Friday, April 26, 2013

TAKUKURU haijapewa ‘meno ya kuwatafuta mafisadi papa’ - Dk HOSEA

  Mkurugenzi wa Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa nchini (TAKUKURU) Dkt. Edward Hosea amewataka watanzania kutoilaumu Taasisi yake katika kushughulikia rushwa ambavyo mara kadhaa zimetajwa kuwahusisha vigogo wa Serikali na wenye uwezo.

Akizungumza katika semina ya kuwaelimsha viongozi wa dini iliyofanyika jana mjini Moshi mkoani Kilimanjaro Dkt Hosea amesema Watanzania wamekuwa wakitupia na kuinyooshea kidole cha lawama taasisi yake kwa kushindwa kufuatilia kwa kina wale wanaoitwa “mafisadi papa” nchini. 

Dkt. Hosea amesema Watanzania wanasema kwa kuwa vigogo wanaotajwa na rushwa nchini wapo katika Serikali ambayo ina mamlaka na TAKUKURU, hivyo taasisi hiyo imekuwa ikiwapendelea vigogo watuhumiwa. 

Pia amesema Watanzania walio wengi ni wavivu wa kusoma sheria mbalimbali ambazo wakati mwingine zimeeleza majukumu na uwajibikaji wa taasisi husika. 

Hata hivyo, Mkurugenzi huyo amesema sio kwamba TAKUKURU imeshindwa kufuatilia nyendo za wabadhirifu wa mali za umma ipasavyo hususani wale wanaotajwa kama “Mafisadi papa” isipokuwa taasisi anayoiongoza imewekewa mipaka ya ufanyaji kazi wake. 

Aidha, amesema mara zote amekuwa akiitaka Serikali kufanyia marekebisho ya baadhi ya sheria za kuzuia na kupambana na rushwa kutokana na ukweli kwamba TAKUKURU haijapewa meno ya kuwashughulikia wabadhilifu wakubwa. 

Dkt Hosea amesema sheria zilizopo zinamtaka ashughulikie na matendo ya kati na ya chini na sio ya juu kama ambavyo wengi wanafikiri na kuongeza kuwa haina sababu ya kuilaumu TAKUKURU kwa kushindwa kuwakamata wala rushwa wakubwa. 

Semina hiyo iliwakusanya viongozi wa dini wa Kaskazini-Mashariki kwa malengo ya kuendelza juhudi za kuielimisha jamii kuhusu masuala ya rushwa na athari zake kwa jamii. 

 Source: http://www.wavuti.com

No comments: