Sunday, February 10, 2013

Taarifa ya Polisi kuhusu Mwanamke aliyafariki JNIA akiwa na dawa za kulevya

Mwanamke aliyefahamika kwa jina la Margaret Temu (45) amekufa ghafla baada ya kudhuriwa na pipi 64 za dawa za kulevya alizomeza ili kuzisafirisha kwenda Osaka, nchini Japan akiwa na mwenzake.

Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Deusdedit Kato alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tukio hilo. 

Kamanda Kato alisema tukio hilo lilitokana na kukamatwa kwa watu wawili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) wakiwa katika harakati za kusafirisha nje ya nchi dawa ambazo wanahisi kuwa ni za kulevya katika tukio lililotokea Jumatano ya wiki hii. 

Kamanda Kato alisema Margaret akiwa na mwenzake Allen Habibu Ally (28) mkazi wa Tegeta jijini Dar es Salaam walikamatwa na askari wa kike wa Kikosi cha Viwanja vya Ndege nchini (ambaye hakumtaja) baada ya kuwatilia mashaka. 

Kwa mujibu wa Kamanda Kato askari huyo alimtilia shaka Ally na ndipo alimfuata na kuzungumza naye ambapo baada ya mtuhumiwa kubaini kuwa alikuwa ni askari alimshawishi apokee dola za Marekani 3,000 ili amwachie aendelee na safari yake ya Osaka, Japan.

Alisema askari huyo wa kike (ambaye jina lake limehifadhiwa kutokana na taratibu za kazi zake) alikataa ushawishi huo na kuamua kuwakamata Ally na Margret baada ya kubaini kuwa mienendo yao kiwanjani hapo ilionekana kuwa wanafahamiana na wako katika safari moja. 

Baada ya kukamatwa Margret na Ally, Polisi waliwahoji na Ally alikiri kumeza pipi 75 za dawa hizo ambazo zinadhaniwa kuwa ni za kulevya lakini Margret alikataa katakata kumeza chochote lakini ghafla wakati mahojiano yakiendelea mtuhumiwa huyo alianza kutokwa na damu puani na povu mdomoni na wakati huo huo Ally pia alianza kutokwa na povu 

Alisema kitendo hicho kiliwafanya polisi kuwakimbiza Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu lakini Margret alifariki kabla ya kufika hospitali wakati Ally alisalimika baada ya kupatiwa matibabu. 

Baada ya mwili wa Maragret kufanyiwa uchunguzi na upasuaji mbele ya ndugu zake ambao polisi iliwapata kwa msaada wa maelezo yake yaliyokuwa kwenye hati yake ya kusafiri alikutwa amemeza pipi 64.

Alisema kwa upande wake Ally, mara baada ya hali yake kutengemaa siku iliyofuata alirudishwa Polisi ambako alitoa pipi 69 kwa njia ya haja kubwa ambazo polisi wanadhani ndizo alizomeza. Alisema pipi hizo zimepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kubaini ni aina gani ya dawa za kulevya. 

Aidha kutokana na kufanikisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao na dawa hizo pamoja kugoma kushawishika kuchukua hongo na kuonesha uadilifu na uaminifu katika kazi yake, Kamanda Kato alisema Jeshi la Polisi limemzawadia askari huyo Shilingi milioni 5 ambazo ni sawa na kiasi cha dola za Marekani 3,000 ambazo aliikuwa anahongwa na watuhumiwa aliowakamata.

Kwa mujibu wa Kamanda Kato, kuwazawadia askari wa aina hiyo ni sera ya Jeshi la Polisi nchini ambayo inaelekeza kutoa kiasi hicho cha fedha kwa askari endapo inathibitika kweli alitaka kuhongwa na kuwataka askari wengine waige mfano bora ulioneshwa na mwenzao.

No comments: