Wednesday, March 13, 2013

KESI YA UAMSHO: DPP hana mamlaka ya kumnyima mtu dhamana mahakamani

Kushoto ni Amir wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Sheikh Farid Hadi Ahmed, katikati ni Amir wa Jumuiya ya Uamsho Sheikh Msellem Ali Msellem na kulia ni Naibu Amir wa Uamsho Sheikh Azzan Khalid Hamdan ambao wote wameshitakiwa kwa makosa mbali mbali na dhamana yao kuzuiwa na DPP

KESI ya viongozi wakuu wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (JUMIKI) imeingia hatua mpya baada ya Mahakama Kuu jana kufuta maamuzi yote ya Mrajis wa Mahakama hiyo.

Viongozi hao wanakabiliwa na kesi ya madai ya uchochezi na kuhatarisha usalama wa taifa la Zanzibar. “Maamuzi ya Mrajis yote yanafutwa kwani hayakuwa sahihi kwa vile Mrajis hana mamlaka ya kisheria ya kupokea, kusikiliza na kutoa uamuzi kuhusu kesi iliyofunguliwa Mahakama Kuu,” alisema Jaji Abraham Mwampashi aliyesikiliza suala hilo jana katika Mahakama Kuu Vuga mjini hapa.

Moja ya mambo makuu yaliyofutwa ni zuio la dhamana ambalo Mrajis alilikubali kama lilivyokuwa limetolewa na Mkurugenzi wa Mashitaka Zanzibar (DPP). 

Jaji Mwampashi alitolea maamuzi baada ya pande mbili katika kesi hiyo za upande wa serikali na utetezi kubishana juu ya uwezo wa Mrajis katika kutoa maamuzi ya dhmana kwa washitakiwa hao. Mawakili wa utetezi walidai kuwa Mrajis hana mamlaka hayo na upande wa waendesha mshitaka walidai kwamba anao uwezo huo.

Jaji Mwampashi alisema DPP anao uwezo wa kuizuia Polisi tu kumpa dhamana mtuhumiwa, lakini sio Mahakama kama ilivyotokea katika suala hili. Jaji Mwampashi alisema DPP alitakiwa aeleze sababu za washitakiwa kutopewa dhamana na ni athari zipi za usalama wa taifa zitatokea iwapo watakuwa nje. 

Alisema kama sheria ingekuwa hivyo kungekuwa hakuna haja ya kuwepo kwa Mahakama kama mtu mmoja anakuwa na haki hiyo na kusingeifanya Mahakama kuwa kimbilio la wanaoona wanapoteza haki zao. Jaji Mwamapashe alisema hawezi kufuta kibali cha DPP cha kufunga dhamana kwa sababu hakupewa nafasi ya kuja mahakamani kutetea hoja yake. 

Aliwaelekeza washitakiwa kuwasilisha upya ombi la dhamana ambalo litasikilizwa baada ya kesi yao ya msingi kupangiwa Jaji wa kuisikiliza. Alisema Mrajis kisheria ana uwezo wa kusikiliza kesi za madai zinapokuwa katika hatua ya awali ya kutajwa, lakini akashangzwa na hatua kwamba Mrajis aliambiwa kwa mdomo na Jaji Mkuu kusikiliza kesi hiyo. 

Washitakiwa hao ni Masheikh Farid Hadi Ahmed, Mselem Ali Mselem, Mussa Juma Issa, , Hassan Bakari Suleiman, Gharib Ahmada Omar, Abdalla Said Ali na Fikirini Majaliwa Fikirini, Azzan Khalid Hamdan, Suleiman Juma Suleiman, Khamis Ali Suleiman. 

Washitakiwa hao wako rumande tangu kesi yao ilipofikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Oktoba 25, mwaka jana. Wamerudishwa rumande wakisubiri kesi yao kupangiwa Jaji wa kuisikiliza na kujilikana itaanza kusikilizwa lini.

Kutoka Gazeti la Tanzania Daima

No comments: