Sunday, November 4, 2012

Kikwete: Lowassa ni jembe

RAIS wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete, amemsifu Waziri Mkuu mstaafu na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, kuwa ni mbunge hodari sana, hivyo atashirikiana naye kumaliza tatizo la maji katika wilaya hiyo. 

Rais Kikwete alitoa sifa hizo kwa Lowassa jana wakati akihutubia wananchi eneo la Nanja, Kata ya Monduli, kabla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Minjingu –Arusha. 

Huku akishangiliwa na umati wa wananchi wa Monduli waliofurika kusikiliza hotuba hiyo, Rais Kikwete alisema anajua uhodari wa Lowassa na kuahidi kwamba atashirikiana naye kusaka fedha za kumaliza kero hiyo ya maji.

“Mhandisi wenu wa maji ametaja mipango mizuri sana ya kuondoa kero ya maji, lakini kwa suala la fedha hapo amefika kikomo kwani liko nje ya uwezo wake. Hilo niachieni mimi, nitatafuta fedha haraka ili tatizo hili liishe. Nitashirikiana na mbunge wenu, mnajua mbunge wenu ni hodari, tena hodari sana, nitashirikiana naye, naamini tutalimaliza tatizo la maji,” alisema Rais Kikwete. 

Alisema suala la maji ni kero ambayo serikali yake tangu ilipoingia madarakani na hata kwenye ilani yake, imeahidi kulishughulikia kwa nguvu zote. Alitaja kero zingine alizoahidi kuzimaliza kabla ya kuondoka madarakani kuwa ni pamoja na suala la miundombinu ya barabara, afya na elimu.

Hata hivyo wakati Rais Kikwete akimwaga sifa kwa Lowassa aliyepata kufanya naye kazi kama Waziri Mkuu wake, mwenyewe hakuwepo kwani yuko nchini Ujerumani kwa ajili ya uchunguzi wa afya yake. Katika hotuba ya Lowassa iliyosomwa kwa niaba yake na Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga, alimmwagia sifa Rais Kikwete kwamba chini ya uongozi wake, shule nyingi zaidi zimejengwa kuliko awamu zote za uongozi zilizopita. “Pili, kilomita za barabara za lami zimeongezeka wakati wa awamu yako kuliko wakati mwingine wowote. Nakupongeza na kukushukuru sana. 

“Kwa hakika umetekeleza vizuri, kikamilifu na kwa uadilifu Ilani za uchaguzi za CCM za mwaka 2005 na 2010. “Sisi wananchi wa Monduli ni mashahidi wa jambo hili. Tunaamini ndivyo ilivyo nchi nzima, na ndiyo maana wana CCM wiki mbili zijazo tunaenda Dodoma kuidhihirishia dunia na Watanzania wenye mashaka, kwamba tunahusudu utendaji kazi wako, tunakuamini na kuthamani uongozi wako,” alisema Lowassa.

Mbunge huyo wa Monduli alimshukuru rais kwa kuzindua miradi ya maji wilayani humo, lakini alisikitika kwa kutokuwepo kwani yuko nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu ya macho. Rais Kikwete amehitimisha ziara yake mkoani Arusha kwa kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Minjingu mradi utakaogharimu sh bilioni 98.511. 

www.freemedia.co.tz

No comments: