Sunday, June 2, 2013

Sheikh Ponda ahutubia Kongamano la Waislam Dar es Salaam

Imamu wa Msikiti wa Mtambani Imam Suleiman akimkaribisha Sheikh Ponda kuhutubia Waislam kwenye Kongamano hilo.
WAISLAM leo wametoa msimamo juu ya masuala mbalimbali yanayoendelea nchini wakati wa kongamano lililoandaliwa na jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania jijini Dar es Salaam. 

Kwenye kongamano hilo ambalo masheikh mbalimbali wakiwemo Sheikh Ponda Issa Ponda, Ally Basaleh, Mussa Kundecha na Kondo Juma Bungo waliwasilisha mada mbalimbali pamoja na kutangaza maazimio ya kongamano hilo. 

Moja ya mambo yaliyozungumzwa ni mapendekezo waliyowasilisha kwenye Tume ya katiba mpya ambapo walisema iwapo mapendekezo waliyowasilishwa hayakuzingatiwa na kutupwa yote basi waislamu watatangaza kusimamisha mchakato huo nchi nzima na kufanya maandamano usiku na mchana. 

Hoja hiyo ilikuja baada ya kunukuliwa kauli ya Waziri wa nchi Sera na Uratibu wa bunge Wiliam Lukuvi, wakati akijibu swali la Mbunge Asumta Mshama aliyetaka kujua kwamba lini serikali itaacha kupanga siku ya kupiga kura kuwa Jumapili wakati wanajua siku hiyo ni siku ya ibada ya Wakristo haioni inawadhulumu haki yao yakufanya ibada?

Lukuvi kwenye jibu lake alisema suala hilo limekuwa likilalamikiwa na watu wengi tu lakini serikali kwenye hilo haina utaratibu maalum wa siku ya kupiga kura ila kwakuwa kuna mchakato wa katiba mpya hilo litazingatiwa.

“Hii ni kinyume kabisa na utaratibu wa tume ya katiba. 

Waziri huyu anataka tuamini kwamba anayafahamu yatakayokuwemo kwenye Katiba Mpya kabla hata wananchi hawajapelekewa na hata haijaandikwa? 

Hivyo iweje Waisilamu wanaodai siku ya Ijumaa iwe ya mapumziko kwa miaka nenda rudi hawapewi, Wakristo wanakosa siku moja tu ndani ya miaka mitano majibu yanapatikana kirahisi?” Alihoji Sheikh Ponda.

“Waisilamu wamekuwa wakiomba ruhusa kwa mabosi wao siku ya Ijumaa kwenda kufanya ibada na mara nyingine wananyimwa ruhusa hiyo, lakini hakuna vurugu yoyote waliofanya. 

Wanadai haki hiyo kwa miaka yote hii hawapewi, lakini wengine wanadai kirahisi na kujibiwa kwa uhakika.” Alifafanua Ponda. 

Aidha Sheikh Ponda alisema kuwa Waislamu wavumilie wasubiri rasimu itakapotangazwa kwenye magazeti ya serikali kama mapendekezo waliyowasilishwa yatapuuzwa, basi hakutakuwepo na Katiba Mpya maandamano usiku na mchana nchi nzima mpaka kieleweke. Sheikh Ally Basaleh alisihi Serikali kuwasikiliza Waisilamu hoja zao na wasiwapuuze.

 Source: http://www.wavuti.com

No comments: