Friday, May 3, 2013

Huu ni Ujasiri wa kijinga


Tarehe 23 mwezi aprili mwaka huu majira ya saa mbili usiku nilipokea ujumbe wa maandishi katika simu yangu kutoka kwa jamaa yangu mmoja akinishtua niangalie habari katika chaneli ya ITV. Wakati huo mimi nilikuwa naangalia katika chaneli nyingine. Bahati mbaya sikuweza kukiona kipande cha habari hiyo.

Hamadi!! Nilifanikiwa kuiona habari hiyo, ingawa nilichokiona sikuamini macho yangu. Nilidhani naota. Siku ya pili yake ilinibidi niingie katika youtube ili kuthibitisha kile nilichokiona kama ni kweli au zilikuwa ni ndoto.

Habari niliyoiona iliniumiza sana kana kwamba ni mimi ndiyo nilitendewa kitendo kile. Nilishuhudia kijana mmoja anayeonekana kuwa na akili timamu kabisa akimkunja askari wa usalama barabarani aliyekuwa akitimiza wajibu wake na kumnyang’anya ufunguo wa gari.

Kitendo kilichofanywa na kijana Yule ambaye sijui nimuite kwa sifa ipi ili imfae ni cha udhalilishaji wa hali ya juu kwa binadamu na kwa jeshi la polisi kwa ujumla wake. Nilitafakari na sikupata jibu. Ni nani asiyejua umuhimu na unyeti wa jeshi la polisi katika uhai wa jamii yoyote ile. Ni nani anayeweza kushabikia pindi anapoona jeshi la polisi linagaragazwa?

Katika siku za hivi karibuni vitendo vya kuwadhalilisha polisi na jeshi la polisi vimekuwa vikiongezeka sana. Miaka michache iliyopita, mfanyakazi katika ubalozi wa nchi moja ya Ulaya alifikia hatua ya kumtemea mate askari wa usalama wa barabarani kwa kuwa tu askari huyo alimsimamisha baada ya raia huyo wa kigeni kwenda kinyume na sheria zinazoongoza matumizi ya barabara. Si hayo tu, bali pia mwaka 2010 tulishuhudia mgombea mmoja wa ubunge akimkata mtama mkuu wa polisi wa wilaya moja katika moja za wilaya hapa nchini.

Ni vigumu sana kupita mwezi mmoja kama hujasikia askari wa polisi ameshambuliwa na watu wakati akitimiza wajibu wake. Wapo wanaouawa na mbaya zaidi wananchi wanathubutu hata kuvamia vituo vya polisi na kuvichoma moto. 

Tumeshuhudia kuchomwa moto kwa kituo cha Hedaru ambapo mali na nyaraka za serikali ziliteketezwa, lakini pia tumeshuhudia mauaji ya askari wakiwa wanatekeleza kazi zao. Wananchi pia walimuua askari mkoani Tabora mwaka 2011 wakati akiwa katika operesheni ya kuteketeza mashamba ya Bangi. 

Huwa najiuliza, je ujasiri huu wa raia katika kuwadhalilisha polisi, unatoka wapi? Inakuwaje kila anayesaka umaarufu mbele ya watu basi hakuna pa kuupatia zaidi ya polisi? Ukienda katika mikutano ya wanasiasa, ni vigumu kukuta mkutano umemalizika bila kuwatupia madongo polisi. Wasanii hasa wa vichekesho (comedians) huwa hawaamini kama kazi yao imekamilika kama hawataweka kejeli kwa jeshi la polisi.

Udhalilishaji huu kwa sasa unachupa mipaka hadi sasa vibaka nao, wanadhani wanaweza kuwachezea polisi.
Tunaweza kutafakari kwa pamoja. Kama inatokea mtu mwenye akili timamu anaweza kumdhalilisha askari mwenye sare kwa kumkunja mchana kweupe mbele ya kadamnasi, atashindwa vipi kumpiga na hata kumchania sare au kumnyang’anya silaha pale atakapokutana nae vichochoroni?

Lakini pia, tunaweza kujiuliza! Kama anaweza kumkunja polisi namna ile, je ikitokea amekasirishwa na raia mwenzake atampa adhabu gani?

Cha ajabu ni kuwa, watu hawa wanaolidhalilisha jeshi la polisi, wanashindwa kufahamu kuwa ujasiri wote walionao unatokana na kazi nzuri inayofanywa na jeshi la polisi katika kuhakikisha kunakuwepo na amani na usalama katika nchi yetu.

Watu hawa wanadhani vitendo wanavyovifanya kwa askari wetu labda vitawajengea woga katika kutimiza majukumu yao. Wanasahau kuwa hizo ni changamoto katika kazi na kwamba vitendo hivyo ndo vinajenga na kuamsha ari ya askari katika kupambana na uhalifu wa aina yoyote katika jamii yetu.

Wanasahau kuwa kama usalama usingekuwepo, inawezekana hata huo muda wanaoutumia katika kuwadhalilisha askari na jeshi zima la polisi wasingeupata.

Baadhi yetu wananchi hatuelewi dhana ya polisi jamii na pia dhana nzima ya Utii wa sheria bila Shuruti. Tunadhani, Utii wa Sheria bila Shuruti kunatokana na polisi kushindwa kutumia maguvu. Uhuru tunaopewa na jeshi la polisi tunautafsiri kama uoga na kushindwa kutimiza majukumu kwa jeshi hilo. 

Tunasahau kuwa lengo la utii wa sheria za nchi bila shuruti ni kupunguza uhalifu na matumizi ya shuruti katika usimamizi ya utiifu wa sheria za nchi. Lakini pia utaratibu huu pia unasaidia kupunguza gharama katika oparesheni za kupambana na uhalifu.

Watu hawa wanapendelea jeshi la polisi linalotumia maguvu kama polisi wa kikoloni, ambapo polisi na raia walikuwa na mahusiano ya kiuadui. Raia alipokuwa akimuona polisi hata kama hana kosa, alikuwa akitimua mbio.

Askari naye ni binadamu. Anatakiwa apewe haki zake zote na heshima yake kama binaadamu. Kumdhalilisha askari ni kuidhalilisha serikali.

Binafsi nimekuwa nikifuatilia sana ripoti za kituo cha Sheria na haki za binaadamu (LHRC). Katika taarifa zake za haki za binaadamu, sijawahi kukuta mahali walipoelezea ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu unaofanywa na wananchi wakora kwa askari wetu. Swali za kujiuliza ni hili! Je, hawaoni ukiukwaji wa haki dhidi ya polisi? Au wanaona lakini wanafumbia macho ili polisi wachukue hatua katika kujihami na wao wapate cha kusema?

Wanaharakati ambao ninaamini kwa sauti waliyonayo wanaweza kukemea utovu wa nidhamu unaofanywa na raia dhidi ya askari. Watumie nafasi waliyonayo katika jamii katika kuhakikisha kuwa wananchi, wanaheshimu sheria kwa kuwaacha askari na watumishi wengine wafanye kazi zao walizokabidhiwa na umma.

Nimalizie makala haya kwa kuwaomba askari wasifadhaike kwa matukio yanayofanywa na raia wachache wasiothamini kazi nzuri ya polisi. Raia wema tupo nyuma yenu na tunathamini na kutambua kazi zenu.

Endeleeni katika kuilinda nchi yetu. Zidisheni mapambano dhidi ya wahalifu popote pale walipo bila woga wala huruma. Pia niwapongeze askari wetu kwa uvumilivu mkubwa walionao, hii ni ishara kuwa wamefunzwa na wameiva. Na kwamba wapo tayari kukabiliana na changamoto yoyote inayojitokeza kwao kwa sura yoyote ile.

No comments: