Wednesday, December 26, 2012

Reli ndefu kabisa duniani ya treni ya kasi yazinduliwa rasmi China

Reli ndefu kabisa duniani ya treni ya kasi leo imezinduliwa rasmi. Reli hiyo yenye umbali wa kilomita 2298 inaunganisha mji mkuu Beijing na Guangzhou, mji muhimu wa biashara kusini mwa China inafupisha muda wa usafari hadi saa 7 na dakika 59 kutoka zaidi ya saa 20 na nusu.

Saa 3 leo asubuhi treni ya kwanza ya kasi iliondoka Beijing, kaskazini mwa China, katika safari ya kilomita 2298, inapita miji zaidi ya 20 mikubwa kutoka kaskazini hadi kusini mwa China, na kufika mwisho wa reli hiyo, mji wa Guangzhou. Katika safari ya majaribio iliyofanyika jumamosi iliyopita, treni iliendeshwa kwa kasi ya wastani ya kilomita 300 kwa saa. 

Bei ya tiketi ni kutoka Yuan 865, dola 140 za kimarekani hadi Yuan 2727, sawa na dola 450 za kimarekani. Si bei rahisi, lakini kutokana na kasi yake, hali ya juu ya usalama ya safari za treni, na kivutio cha teknolojia za hali ya juu za treni ya kasi, tiketi za treni zote za leo zimeuzwa kabisa. Ofisa wa kituo cha reli cha Beijing alisema treni ya kwanza ina viti 1051, tiketi zote ziliuzwa na abiria wengi wanakwenda Guangzhou kutalii au kuwatembelea jamaa zao.

Bibi Li ni abiria wa treni hiyo ya kwanza. "Hii ni reli ndefu kabisa ya treni ya kasi nchini China na duniani. Nafurahi sana nimeweza kununua tiketi ya treni yake ya kwanza. Nasikia salama zaidi kusafiri kwa treni kuliko ndege. Bei yake ni kubwa kweli, lakini nasikia salama."

Wizara ya reli ya China imechukua hatua kadhaa za kuhakikisha usalama wa safari, zikiwemo kuimarisha shughuli ya marekebisho ya vifaa vya kudumu na vifaa vya mikononi ndani ya treni , na kuboresha mfumo wa udhibiti ili kushughulikia matatizo yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa. 

Wachina watasherehekea mwaka mpya wa jadi mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka 2013. Katika kipindi cha sikukuu hiyo muhimu zaidi kuliko nyingine katika jamii ya wachina, mamilioni ya watu watasafiri nchini China, na safari za treni ni njia kuu ya mawasiliano. Uzinduzi wa reli hiyo ya treni ya kasi inatarajiwa kupunguza msongamano wakati wa sikukuu hiyo.

Mbali na kuongeza uwezo wa uchukuzi wa reli nchini China, reli hiyo ya treni ya kasi pia inayopita maeneo kadhaa muhimu ya kiuchumi inatarajiwa kuchangia mambo ya uchumi na biashara. Imefahamika kuwa hadi mwaka 2015 reli hiyo itarefushwa hadi Hong Kong.

No comments: