Monday, December 24, 2012

LEO Trh 24 Disemba katika Historia

Leo ni Jumatatu tarehe 10 Mfunguo Tano Safar mwaka 1434 Hijiria inayosadifiana na tarehe 24 Disemba mwaka 2012 Miladia. Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita Libya ilijipatia tena uhuru wake baada ya kupasishwa Azimio la Umoja wa Mataifa na Muhamad Idriss al Mahdi kuteuliwa kuwa mfalme wa nchi hiyo. Huko nyuma Libya ilijulikana kwa jina la Tripoli na kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya himaya kubwa ya nchi za kigeni. Katika karne ya 16 Miladia Libya ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na jeshi la Othmania. Aidha wakati wa kukaribia Vita vya Kwanza vya Dunia, nchi hiyo ilivamiwa na Italia lakini wananchi wa Libya wakapambana vikali na wavamizi hao wa Ulaya. Ilipofika katikati ya Vita vya Pili vya Dunia, Uingereza na Ufaransa zikaikalia kwa mabavu nchi hiyo, na hatimaye Libya ikarejesha uhuru wake mwaka 1951 Miladia.
Chanzo: irib

Miaka 147 iliyopita katika siku muafaka na leo, kundi la siri lililojulikana kwa jina la Ku-Klux-Klan ambalo liliitakidi kuwa watu weupe ni jamii ya watu bora na wa daraja la juu, liliasisiwa nchini Marekani kwa shabaha ya kupambana na watu wa jamii nyinginezo, khususan raia weusi. Hata kama kundi la Ku-Klux Klan lilipigwa marufuku miaka minne baada ya kuasisiwa kwake, lakini hadi kufikia sasa limeshafanya mauaji mengi dhidi ya raia weusi wa Marekani, kutesa, kuwaudhi na kutoa vitisho dhidi yao. 

Siku kama ya leo miaka 163 iliyopita, wanajeshi wa Ufaransa waliivamia ardhi ya Guinea nchi iliyo magharibi mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa kudhibitiwa na Ufaransa nchi hiyo tajiri kwa madini ya dhahabu. Kampuni ya Dhahabu ya Pwani iliundwa huko Guinea kabla ya uvamizi huo ili kuandaa mazingira ya kuingia kimabavu Ufaransa nchini humo.

Na miaka 488 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, aliaga dunia Vasco da Gama baharia na mvumbuzi mashuhuri wa Kireno. Vasco da Gama alizaliwa mwaka 1460 Miladia. Mwaka 1498 Miladia, baharia huyo wa Kireno alifanya kazi muhimu ya kuvumbua njia ya majini kutoka Ulaya hadi bara la Asia na India.

No comments: