Sunday, February 17, 2013

Wazazi Kigoma wawacharaza walimu

Walimu watatu wa Shule ya Msingi Misingeni katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wamejeruhiwa sehemu mbalimbali za miili yao kufuatia kushambuliwa na kundi la wazazi wenye watoto kwenye shule hiyo.

Akizungumza na mwandishi, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Hilda Msita alisema wazazi hao walivamia shule kupinga kitendo cha Mwalimu wa shule hiyo, Mathias Banzi kuwaadhibu watoto wao kwa kuwachapa viboko kutokana na utovu wa nidhamu. Mwalimu Msita alisema baada ya kutokea vitendo hivyo vya utovu wa nidhamu kwa watoto hao, Mwalimu Banzi aliwachapa viboko wanafunzi hao na ndipo mwanafunzi mmoja (Fadhili Mlibo) alikimbia na kwenda kutoa taarifa kwa wazazi wake kuhusu jambo hilo.

Alisema kuwa baada ya kufika nyumbani na kutoa taarifa kwa wazazi wake, Mama wa mwanafunzi huyo, Amina Rashidi aliwaeleza wazazi wengine wenye watoto shuleni hapo na ndipo kundi la wazazi zaidi ya 20 walivamia shule wakiwa na silaha za jadi na kuwajeruhi walimu.

Mwalimu Mkuu wa shule huyo, Hilda Msita aliwataja walimu waliojeruhiwa kwenye sakata hilo kuwa ni pamoja na Mathias Banzi, Barnabas Matalisi na Sikujua Bunoge, ambao baada ya kipigo cha wazazi hao walitibiwa katika hospitali ya mkoa Kigoma Maweni na kuruhusiwa. 

Kwa upande wake Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Mohammed Kihenya amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kwamba polisi inamshikilia Amina Rashidi mzazi wa mmoja wa watoto walioadhibiwa katika sakata hilo. Kamanda Kihenya alisema kuwa pamoja na kumshikilia mzazi huyo kwa kufanya vurugu mahala pa kazi na kujeruhi, pia inawatafuta watu wengine ambao walihusika katika vurugu hizo.

No comments: