo Mwamalala wa Mbeya ambaye hata hivyo CHADEMA mkoani humo ilithibitisha kuwa ilikwishamtimua uanachama, huku Salvatory Magafu naye akiibuka juzi mkoani Mwanza akijitambulisha kama Katibu wa Mkoa BAVICHA wakati uongozi wao ulivunjwa muda mrefu. 

Katika harakati hizo za kueneza propaganda hiyo ya kuonesha kuna mgogoro ndani ya CHADEMA, inadaiwa kuwa baadhi ya vyombo vya habari vimepenyezewa fungu kuhakikisha vinaandika habari za kukisambaratisha chama hicho.

BAVICHA Mwanza wanena 
Mwenyekiti BAVICHA Mkoa wa Mwanza, Liberatus Mulebele, amelazimika kutoa ufafanuzi na kuweka kumbukumbu sawa kutokana na habari zilizosambazwa kuhusu upotoshaji wa Magafu.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, mwenyekiti huyo alisema habari zilizoripotiwa kuwa BAVICHA Mwanza wanataka Dk. Slaa aondoke madarakani na vinginevyo watamng’oa si za kweli.

“Napenda kutumia nafasi hii kusema maneno machache juu ya upuuzi huo ambao kila mtu anajua umetokana, na unaratibiwa na kusimamiwa na CCM, ikiwa eti ndiyo moja ya mikakati ya sekretarieti ya chama hicho inayoitwa kuwa ni mpya,” alisema.

Alisema kwa nafasi yake kama msemaji mkuu wa BAVICHA mkoani Mwanza, vijana hawajawahi, wala hawana mpango wa kubeba propaganda za CCM dhidi ya CHADEMA na viongozi wake kuanzia ngazi ya chini hadi ya juu, akiwemo Dk. Slaa. 

“Vijana CHADEMA Mwanza tuko imara kukilinda chama chetu na viongozi wetu dhidi ya propaganda za CCM na serikali, ambazo zina lengo la kudhoofisha harakati za kujenga taasisi imara inayobeba matumaini ya Watanzania kwa ajili ya ukombozi wa awamu ya pili,” aliongeza.

Mulebele alifafanua kuwa, wanatambua kuwa katiba za vyama vya siasa, ikiwemo ya CCM, zinasema wazi kuwa mwanachama wa chama hicho akijiunga na chama kingine, anapoteza uanachama wake kwa chama hicho cha awali.

“Lakini pia vijana wa CHADEMA Mwanza ambao ni makini kama ilivyo kawaida, tunaelewa wazi na tunaweza kusimamia kauli hii, kuwa Dk. Slaa tangu alipohama CCM mwaka 1995 hajawahi, kwa maana ya kila mwaka, kwenda ofisi yoyote ya CCM kulipia kadi yake,” alisema.

Aliongeza kuwa, BAVICHA Mwanza haijafanya uamuzi wa kuendesha harakati zozote za kutaka Dk. Slaa ajiuzulu, wala haitambui maandalizi ya maandamano kwani ni batili na aliyetoa tamko hilo, Salvatory Magafu si msemaji wa vijana wa CHADEMA Mkoa.
www.freemedia.co.tz 

No comments: