Saturday, October 20, 2012

Ulimwengu walaani shambulizi la Beirut

Afisa mmoja mashuhuri wa kijasusi nchini Lebanon anayeupinga utawala wa Rais Bashar al - Assad, jana aliuawa katika mripuko mkubwa wa bomu la kutegwa ndani ya gari katika mji mkuu Beirut. Tukio hilo ni dalili nyingine inayoonyesha kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria vinaiingiza nchi hiyo jirani, Lebanon, katika mgogoro huo. Wissan al-Hassan, ambaye aliongoza uchunguzi uliozihusisha Syria na kundi la Hezbollah katika mauwaji ya Waziri Mkuu wa zamani Rafik al-Hariri, na watu wengine saba waliuawa jana wakati bomu liliporipuka katikati ya mji wa Beirut.

Upinzani wailaumu Syria 
Viongozi wawili wakuu wa Upinzani wamemlaumu Rais wa Syria Bashar al-Assad kwa shambulizi hilo, ambalo limeshutumiwa vikali na jamii ya kimataifa. Na Makundi mawili makuu ya upinzani nchini humo, baada ya mkutano wa dharula jana, yakaitaka serikali ya Lebanon kujiuzulu. Katibu Mkuu wa kundi la Future Movement, Ahmad Hariri alisema serikali ni sharti ijiuzulu na Waziri Mkuu Najob Mikati ni lazima aondoke. Marehemu Hassan alikuwa na uhusiano wa karibu na mwanawe Hariri, Saad, ambaye ni kiongozi wa upinzani na anayepinga utawala wa Assad. Waziri wa Habari wa Syria Omran al-Zohbi alilaani kile alichokitaja kuwa ni “shambulizi la kigaidi” akisema matukio kama hayo hayakubaliki kamwe. Saad Hariri na Walid Jumblatt, kiongozi wa chama cha Druze cha Lebanon, waliishutumu serikali ya rais wa Syria kufanya shambulizi hilo. Shutuma za jamii ya kimataifa, Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Marekani, Uingereza na Ufaransa wote wameshutumu shambulizi hilo. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon alivitaka vyama vyote vya Lebanon kutochochewa na tukio hili la kinyama. Nayo taarifa ya Mkuu wa Sera za Kigeni wa Umoja wa Ulaya Catherine Ashton ilisema waliohusika na uhalifu huo ni lazima wasakwe na kufunguliwa mashitaka. Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Hillary Clinton alilaani vikali shambilizi hilo, akisema kuuawa mkuu wa kijasusi wa jeshi la ndani la Lebanon, Jenerali Wissam al-Hassan ni dalili mbaya kuwa wale ambao wanaendelea kuhujumu utulivu wa Lebanon.

Brahimi yuko Damascus
Wakati huo huo, Mjumbe wa Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiarabu kuhusu mgogoro wa Syria, Lakhdar Brahimi amewasili mjini Damascus jana ambapo anatarajiwa kufanya mazungumzo ya kuweka chini silaha wakati wa siku kuu ya Waislamu, baadaye mwezi huu. Msemaji wa Brahimi, Ahmed Fawzi alisema mjumbe huyo wa amani atakutana na rais wa Syria, Bashar al-Assad hivi karibuni. Vyombo vya habari vya serikali viliripoti kuwa Brahimi atakutana na Waziri wa Mambo ya Kigeni Walid al-Muallem hii leo. Brahimi, anapendekeza mapigano yasitishwe kati ya serikali ya Syria na waasi wakati wa sherehe za siku kuu ya Kiislamu, Eid al-Adha, ambayo inaanza Oktoba 26. Serikali ya Syria na upinzani zimeelezea nia yao ya kuwa tayari kusitisha mapigano. Brahimi amewasili Syria baada ya kuzuru Saudi Arabia, Uturuki, Iraq, Misri, Lebanon na Jordan kutafuta uungaji mkono wa pendekezo lake. Pia alizuru Iran, mshirika mkuu wa utawala wa Assad. 

DW

No comments: