Monday, November 26, 2012

Lowassa: Nina utajiri wa watu si fedha

WAZIRI Mkuu mstaafu Edward Lowassa, amesema kuwa hana utajiri wa fedha bali wa watu. Lowassa ambaye pia ni Mbunge wa Monduli, alisema hayo jana katika Kanisa la Moravian Tanzania Usharika wa Ruanda, wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa hosteli ya wanachuo wa kike wa Chuo Kikuu cha Teofilo Kisanji mkoani Mbeya.

Alisema kuwa amekuwa akisingiziwa mara nyingi kuwa yeye ni tajiri jambo ambalo si kweli bali utajiri alionao ni wa watu ambapo anaamini kuwa hawezi kufilisika na kwamba ataendelea kuchangia kwenye harambee. 

“Nasingiziwa sana kuwa mimi ni tajiri, lakini utajiri wangu unatokana na harambee hizi ambazo zinachangiwa na marafiki na ninaamini sintafilisika,” alisema Lowassa huku akishangiliwa. 

Lowassa alifafanua kuwa upo usemi kwamba ukimwelimisha mwanaume ni sawa na kuelimisha mtu mmoja, lakini ukielimisha mwanamke ni kuelimisha taifa zima, hivyo kuchangia hosteli ya wanawake katika harambee hiyo ni jambo jema. 

“Wanafunzi mtambue kuwa wanaowasomesha wanajinyima, hivyo epukeni vishawishi na ukombozi wenu haupo kwa wanasiasa bali tumieni nafasi hiyo vizuri,” alisema Lowassa. 

Kabla ya kuanza harambee hiyo, aliongoza kuimba wimbo wa ‘Bwana Mungu nashangaa kabisa’, ambao alisema mara kadhaa amekuwa akiuimba kwa kuwa anafarijika akiusikia na kuuimba wimbo huo wa tenzi za rohoni. 

Naye Askofu wa Kanisa la Moravian Tanzania Jimbo la Kusini Magharibi, Alinikisa Cheyo, alisema kuwa ujenzi wa hosteli hiyo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 348 unatarajia kugharimu sh milioni 215.

Katika harambee hiyo, Lowassa alichangia sh milioni 25 ambazo alisema kuwa ni mkusanyiko wa michango ya marafiki zake na famiia yake pia. 

www.freemedia.co.tz

No comments: