Wednesday, October 31, 2012

20 wauawa na wavamizi Nigeria

Wavamizi wamewaua watu 20 akiwemo kiongozi mmoja wa kijamii katika uvamizi waliofanya katika kijiji kimoja Kaskazini mwa Nigeria katika jimbo la Zamfara. 

Kwa mujibu wa afisaa mmoja mkuu wa jimbo hilo, wavamizi walivamia kijiji cha Kaboro na kuanza kuwashambulia watu kwa kuwapiga risasi kiholela.

Lengo la mashambulizi yao, ilikuwa wizi na baada ya kutekeleza kitendo chao, kwa kupora watu na kuiba mali yao,walitoroka. 

Takriban watu 23 waliuliwa mwezi Juni katika vijiji kadhaa jimboni humo na wavamizi. Baadhi ya waathiriwa walichinjwa. Katika eneo la Kaboro, mkuu wa kijiji, aliwataka wavamizi kukomesha vitendo vyao lakini badala yake walimshambulia. 

Gazeti la Tribune limeripoti kuwa wezi hao walikuwa wamejihami kwa bunduki aina za AK-47 wakiwa wanaendesha farasi na pikipiki, walivamia vijiji huku mashambulizi yakidumu saa mbili. Wapiganaji wa kiisilamu, wa kundi la Boko Haram wamewahi kufanya mashambulizi kadhaa Kaskazini mwa Nigeria lakini hakuna dalili kuwa mashambizi hayo yanahusiana. 

Nigeria ni mojawapo ya nchi zenye viwango vya juu vya uhalifu, na hutokea visa vingi vya mashambulizi na uvamizi ikiwemo utekaji nyara na wizi. Baadhi ya watu wamelazimika kuunda vikundi vya kujilinda dhidi ya uhalifu. 

bbcswahili
 

No comments: