Sunday, October 28, 2012

KUELEKEA 2015: Kambi ya Lowassa ngoma mdundo


Hofu ya mpasuko mkubwa yanukia CCM

Matokeo ya chaguzi za ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), yameibua taswira isiyotarajiwa kutokana na kundi linalomuunga mkono Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, kupata ushindi mnono.

Tayari CCM inaaminika kuwa katika wakati mgumu kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, ambapo ‘safu’ iliyoshinda maeneo tofauti ya uongozi na vikao vikubwa vya chama hicho, wapo upande wa Lowassa.

Lowassa ambaye mwaka 2005 alikuwa mmoja wa wasaidizi wa karibu wa Rais Kikwete, alipowania urais kwa mara ya kwanza, anasadikiwa kukigawa chama hicho hasa baada ya kuibuka kwa kashfa mbalimbali za rushwa na matumizi mabaya ya madaraka. 

Lakini kashfa kubwa zaidi ni ile iliyohusu mkataba wenye utata wa kuzalisha umeme, uliosainiwa kati ya serikali ya kampuni ya Richmond, ambao hata hivyo ulikuwa chanzo cha kujiuzulu kwake (Lowassa).

Chanzo cha habari cha kuaminika kutoka ndani ya mtandao unaoegemea upande wa Lowassa, kimeliambia NIPASHE Jumapili kuwa, hadi kufikia mwishoni mwa wa wiki, walikuwa wamemiliki asilimia 65 ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec). 

Takwimu hizo zinajumuisha matokeo ya uchaguzi wa jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UV-CCM) ambapo kwa mujibu wa chanzo hicho cha kuaminika, ni watu watatu pekee walioshinda, ambao hawamuungi mkono Lowassa.

“Huyu jamaa (Lowassa) anaenda vizuri na inavyoonekana hakuna namna ya kumzuia katika urais 2015,” kilieleza chanzo hicho ambacho hata hivyo, kinasisitiza kuhifadhiwa kwa jina lake.

Matokeo ya chaguzi hizo yamelalamikiwa sehemu kubwa ya nchi, kwamba ulitawaliwa na vitendo vya rushwa, lakini Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alikana na kusema hali ni shwari na kwamba kashfa hizo zinakuzwa na vyombo vya habari. 

HOFU YA MPASUKO YATANDA 

Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa zinaeleza kuwa hofu ya mpasuko mkubwa kukikumba chama hicho umetanda, hasa ikiwa kundi linaloonekana kumuunga mkono Lowassa, litafanikiwa kumpitisha mgombea urais wake kwa mwaka 2015.

Awali, ilielezwa kuwa chaguzi za ndani ya CCM zilisubiriwa kuwa kipimo cha kukubalika ama kukataliwa kwa Lowassa, ili kupata mkakati wa namna ya kumpata mgombea urais anayestahili. 

Vyanzo tofauti vieleza kuwa wapo wajumbe ndani yake, waliotaka Lowassa asiwanie urais 2015, kwa kigezo kwamba jina lake lilishachafuka, hivyo itatumika nguvu kubwa kumnadi ndani na nje ya chama.

Watetezi wa hoja hiyo wanaeleza kuwa, kutokana na hilo, yapo majina yaliyopendekezwa ili mmojawao apitishwe na kuungwa mkono na wengine, akiwemo Lowassa.

Mmoja wa waliotajwa kufaa kwa ajili ya uteuzi ni aliyekuwa Waziri katika wizara moja muhimu, lakini akaenguliwa katika sakata lililotokana na shinikizo la wabunge. 

Waziri huyo ambaye hadi sasa anaaminika kuwa mfuasi wa Lowassa, ni miongoni mwa mawaziri sita waliofukuzwa kazi na Rais Kikwete, kwa njia ya kutoteuliwa. 

Tukio hilo lilitokana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi MKuu wa Serikali za Mitaa, Ludovick Utouh na ile ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Mazingira na Maliasili inayoongozwa na Mbunge wa Kahama, James Lembeli.

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema, ikiwa Lowassa atasimamishwa kuwania urais mwaka 2015 kupitia CCM, kuna kila dalili za viongozi na wanachama kukihama katika hali ya kutisha.

Wanaotajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuondoka CCM ikiwa Lowassa atapitishwa kuwania urais ni wazee waandamizi waliowahi kushika nafasi kubwa za uongozi ndani ya chama na serikalini. 

“Unajua kwa hali ilivyo, si rahisi watu kama (anawataja majina) kuwa ndani ya CCM na serikali yake inayoongozwa na Lowassa, kwa hiyo msione ajabu watu msiowatarajia wakakihama chama,” kinaeleza chanzo chetu.

KIKWETE NJIA PANDA 

Kwa upande mwingine, Rais Kikwete anatajwa kuwa ‘njia panda’ kutokana na mabadiliko ya siasa ndani ya CCM, hasa pale rushwa na hujuma vinapotajwa kutawala.

Kauli aliyoitoa katika mkutano wa Jumuiya ya Wanawake wa chama hicho (UWT), kwamba watakaoshinda wawe tayari kufanya kazi na walioshindwa, inatajwa kuwa moja ya jitihada za kuepusha mgawanyiko ndani ya chama hicho. 

“Kikwete anakerwa na rushwa lakini kwa hali ilipofikia sasa, ni wazi kwamba hawezi kuzuia upepo wa kundi linalotajwa na kutuhumiwa kwa rushwa, “ kinaeleza chanzo chetu. 

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Rais Kikwete ameuona mwelekeo wa CCM si mzuri mbele ya umma, hivyo kutumia chaguzi hizo kama sehemu ya kutahadhalisha, kwamba kisipoangalia ‘kitaangukia pua’ katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

LOWASSA AZIDI KUTETEWA 

Wakati shutuma na tuhuma zinazomhusisha Lowassa zikitolewa sehemu tofauti, wapo wana-CCM wanaoamini kwamba kiongozi huyo ni jasiri na kwamba ana uwezo wa kuongoza. 

Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, Hussein Bashe, amekaririwa akisema Lowassa ni kiongozi mwenye uvumilivu na anayedhihirisha kuwa tayari kukabiliana na kuvishinda vikwazo, hivyo kustahili uongozi wa nchi.

Bashe ambaye jina lake lilitajwa katika tuhuma za rushwa wakati wa uchaguzi wa UVCCM mjini Dodoma hivi karibuni, alisema anajisikia fahari kuzifuata na kuzitekeleza siasa za Lowassa. 

Kauli hiyo ni tofauti na zile zilizowahi kutolewa na wanaojulikana kama ‘makamanda wa ufisadi’ akiwemo Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta na Waziri wa Ujenzi, Dk Harrison Mwakyembe.

Makamanda wa ufisadi wamekuwa wakiwataja matuhumiwa wa ufisadi ambao jina la Lowassa limekuwa miongoni mwao, kuwa wanastahili kufukuzwa uanachama na kunyimwa nafasi ya uongozi wa nchi.

www.ippmedia.com

No comments: