Sunday, January 6, 2013

Assad apinga mazungumzo na "vibaraka"

Rais Bashar al-Assad wa Syria amefuta uwezekano wa mazungumzo na makundi ya upinzani ambayo ameyaita kuwa "vibaraka" wa mataifa ya magharibi na ameapa kupambana na "magaidi" na "magenge ya wahuni." 

Al-Assad amesema katika hotuba yake ya kwanza kwa umma baada ya zaidi ya miezi saba ameueleza umma kwamba hao ni maadui wa wananchi, maadui wa Mungu na kwamba hatimaye wameamuwa kufanya ugaidi kwa kuwatisha wananchi. Ameongeza kusema kwamba wanayaita hayo mapinduzi lakini wanachokifanya hakihusiani kabisa na mapinduzi kwani mapinduzi yanahitaji watu wenye fikra wakati watu hao ni kundi tu la wahalifu. Wafuasi wake waliokuwa kwenye ukumbi wa jengo la michezo ya kuigiza mjini Damascus walimkatiza mara kwa mara kwa kumshangilia kwa mayowe "Kwa roho na damu yetu tutakulinda Assad".

Taifa latakiwa kujiandaa kwa vita
Al-Assad amesema waasi wanaoungwa mkono na mataifa ya kigeni wanaendesha vita nje ya nchi hiyo dhidi ya Syria. Akisisitiza madai ya serikali yake kwamba magaidi wa kigeni wanahusika na mzozo wa miaka miwili wa nchi hiyo amesema kwamba kilicho yakini ni kwamba wale wanaopambana nao hivi leo ni wale wenye kufuata itikadi ya Al Qaeda. Al-Assad ametowa wito kwa kujiandaa kwa taifa kuihami nchi hiyo kwa kile alichokiita kuwa "hali ya vita kwa maana halisi ya neno lenyewe."

Amezishukuru Urusi, China na Iran ambazo ni washirika wake wakuu kwa kuwaunga mkono wakati huu wa mzozo ambao ulianza kwa uasi wa kudai demokrasia hapo mwezi wa Machi mwaka 2011 na baadae kugeuka kuwa mzozo wenye kuhusisha matumizi ya silaha. Al-Assad pia alitaja mpango wa kumaliza mzozo huo ambao umetupiliwa mbali na wapinzani kwamba unakusudia kuvuruga juhudi za kidiplomasia. Kwa mujibu wa al-Assad mpango huo unajumuisha mkutano wa upatanishi wa kitaifa, serikali itakayokuwa na uwakilishi mpana, chaguzi za bunge na katiba mpya. Hata hivyo ametowa masharti ya kuanza kwa utekelezaji wa mpango huo kwa kusitishwa msaada wa kigeni kwa waasi. Assad amesema " Tutakuwa tu na mzungumzo na mabwana (wa maamuzi yao) na sio watumwa (wa mataifa ya kigeni)." 

Kun'gatuka kwa Assad bado kwasisitizwa 
Makundi ya upinzani wameyakataa madai hayo ya al-Assad na kusisitiza kwamba ufumbuzi wa kisiasa kwa mzozo huo hauwezi kufikiwa bila ya kujiuzulu kwa kiongozi huyo. Rami Abdel Rahman mkuu wa Shirika la Kuangalia Hali ya Haki za Binaadamu nchini Syria amesema hakuna nafasi ya kufikia suluhisho nchini Syria wakati serikali hiyo ikiwa madarakani. Amesema hotuba hiyo ya Assad ni marudio tu na kwamba yeye na washauri wake wanaishi wakiwa mbali kabisa na uhalisia wa mambo.

Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton amesema kuwa Rais Bashar al-Assad ni lazima aachie madaraka ili kurejesha hali ya utulivu na amani nchini Syria.Ashton amesema kuwa wataichambua kwa makini hotuba ya Assad kuona kama kuna kitu kipya lakini msimamo wao unabaki palepale kwamba Assad inabidi an'gatuke na kuruhusu mchakato wa kuanzisha kipindi cha kisiasa cha mpito.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza William Hague ameandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba hotuba ya Rais Assad "imepindukia unafiki " na ahadi zake tupu hazitamghilibu mtu yeyote. Umoja wa Mataifa umesema kwamba idadi ya vifo nchini Syria imefikia 60,000 tokea kuanza kwa mzozo huo miezi 22 iliopita.

No comments: