Sunday, May 12, 2013

Dk. Hoseah: Mimi ni mpambanaji


Dk. Hoseah alitoa kauli hiyo mwanzoni mwa wiki hii alipokuwa akizungumza katika kipindi cha ‘Dakika 45’ kinachorushwa hewani na kituo cha Televisheni cha ITV alipoulizwa kuwa haoni kauli yake aliyoitoa hivi karibuni wakati akizungumza na wakuu wa madhehebu ya dini kuwa rushwa ni janga la kitaifa inaonyesha kuwa ameshindwa kazi. 

“La hasha, siwezi kusalimu amri kwa sababu mimi ni mpiganaji nawe unafahamu. Nilisema rushwa ni janga la kitaifa kwa kwa sababu kubwa tatu; kwanza haibishaniwi kuwa rushwa bado ni kero, kero kwa wananchi wa kawaida, kero kwa maana ya taifa, kero kwa maana bado ni tatizo na hivyo kuna haja kabisa ya kuongeza bidii zaidi kuliko bidii zilizopo ili kuifanya rushwa iweze kushughulikiwa ipasavyo,” alisema Dk. Hoseah. 

Alisema pia kumekuwepo na majanga mengine nchini, akatolea mfano janga la ukimwi na kwamba taifa limeweka msisitizo mkubwa kwenye kampeni, uwezeshwaji na wananchi kushirikishwa na kuamka hivyo kwa mantiki hiyo alidhani katika mtazamo wake kwamba rushwa ikifanywa kwa mrengo wa namna hiyo (janga la kitaifa) anafikiri itapungua kwa kiasi kikubwa kuliko ikaachiwa TAKUKURU peke yake kana kwamba ni tatizo lake pekee. 

“Janga la taifa ni kama mnavyoona ukimwi, kila mtu sasa ashiriki, kila mtu aogope kutoa rushwa, tatu; ili kutatua tatizo ambalo ni janga lazima wananchi na jamii washirikishwe na ndiyo maana utatambua kuwa nilizungumza haya wakati naongea na wakuu wa madhehebu ya dini na wamenielewa sana na hasa nilipotamka kuwa ni janga la taifa,” alisema Dk. Hoseah. 

Alieleza kuwa viongozi hao wa dini wamekubali kuchukua sehemu yao ya kuhakikisha kwamba wanawahubiri waumini wao kwamba rushwa ni dhambi na namna gani ya kuachana kabisa na rushwa.

Pamoja na mambo mengine, alisema Tanzania ni nchi na Mwenyezi Mungu ameibariki hivyo Watanzania wanapaswa kutambua hiyo kwamba nchi yao ni kubwa yenye misitu, hali ya hewa nzuri, maziwa makubwa hivyo wasijisahau wakaliacha tatizo la rushwa likatawala maisha yao yote.

No comments: