Saturday, December 29, 2012

Lissu asema Profesa Shivji amepotoka kuponda kesi ya Lema

HATUA ya mwanazuoni wa siku nyingi nchini, Profesa Issa Shivji kupinga hukumu ya Mahakama ya Rufani Tanzania iliyomrejeshea ubunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema imemtia matatani na baadhi ya watu wanasema gwiji huyo wa sheria “huenda amenukuliwa vibaya au hajasoma hukumu husika.”

Jana Wakili wa Lema, Tundu Lissu, alimkosoa Profesa Shivji pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Francis Stolla akisema wanasheria hao wamepotoka katika matamshi yao ya kupinga hukumu ya Mahakama ya Rufani.

Matamshi ya Shivji pia yaliiteka mijadala katika mitandao ya kijamii ya Jamii Forums, Mabadiliko na Facebook ambako wachangiaji walikuwa wakivutana huku baadhi yao wakisema wazi kwamba msomi huyo amekosea huku wengine wakimtetea kwamba yuko sahihi. 

Akizungumza na gazeti hili jana kutoka Songea mkoani Ruvuma, Lissu alipinga vikali hoja zilizotolewa na Profesa Shivji pamoja na Stolla, akisema kuwa hazina mashiko na zinaweza kutolewa tu na mtu ambaye hakufuatilia mwenendo wa kesi hiyo. 

Juzi Profesa Shivji na Stolla walinukuliwa wakiikosoa hukumu ya Mahakama ya Rufani, iliyomrejesha bungeni Lema wakisema hukumu hiyo iliyotolewa na majaji watatu Salum Massati, Bernard Luanda na kiongozi wao Nathalia Kimaro, inapingana na sheria. 

Lissu katika maelezo yake alisema uamuzi wa mahakama katika kesi ya Lema umejenga upya msingi bora wa matumizi ya vyombo vya uamuzi, kwani kesi nyingi za kupinga matokeo ya ubunge, zimekuwa zikifunguliwa na watu ambao wamekuwa wakitumwa na vigogo wa kisiasa na watu wenye fedha.

Akizungumza na Mwananchi, Lissu alisema hoja hizo hazina mashiko na kuwa ile iliyotolewa na Profesa Shivji inatokana na msomi huyo kuzungumza kitaalamu bila kuangalia mazingira halisi ya siasa za Kitanzania.

Lissu alisema mahakama ya rufani haikupiga marufuku wapiga kura kufungua kesi za kupinga ila iliwataka tu kufanya hivyo pale haki zao zinapokiukwa. 

“Kwanza siyo kweli kwamba mahakama imepiga marufuku wapiga kura kufungua kesi, ilisema watafanya hivyo pale ambapo haki zao zimevunjwa, haki zenyewe ni kupiga kura, kura zao kutohesabiwa ama suala jingine litakalomnyima kupiga kura, hizo ndiyo haki za mpiga kura,” alisema na kuongeza: 

“Sasa mwalimu wangu, Profesa Shivji yeye anatazama tu kwa jicho la kitaalamu na kusema haki za binadamu zimekiukwa, kwa muda wanasiasa, matajiri na CCM wamekuwa wakiwatumia wananchi kuwapinga wabunge wa upinzani.”

Uchambuzi wa Lissu
Alitoa mfano akisema katika uchaguzi wa 1995, Dk Willibrod Slaa alishinda ubunge na watu wanaojiita wananchi walifungua kesi kupinga ushindi huo, mwaka 2000 wakampinga tena na hata 2005.

Alisema 1995 Makongoro Nyerere aliposhinda ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini kupitia NCCR- Mageuzi, watu wanaojiita wananchi walifungua kesi ambayo matokeo yake yalikuwa mbunge huyo kupoteza kiti chake. 

Lissu alisema 2005 aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Marehemu Chacha Wangwe alifunguliwa kesi na watu waliojiita wananchi ambao mwisho wake walishindwa. 

www.mwanachi.co.tz

No comments: